KILIO MIMBA ZA UTOTONI

03Dec 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
KILIO MIMBA ZA UTOTONI
  • Ulawiti, ubakaji… wanafunzi kuhadaiwa juu

NOVEMBA 25 mwaka huu, kama ilivyo wakati wote kila mwaka ni mwanzo wa siku 16 za harakati za dunia za  kupinga ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu.

Kipindi hiki kila taifa huzinduana kushiriki kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia, ambazo pia zinatambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Katika kutimiza azma hiyo, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kiliungana na serikali na wadau wengine kutetea haki za binadamu kwa kuzindua maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Nchini, kampeni za siku 16 zimeanza na zinatarajiwa kufikia kilele wiki ijayo Desemba 10, huku kauli mbiu ikiwa ni “Funguka! Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto Haumuachi Mtu Salama. Chukua Hatua.

Maadhimisho hayo ambayo yanafanyika kote duniani kufuatia kauli mbiu hiyo inalenga kuwakumbusha watu wote wazazi, walezi, ndugu, jamaa na jamii kwa ujumla kushirikiana na serikali kuvitolea taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia.

Katika uzinduzi, Mkurugenzi wa Tamwa, Eda Sanga, anasema lengo la kampeni hiyo ya siku 16 ni kuhakikisha wanaofanya vitendo hivyo wanachukuliwa hatua stahiki.

Anasema vitendo hivyo ambavyo vimeshamiri kwa wanawake na hasa watoto wa kike, vinasababisha kukatiza ndoto zao na kuwakomisha kufikia hatma.

"Tamwa tunaungana na mashirika mengine nchini kupinga ukatili wa kijinsia na kuzuia matukio haya. Kauli mbiu inawakumbusha wote, wadau na jamii kwa ujumla na kushirikiana na serikali, kutoa taarifa na kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia ambao unasababisha mabinti na wanawake kupoteza ndoto zao," alisema.

Sanga anasema pia lengo la kutangaza siku hizo 16 za kupinga ukatili kunakusudia pia  kuishawishi serikali na jamii kutoa taarifa za matukio yanayohusu ukatili wa kijinsia.

“Tunachotaka kuona ni vitendo hivi vinamalizika mitaani kwa sababu wanaofanya hivyo ni ndugu zetu, jamaa na marafiki ambao wanatuzunguka. Kama tukielimishana ni rahisi kuwafichua wanaofanya ukatili ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa,” anaongeza.

Ubakaji waongezeka

Sanga anasema kwa mujibu wa takwimu zilizo kusanywa  na Tamwa katika ofisi zao kupitia kitengo cha Usuluhishi cha CRC, imebainika kuwa ukatili wa kijinsia hasa ubakaji umeongezeka kwa watoto.

Anasema katika kipindi cha miezi minane kuanzia Januari hadi Agosti mwaka 2016, kesi zilizohudumiwa katika kituo hicho zilikuwa ni tisa wakati kwa kipindi kama hicho mwaka huu 2017, vitendo vimeongezeka na kufikia 57.

“Kwa takwimu hizi inadhihirisha wazi kuwa, matukio ya ukatili yanazidi kushamiri maeneo mbalimbali nchini hususani Dar es Salaam, ambako tumepokea taarifa za matukio haya,” anasema.

Aidha, anasema katika Kituo cha One Stop Centre cha Hospitali ya Amana  Dar es Salaam, takwimu zinaonyesha kuwa, kiwango cha ubakaji kwa mwaka huu kiko juu kwa idadi ya watoto 141 walio chini ya umri wa miaka 18 ukilinganisha na idadi ya watu wazima 27.

Anasema taarifa hiyo imeonyesha kuwa kuanzia Julai 2016 hadi Juni 2017 wanawake 168 walibakwa.

Sanga anasema kituo hicho pia kimehudumia jumla ya waathirika 420 ambao kati ya hao watoto ni 316 sawa na asilimia 75 na watu wazima ni 104 sawa na asilimia 25 ya ukatili wa kijinsia.

