Kilichotokea kwa Seif, Lipumba hatima ya kilichoanza mwaka 2015

20Mar 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Kilichotokea kwa Seif, Lipumba hatima ya kilichoanza mwaka 2015

HATIMA ya Maalim Seif Sharif Hamad, sasa ni rasmi kuwa haiko ndani ya CUF bali amepewa makao mapya na chama cha ACT- Wazalendo kinachoongozwa na Kiongozi Mkuu Zitto Kabwe.

Seif anachukua hatua hiyo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutangaza rasmi kuwa Profesa Ibrahimu Lipumba ndiye Mwenyekiti halali wa CUF na kumshinda Maalim aliyempeleka mahakamani kupinga kushika wadhifa huo.

Muda mfupi baada ya kutoka mahakamani juzi, ambako alishindwa katika shauri lake la uongozi wa kisiasa dhidi ya Prof. Lipumba, Maalim Seif, alitangaza rasmi kujiunga na ACT –Wazalendo.

Jana Maalim Seif, aliyeambatana na Mwenyekiti Zitto Kabwe, katika makao makuu ya ACT-Wazalendo, Kijitonyama Dar es Salaam, walikuwa na tukio la kugawa kadi nyingi kwa wanachama wapya, wengi wanadaiwa wanatokea CUF.

Haya yanatokea ikiwa ni takribani miaka minne tangu wawili hao Profesa Ibrahimu Lipumba na Maalif Seif waanze kufarakana na katika siku za karibuni Profesa Lipumba anakumbushia kile kilichowagombanisha na kuwasambaratisha, akianza kwa kusema:

“Katika siku ambayo nilikasirika kidogo nirushe ngumi ni kwenye ule mkutano aliokuwa anauongoza Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif mwaka 2015, alituona CUF kama hatuna mkakati kuweka mgombea. Wakati hatujazungumza wala kukubaliana.”

Lipumba ambaye amekuwa kiongozi wa chama hicho kwa muda mrefu anasema hayo wiki iliyopo wakati akiwahutubia wanachama wa CUF katika Mkutano Mkuu, ambao ulimchagua kuwa Mwenyekiti wa Taifa, akipata ushindi wa kishindo wa kura 516 sawa na asilimia 88.

Makamu Mwenyekiti wa CUF Bara ni Maftaha Nachuma, aliyepata kura 231 sawa na asilimia 41.9 na Makamu Mwenyekiti Zanzibar ni Abbas Juma Muhuzi, aliyejizolea kura 349 sawa na asilimia 60.

Wakati akiwashukuru wanachama wa CUF baada ya kutangazwa mshindi anagusia tukio la kutaka CUF, licha ya kuwa mwasisi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), uliovijisha vyama vikuu vya upinzani, asishiriki kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, badala yake iachie majukumu hayo kwa Chadema.

Anakumbusha kuwa aliumia na kutamani hata kurusha ngumi kwa kuwa kitendo hicho anachokifananisha na kuvuliwa nguo hadharani.

Profesa Lipumba anakumbusha kuwa alifika katika kikao hicho kilichofanyika Dar es Salaam na kumkuta Maalim Seif, akizungumza na viongozi wa Chadema, kuwaeleza kuwa ni lazima wafanye maamuzi ya nani atakuwa mgombea wa urais.

Mwenyekiti mteule huyo, anawakumbusha wajumbe kuwa Maalim Seif alianza kuwahoji CUF iwapo wana mikakati na rasilimali za kutosha za kuwawezesha kugombea urais wa Tanzania mwaka 2015?

Lipumba anasema: “Maana ya kauli hiyo ni kwamba CUF hatuna mkakati wa kuweka mgombea urais kwa mwaka 2015. Anasema hayo wakati anajua kuna nia ya kuweka mgombea urais. Anakuja kunivua nguo hadharani. Hayo mambo yalikuwa ya kuzungumza kwanza na si kueleza kuwa sisi hatuna mpango wowote,” anasema Lipumba.

Profesa Lipumba ambaye mara kadhaa amekuwa akipeperusha bendera ya chama hicho kwenye urais, anasema walitakiwa wakubaliane, washauriane wenyewe ndani ya vyama vyao na si mtu mmoja kufanya maamuzi.

Anaongeza : “Tukakubaliana kesho tufanye kikao cha mashauriano asubuhi ofisini Buguruni. Tukamwita Maalim Seif, lakini baadaye akanitumia ujumbe kuwa amepata dharura. Lakini akaahidi kuhudhuria kikao cha saa 9 alasiri siku hiyo. Hii ina maana anataka tuende kwenye kikao cha Umoja wa Katiba ya Wananchi –Ukawa, bila ya kuwa na msimamo wa pamoja wa ndani ya CUF.”

Anaelezea kuwa alilazimika kumwambia Hamad kuwa iwapo hatakuja kwenye kikao cha Buguruni naye Lipumba hatashiriki kikao cha Ukawa.

Anakiri kuwa mbele ya wanachama hao kuwa ni kweli katika kipindi hicho ndani ya chama walikuwa hawajajipanga kikamilifu kuhusu mgombea, hivyo alikwenda kukutana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa pamoja na viongozi wengine wa chama kujadili zaidi na kukubaliana Dk. Slaa awakilishe Ukawa.

KUINGIA LOWASSA

Mwenyekiti Lipumba anasema wakati wamekubaliana na Dk. Slaa wenzao wa Chadema wakabadilisha gia angani na kumpitisha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, kuwa mgombea urais wa Ukawa.

