Kilio cha ‘Lumbesa’ na soko ‘kudoda’ chatawala

30Jun 2017
George Tarimo
Iringa
Nipashe
Kilio cha ‘Lumbesa’ na soko ‘kudoda’ chatawala

UKOSEFU wa masoko ya uhakika, unatajwa kuwa changamoto kwa wakulima wa zao la vitunguu,  wilayani Iringa.

Hicho ni kilio ambacho kila mpita njia atawasikia wakililama kuhusu masoko na gharama kubwa ya kuzalisha zao hilo.

Wakulima hao wanadai kushindwa kuhudumia mashamba yao, kutokana na kukosa masoko ya uhakika, hali imeyowaathiri kiuchumi na kisaikolojia.

Mkurugenzi Mtendaji

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Robert Masunya, anakiri Halmashauri inafahamu kuwapo ‘lumbesa’ na Sheria ya Wakala wa Vipimo ya Mwaka 2002, Sura ya 340, inayotoa mwelekeo kuhusu usimamizi wa mazao hayo.

“Kwa mfano, mahindi yanatakiwa gunia lenye ujazo usiozidi kilo 90, nyanya kwa ‘teka’ kilo 50, vitunguu kilo 70 na mchele kilo 100 na magunia mengi yanaweza yakaeleweka vizuri, kama ni ‘lumbesa’ au siyo ‘lumbesa.’

“Kama magunia yamezidi ujazo huo, maana yake ni ‘lumbesa.’ Wajibu wa serikali ni kusimamia Sheria hiyo ya Vipimo ya Mwaka 2002 na kuwataka wakulima wasiuze kwa uzito ambao unazidi hivyo vipimo,” anasema Masunya.

Masunya anasema serikali sasa inaelekeza uongozi wa vijiji na wananchi, kuzingatia sheria zilizoko kwenye manunuzi na anawataja wanunuzi kuwa wanawalazimisha wakulima kuuza kwa bei wanayotaka, pia kuweka mzigo wa ‘lumbesa.’

Ofisa Kilimo

Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Lucy Nyalu, anakiri kuwapo changamoto hiyo na kwamba, serikali inawahamasisha wakulima kulima kibiashara, ili kujihakikishia kipato pamoja na chakula cha uhakika.

Lucy anasema, wakulima wengi wanapoona fursa kwenye kitunguu, hulikimbilia kulilima, hali inayosababishia wakose masoko, kutokana na kuwapo ziada katika uzalishaji na kujienyesha kwenye soko.

Anasema kwa sasa, wanahamasisha wakulima kulima kilimo cha mkataba ambacho wanawa hamasisha kupitia kinachoitwa (SAGCOT).

“Sisi tunataka mkulima azalishe, lakini aingie mkataba na mnunuzi au wakulima hao waunde vikundi, ambavyo vitawasaidia kuuza kwa umoja walio nao kwa mnunuzi, ambaye wameamua kuingia naye mkataba. Kwa hapo, watakuwa na uhakika na masoko tofauti na kuuza mtu mmoja mmoja,”anasema Nyalu na kuongeza:

“Mfano mkulima ametumia gharama kubwa kuzalisha, lakini mavuno yake ni machache kwa kweli hii inawakatisha tamaa hata kama ingekuwa ni mimi na wangelima kwa mkataba, basi mnunuzi angeweza kusema niletee tani kadhaa ambazo zitamtosheleza matumizi yake,” anasema Nyalu.

Ni wakulima kutoka maeneo ya Kiwere wilayani Iringa, wanaodai kutekeleza mashamba, huku wakiilalamikia serikali kuweka ushuru mkubwa, kwenye mageti ya kupitishia mizigo yao.

Wakulima

Mkulima, Idhaa Allym, anasema kutokana na changamoto hizo, wengi wameathirika kiuchumi na kisaikolojia, kwani wamekopa kutoka kwenye taasisi za kifedha, kwa ajili ya mtaji wa kufanikisha kilimo, lakini wanaambulia patupu katika kile walichokizalisha.

