Kilio cha kudhalilisha watoto Zanzibar bado ni kikubwa

16Jun 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Kilio cha kudhalilisha watoto Zanzibar bado ni kikubwa

KILA inapofika siku ya leo, yaani Juni 16, dunia huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.

mtoto anaodaiwa kubakwa na baba yake wa kambo, akiwa nyumbani, walipozungumza na mwandishi wa makala hii. (PICHA NA RAHMA SULEIMAN)

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Ubakaji na Ulawiti kwa Watoto Unaepukika, Chukua Hatua Kumlinda Mtoto.’

Zanzibar kunaelezwa hivi sasa kuwa miongoni mwa maeneo ambayo si shwari katika mustkabali wa matukio ya ubakaji. Tayari kumeripotiwa na matukio mengi ya udhalilishaji kijinsia kwa watoto

Hilo limewafanya wazazi na walezi kuwa na hofu kubwa kuhusiana na usalama wa watoto wao, maana ni vitendo vilivyoshamiri kila kona.

Inaelezwa kuwa, jambo la kusikitisha ni kwamba wanaotenda hayo kwa kiasi kikubwa, ni watu wazima na jamii ya karibu wa uhusiano, kama vile mzazi, kaka, mjomba au jirani.

USHUHUDA

Mama mmoja (jina linahifadhiwa) katika kufafanua kilichomkuta, alijikuta anashindwa kuanza simulizi kwa kuangusha kilio, baada ya kupewa taarifa watoto wake watatu wamebakwa na mume wake, ambaye ni baba wa kambo wa watoto hao.

Mama huyo ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Kati, Unguja, anasimulia mkasa wake akisumulia namna mumewe alivyowabaka watoto wake aliowazaa kwa mume mwingine

“Sijaamini kama mume wangu angeweza kunifanyia kitendo hiki cha kinyama, kunibakia wanangu” anasema mama huyo, huku akibubujikwa na machozi.

Anasimulia kwamba, siku moja akiwa ametoka na kwenda mbali kidogo, alipigiwa simu na mdogo wake akipewa taarifa hiyo, kuwa mwanawe 11 amebakwa na baba yake wa kambo.

“Baada ya kupewa taarifa mtoto wangu kabakwa, nilipanga safari ya kurejea nyumbani. Kabla sijafika nyumbani, mume wangu alinipigia simu ni kuniuliza ‘unarudi saa ngapi,’ nilimjibu nisubiri nipo njiani narudi,” anasema.

Anaendeleza simulizi kwamba baada ya kufika nyumbani hakumkuta mumewe, tayari alishatoroka, huku yeye akiamua kumchukua mtoto kwenda naye katika Kituo cha Polisi kuripoti shauri hilo.

Mama huyo anasema baada ya kupata maelezo ya Polisi, waliongozana na askari naye askari mmoja hadi katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, kwa ajili ya uchunguzi wa daktari na ikathibitika kuwa mtoto alibakwa.

Baada ya kumueleza daktari kwamba mbakaji ni mume wake, tabibu huyo alimshauri watoto wengine nao wachunguzwe, ili kufahamu usalama wao na lilipofanyika hilo, ilibainika nao wamebakwa.

Mama huyo anasema kwamba, baada ya kuwahoji watoto kutaka kujua mtu aliyewatendea hilo, wote walikiri kwa pamoja ni baba yao.

Mama anasema hiyo ndio ilimfanya agundue kwamba mumewe alikuwa akitumia fursa anapoondoka, kufanya ubakaji nyumbani.

Anaendeleza simulizi kwamba: “Mimi ni mfanyabiashara ndogondogo. Nikitoka asubuhi nyumbani na kwenda katika biashara zangu na ninarudi jioni, kumbe hutumia mwanya nikiwa sipo ananidhalilishia wanangu.”

WATOTO WASIMULIA

Watoto hao wenye umri kati ya miaka 10 na 16, wanasema walibakwa na kisha walitishiwa iwapo wangetamka lolote kuhusiana walichotendewa.

“Baba ameshanifanyia mara nyingi na aliniambia nikihadithia kitendo anachonifanya, ataniua! Ndio maana nikashindwa hata kueleza chochote kwa mama,”anatamka mtoto mmojawapo.