“Hapa nilikuwa katika wakati mgumu nikajiuliza hivi kweli Lipumba nizunguke nchi nzima ninamnadi Lowassa kuwa huyu ni mpambanaji.”

“Huu mzigo wa kumnadi Lowassa kuwa ni kamanda wa kupambana na ufisadi Tanzania nikaona siuwezi, ndiyo sababu nikaamua kukaa pembeni.” Anasema Lipumba.

KUTOFAUTIANA NA HAMAD

Profesa Lipumba, anaeleza mambo ambayo walikuwa wanatofautiana na Katibu Mkuu Hamad na kutaja suala la Muungano, akisema msimamo wao ni kuunga mkono mapendekezo ya Tume ya Jaji Francis Nyalali kwamba mfumo utakaokidhi mahitaji yao kwenye Muungano ni ule wa shirikisho la serikali tatu.

Anasema walipokuja kwenye masuala ya kupendekeza mapendekezo ya kupeleka kwenye Tume ya Jaji Joseph Warioba iliyokuwa inakusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya, Maalim Seif akapeleka mapendekezo ya CUF kuwa wanataka Muungano wa mkataba jambo ambalo hawakukubaliana.

Profesa Lipumba akumbusha kuwa awali Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitaka Chadema ipewe nafasi ya kugombea urais na kama wakishinda nafasi ya Waziri Mkuu itatoka ndani ya CUF.

Anasema Maalim Seif aliliunga mkono na kueleza kuwa katiba ya Zanzibar chama kinachotoa Rais ndicho kinachotoa makamu wa Rais ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za serikali.

“Sisi hapa tunashirikiana kilichokuwa tunatakiwa kukifanya ni kuchagua mgombea ambaye wote wanakubaliana na kutekeleza malengo ya Ukawa,” anasema Lipumba.

Ukawa ni ushirikiano usiokuwa na malengo ya haki lakini ilivyoonekana wengine walikuwa na mkakati wa kuua vyama vya upinzani.

Anasema kama wangekuwa na mkakati wenye umoja ingesaidia kufikia yale malengo ambayo walikubaliana kuanzisha Ukawa, lakini matokeo yake baadhi ya vyama vililenga kuua vyama vingine, jambo ambalo hawakubaliana nalo.

VIPI SULUHU

Aidha, Profesa Lipumba anaeleza bayana kuwa Maalim Seif Sharif, si mtu aliyetaka suluhu katika mgogoro huo.

“Msuguano ndani ya chama ni matokeo ya Maalim Seilf kukataa suluhu jambo ambalo linaonyesha kuwa haitakii CUF mema,”anasema na kuongeza kuwa binafsi alikuwa tayari kwa suluhu na alishafuatwa na viongozi wa dini akawasikiliza, hivyo tatizo lilibaki kwa Maalim Seif.

Katika hilo anamrushia lawama kuwa chama hicho kimekosa nafasi za uwakilishi katika serikali ya Umoja wa Kimataifa, kutokana na misimamo ya Maalim Seif.

MIKAKATI MIPYA

Profesa Lipumba anasema maadamu amepewa rungu anakwenda kutibu chama na hatakuwa na msamaha na hao wanaoleta mgawanyiko.
Anayaeleza haya wakati akizungumzia mikakati yake baada ya kushinda nafasi ya uenyekiti kwa mara ya tano, na kusisitiza kuwa anakwenda kutibu majeraha yalitokea ndani ya chama.

“Atakayetaka kuyaendeleza tutamchukulia hatua kali.” Anaonya mwenyekiti huyu mzoefu.

“Ninakwenda kukisimamia chama na kuhakikisha kina kuwa imara ili kujiandaa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kiweze kupata ushindi.”

"Hii ni awamu yangu ya tano kushinda hii nafasi tuna changamoto kubwa, tumeingia katika mgogoro na huu mgogoro nimeuhesabu ni kama vile chuma kimepitishwa kwenye moto kikitoka salama kinakuwa chuma imara zaidi," anatamba Lipumba.

AOTA URAIS ZANZIBAR

Anaongezea kuwa:"Tunakwenda kutibu majeraha kwa haraka iwezekanavyo tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 lengo letu kubwa kwa upande wa Zanzibar ni kulinda katiba iliyotupatia serikali ya Umoja wa Kitaifa ili tuwepo katika serikali hiyo na tunataka kushinda uchaguzi wa urais na uwakilishi." Lipumba

Mwenyekiti wa CUF anasema kwa Tanzania Bara watahakikisha wanajenga chama chenye mvuto zaidi na msimamo wa chama ni haki sawa kwa wananchi wote.

Anawapa wajumbe wote waliohudhuria uchaguzi huo, kuhakikisha wanashiriki katika uchaguzi wa serikali za mtaa na kupata ushindi.

KUIGWA NA CCM

Aidha, Lipumba anasema, kuna sera zao ambazo zimechukuliwa na CCM, kama elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, na kwamba CUF iliitangaza tangu 1995.

“Sera ya kuhakikisha tunatumia rasilimali za nchi kama madini kwa manufaa ya nchi ni yetu tangu mwaka 1995 lengo letu sasa ni kuhakikisha haki sawa kwa wote zikiwamo za kiuchumi, kijamii na kisiasa tutayatekeleza kwa kuyajengea hoja,” anaahidi mwenyekiti huyu wa CUF.

Habari Kubwa