Ally anasema kwamba, wanunuzi wamekuwa wakiwalazimisha wakulima kujaza magunia kwa mtindo wa ‘lumbesa,’ ili yanunulike, huku wakibakiwa na changamoto ambayo ni kikwazo kwa soko na mazao yanayooza shambani.

Mkulima huyo anasema mazao yao wanategemea kuyauza kwenye masoko mbalimbali kuazia Iringa, lakini hali iliyopo ya kukosa wanunuzi mkoani Iringa, wanalazimika kupeleka mazao jijini Dar es Salaam na Zanzibar, kote kukiwa na changamoto ya kupata mnunuzi.

Anasema kwa sasa wakulima wamelima vitunguu kwa wingi, akitoa mfano hai wa maeneo kama; Iringa, Mpwapwa, Ruaha Mbuyuni, Malolo, Idodomia na Msosa, ambako kote biashara ni mbaya, isipokuwa Singida ambako kuna soko la kimataifa.

 “Sisi tunatumia gharama kubwa kuanzia kuandaa shamba hadi kuvuna, lakini changamoto inakuja kwenye soko na ukiangalia wengi wetu wakulima tumechukua mikopo na mikopo hiyo tunashindwa kurudisha kutokana na mazao kutonunulika,”alisema Ally.

Chacha Omary, anadai kuwapo bei kubwa ya pembejeo za kilimo zenye gharama kubwa sana, kiasi cha wakulima wadogo kushindwa kumudu gharama hizo.
Omary anasema tatizo lililopo ni kwamba, wakulima wanaumia kwenye dawa wanazotumia shambani, kwani ni za gharama kubwa kuliko faida inayopatikana.

“Mfano ukiangalia jaluba moja unapanda kwa 500,palizi kwa jaluba 500,mpigaji dawa kwa jaluba 1,000 halafu unakuta umelima hekari mbili au tatu, bado hujamlipa mchora ramani wa shamba ambaye atachora ramani ili maji yaweze kuingia shambani vizuri na sio chini ya 350,000,” anasema.

Chacha anafafanua: “Mfuko mmoja wa mbolea Sh. 50,000, sasa ukiangalia shamba lina majaluba mangapi? Bado hujaweka matumizi mengine ya shamba, hivyo utakuta mkulima anaumia kiasi cha kukata tamaa ya kuacha kuendelea na shughuli ya kilimo.”

Ombi la mkulima huyo ni kwamba, serikali ipunguze gharama za pembejeo za kilimo, ili wakulima wadogo wamudu gharama za pembejeo hizo.

Mkulima Elizabeth Chilala, mwenye ekari mbili, anadai kutumia zaidi ya Sh. milioni 4.5, lakini ameambulia magunia 70 tu ya zao hilo, hali inayomkatisha tamaa ya kuendelea ukulima huo, kutokana na kukwazwa na gharama kubwa ya uendeshaji kilimo pasipo faida.

“Hapa nimelima ekari mbili. Nimetumia Sh. mil.4.5 na nimepata gunia 70 licha ya kwamba kanuni zote za kilimo nimefuata na kukokana na kukosekana kwa masoko ya uhakika vitunguu vyangu vitaozea shambani.”alisema Chilala na kuongeza:

“Matarajio yangu yalikuwa kila gunia niuze Sh.100,000 hadi Sh.150,000, lakini hali imekuwa tofauti na kulazimika kuuza kwa gunia moja Sh. 40,000 hadi Sh. 50,000 na kwa mkulima mdogo ambaye amekopa fedha, hawezi kuendelea na kilimo hiki,”anasema Chilala

Noah Juma ni mkulima anayesema alikodisha shamba kwa bei ya Sh.300,000 na kulima kwa trekta ni gharama kubwa kwa mkulima mdogo, labda kupitia msaada wa ng’ombe ,vibarua ambao ni gharama ya Sh.150,000 kwa ekari moja na upandaji jaluba ni Sh. 500 kwa ekari moja.

Anasema wakati kuna gharama hiyo kubwa, pia kuna zaidi ya Sh. 350,000 kwa ajili ya kulipia maji shambani na kuongeza kuwa hiyo kwao ni changamoto kubwa sana.

Habari Kubwa