Anasimulia mkasa akisema, mara ya kwanza alifanyiwa kitendo hicho kwa kuambiwa ana matatizo mwilini na alitaka kummfanyia matibabu. Ni maelezo yaliyofanana na ya ndugu zake wawili

KAULI YA POLISI

Mkuu wa Dawati la Jinsia wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Khadija Haji Khatibu, anakiri kufahamu tukio hilo lililoripotiwa katika dawati lake hivi karibuni.

Khadija anatumia fursa hiyo kwa wazazi kujenga mazoea ya wenzake, kuwa karibu na watoto wao kuwaelimisha juu ya namna ya kukabiliana na woga na mwenendo usiofaa.

Anasema kupitia dawati lake, kuna jumla ya kesi 16 za udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto ambazo zimeripotiwa katika mkoa wa Kusini Unguja, ikiwamo watoto kubakwa na kupewa ujauzito.

Mkuu huyo wa Dawati la Jisnia anasisitiza kwamba, ili kukomesha vitendo vya aina hiyo, kunapaswa kutolewe adhabu kali na kuwa fundisho kwa wote wanaoendekeza tabia hiyo.

SERIKALI
Mkurugenzi Idara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Wahida Maabadi Mohammed, anasema kuwa jitihada za pamoja zinahitajika kupinga udhalilishaji huo wa watoto, kuwawezesha kuishi na kukua vizuri.

Anatahadharisha kwamba vitendo hivyo vikiachiwa, ni mwenendo wa kulifanya likose taarifa likose mwelekeo wa taifa linakoenda.

Wahida anajitambulisha kuwa shuhuda wa vitendo vya udhalilishaji vinavyowaathiri watoto wa Zanzibar, hali inayowanyima raha watoto kuwa na maisha ya kusoma kwa amani.

Mkurugenzi huyo anaitaka jamii kubadilika na kuondokana na muhali, jambo alilolisema linarudisha nyuma jitihada za kutokomeza vitendo hivyo.

WAZIRI ANENA

Waziri wa Kazi,Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Castico, anaeleza kushangazwa na kuwapo hukumu chache za kesi za udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Anasema sehemu kubwa ya kesi hizo zimekuwa zikiripotiwa katika katika mamlaka za kisheria ikiwamo mahakamani, zinazotolewa hukumu ni chache.

Waziri anasema kuna kesi 96 za udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto, ambazo ziliripotiwa mwaka juzi na katika hizo, ni kesi 29 (Asilimia 30.2) tu ambazo zilizotolewa hukumu. Kati ya hizo, kesi 24 zilitupiliwa mbali na mahakama na waliochukuliwa hatua ni watano tu.

Castico anasema bado kuna changamoto nyingi zinazokwamisha mikakati ya kumaliza udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar.

Anasema mwaka jana kulikuwapo kesi 49 za udhalilishaji zilizofunguliwa katika mahakama za Visiwani na kati ya hizo, kesi mbili tu( asilimia nne) ndizo zilizopatiwa hukumu.

“Kwa upande wa Mahakama ya Watoto, jumla ya kesi 64 zilifunguliwa mwaka 2015 na kati ya hizo, kesi 55 zilitolewa maamuzi na kuna kesi tisa zinaendelea,” anasema Castico.

Waziri huyo anaongeza kwamba, ni hali inayosikitisha na inayovunja moyo, kwani kuna kesi chache tu zinazopatiwa hukumu, hali inayosababisha kuzidi kuongezeka vitendo vya udhaililshaji wa kijinsia Visiwani.

Anapendekeza baadhi ya sheria zifanyiwe marekebisho, akisema anaami sheria hizo ni kandamizi, hali inayowapa mwanya wahalifu wa udhalilishaji wa kijinsia wasinaswe na mikondo ya sheria.

Castico anataja sehemu mojawapo anayoona ina kasoro ni kwenye ushahidi wa mazingira, akisema ni jambo linaloleta ugumu katika kufanikisha utoaji ushahidi, kwani hufanyika kwa usiri mkubwa na kuleta ugumu katika kuwatia watuhumiwa hatiani.

Habari Kubwa