Kilichoimaliza Simba Congo

21Jan 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kilichoimaliza Simba Congo

KILIKUWA ni kipigo kizito cha mabao 5-0 ilichokipata Simba dhidi ya AS Vita mjini Kinshasa nchini Congo DR.

Mabingwa wa Tanzania Bara, Jumamosi walikutana na kipigo hicho wiki moja tu baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya JS Saoura ya Algeria.

Huo ni mchezo wa pili wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba iliondoka nchini ikiwa na matumaini kibao ya kupata ushindi, lakini ilikuwa inajua kuwa inakwenda kupambana na wanafainali wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliomalizika.

Ni kitu gani kilichosababisha Simba kupoteza mechi hiyo? Lakini pia ni kwa nini imepoteza kwa idadi kubwa ya mabao?

 

Woga wa mechi

Ni kama vile wachezaji wa Simba waliingiwa na woga kutokana na  sifa na rekodi ya AS Vita.

Rekodi ya kufika fainali ya CAF, pamoja na kutopoteza mechi  nyumbani kwao tangu mwaka 2017, iliwafanya wachezaji wa Simba kuanza mechi kwa taratibu kuonekana kuwahofia wapinzani wao kinyume na ilivyozoeleka.

Hiyo ilisababisha kufungwa bao la kwanza na lilipofungwa la pili, tayari wachezaji wa Simba walionekana kuondoka mchezoni na kuchanganyikiwa kiasi cha kuanza kufanya makosa madogo madogo yaliyowagharimu.

 

Wengi hawakuwa kwenye ubora

Wachezaji wengi wa Simba kwenye mechi hiyo hawakuwa kwenye ubora uliozoeleka. Ndiyo maana haikushangaza kuona Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, akimtoa Clautous Chama na kumwingiza Haruna Niyonzima.

Chama kwa sasa ni kama moyo wa timu ndani ya uwanja. Yeye ndiye anayeongoza timu icheze vipi, iende kushoto au kulia. Kitendo cha kutolewa, kilionyesha kuwa hakuwa kwenye ubora wake na maji yalizidi unga.

 

Manula, Gyan, Niyonzima waling'ara

Cha kushangaza kwenye mechi dhidi ya AS Vita, mchezaji ambaye anapigiwa kelele sana na mashabiki wa Simba kuwa huwa hachezi vizuri, Nicolaus Gyan ndiye aliyekuwa kwenye ubora wa hali ya juu kwenye mechi hiyo.

Ndiye mara nyingi alionekana akifanya vitu kwa usahihi, tofauti na wengine ambao mashambulizi yao walikuwa yakizuiwa kirahisi na mabeki wa upinzani.

Hata kwenye kukaba alijitahidi zaidi kuliko hata Mohamed Hussein Tshabalala.

Kipa Aishi Manula ambaye naye huwa analaumiwa sana na mashabiki wa Simba kwa kufungwa baadhi ya mabao ya kizembe, aliiokoa timu yake isibebeshwe kiroba cha mabao.

Aliokoa hatari nyingi ambazo mastraika wa AS Vita walikuwa  wakibaki wao na yeye, huku mashabiki wao wakiwa wameinuka kushangilia wakitegemea kabisa kuwa lingekuwa bao. Aliokoa kiasi cha hatari tano hivi ambazo zilitakiwa kuwa mabao.

Kiungo Haruna Niyonzima alipoingia aliituliza timu na kuanza kucheza soka lao lililozoeleka, lakini tatizo lilikuwa ni muda. Tayari Simba ilikuwa imeshapoteza mechi kwa idadi kubwa ya mabao, hivyo wachezaji walionekana wameshakata tamaa.

Huenda kama angeingia mapema wakati AS Vita inaongoza kwa mabao mawili, mambo yangeweza kuwa tofauti. Labda mabao matano  yasingefika.

 

Mabeki Simba bado majanga

Kama alivyowahi kunukuliwa kocha wa Nkana FC, Beston Chambeshi kuwa kitakachowakwamisha Simba kwenye hatua ya makundi ni  mabeki.

Akasema haoni kama ina walinzi imara watakaoweza kupambana na mastraika na mawinga wa timu zingine, hasa Waarabu. Kabla hata haijacheza na timu ngumu kutoka Uarabuni hususan Al Ahly, majibu yameshaanza  kupatikana.

Mabeki wa Simba wa kati na pembeni wote ni rahisi mno kupitika. Si wabishi, na wanaruhusu sana mastraika kuingia kwenye eneo la hatari kirahisi, pia mawinga kupiga krosi watakavyo.

Simba Jumamosi ilikutana na timu ambayo inaweza kutumia udhaifu huo kupata mabao.

Mastraika wa AS Vita alikuwa akiipita beki wa Simba wapendavyo na mawinga walikuwa wakipiga krosi kila wanapojisikia, kitu kilichokuwa kikiliweka goli la timu hiyo kuwa mashakani muda wote  wanapokwenda kushambulia.

Simba waliwazuia mara chache sana kuliko wao kupita na kwenda kumsalimia Manula.

Mabeki wa kati Simba walikuwa hawaruki kuzuia mipira ya krosi  ilipita na kuwakuta wapinzani wao. Kati ya mabao matano yaliyofungwa, mawili ya kona yalikuwa ni uzembe na mabeki kutoruka kuokoa.

Wafungaji walikuwa wakiruka peke yao na kukwamisha mpira  wavuni wakiwa kwenye rundo la mabeki wa Simba waliokuwa  wamesimama tu wakiutazama mpira ukiwapita juu ya vichwa vyao bila jitihada zozote.

 

AS Vita ni bora zaidi

Kiuwezo AS Vita ilionekana ni timu iliyokamilika zaidi kuliko Simba. Kila idara ilikuwa iko imara kuanzia golini, mabeki wa pembeni, wa  kati, viungo wakabaji na washambuliaji, hata mawinga, tofauti ya Simba ambao ina baadhi ya wachezaji tu ambao ni bora.

Hata waliokuwa wakiingia kipindi cha pili walionekana kuwa na uwezo mkubwa wakati mwingine zaidi kuliko hata aliyetoka.

Habari Kubwa