Ulawiti

Anaitaja taarifa hiyo kuwa inaonyesha kuwa idadi ya waliolawitiwa na kuripoti katika kituo hicho ni 44 sawa na asilimia 10.47 kati ya hao watoto ni 39 ukilinganisha na watu wazima ambao watano  kwa mwaka.

“Hali hii ya ukatili iko juu kwa sababu watoto waliofanyiwa vitendo hivi wana uwezekano mkubwa wa kuwafanyia wengine katika kipindi cha makuzi yao,” anaonya  Sanga.

Anaeleza zaidi kuwa, Tamwa inaamini kuwa jukumu la ulinzi na malezi bora kwa watoto ni la jamii nzima wakiwemo marafiki, wazazi, ndugu, walezi na majirani.

Anasema pia viongozi wakishirikiana na serikali kuboresha na kusimamia utekelezaji wa sera na kubadilisha sheria kandamizi ili wahusika wa ukatili huo hasa kwa watoto wa kike wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.

Wanaume wahusika ukatili

Gladness Munuo ni Mkuu wa Kituo cha Usuluhishi Tamwa CRC, anasema kasi ya kuripotiwa kwa matukio hayo ya ukatili inaongezeka na kwamba wengi wanaoripoti kufanyiwa vitendo hivyo ni wanawake.

Anataja sababu za takwimu hizo kuongezeka kila mwaka kuwa  ni kutokana na jamii kuelimika kuhusu matukio hayo.

Pia anasema wanaofanyiwa vitendo vya ukatili si tu wanawake na watoto bali wanaume nao wanafanyiwa isipokuwa ni wagumu kuripoti.

Munuo anasema, vitendo wanavyofanyiwa wanaume ni pamoja na kunyimwa chakula ili hali wanaacha fedha na katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam aina ya ukatili unaofanywa ni wa kunywa pombe, kudhalilisha familia na vipigo kwa wanawake na watoto.

Munuo anatumia fursa hiyo kuwataka wanaume kujitokeza kutoa taarifa kuhusiana na matukio wanayofanyiwa na wake zao.

“Si kwamba kesi zote zinazoletwa hapa tunapelekana polisi au mahakamani nyingine zinaishia  hapa kwa kukaa pamoja na kusuluhisha,” anasema Munuo.

Wanafunzi waathirika zaidi

Mkurugenzi wa Kitengo cha Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Eugenia Kafanabo, katika utafiti wake alioufanya mwaka 2015 katika shule 40 uliohusisha wanafunzi 4,000, ulibaini kuwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari na walimu walezi, madereva bodaboda, wauza chips na vijana wa mitaani, wametajwa katika kundi la watu wanaohusika kufanya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanafunzi

Anataja aina ya unyanyasaji wanaofanyiwa wanafunzi hao ni kunyimwa chakula na 1,268 walikiri kufanyiwa vitendo hivyo na wazazi au walezi wao wanapokwenda shule au baada ya kurudi nyumbani.

Dk. Kafanabo anasema wanafunzi 663 walikiri kupigwa na wazazi au walezi wao bila sababu za msingi na wengine 531 walikiri kusumbuliwa kwenye uhusiano na walimu, wazazi, wafanyakazi, watu wa mitaani na wanafunzi wenzao.

"Katika utafiti wangu huu ambao niliwapa wanafunzi madodoso na kuyajaza moja kwa moja walikiri wazi kufanyiwa vitendo vya kikatili na kwa asilimia kubwa hawana pa kwenda kuripoti kwa sababu ya woga na kuhofia kuchukuliwa hatua zaidi," anasema.

Anaeleza zaidi kuwa wanafunzi 1,334 walikiri walimu wakuu wa shule kuhusika kufanya vitendo hivyo na 993 waliwataja walimu walezi, 240 wanafunzi wenyewe na jumla ya wanafunzi wa kike 1,822 walifanyiwa vitendo hivyo.

Pia anataja wanafunzi 909 waliwataja vijana wa mitaani na bodaboda na 377 waliwatuhumu wauza chips na makondakta wa daladala.

Dk. Kafanago anasema pia jumla ya wanafunzi 994 walisema wanaowasumbua kwenye mahusiano ni wazazi wao wa kiume na wageni ambao walitajwa na wanafunzi 257, majirani, dada na kaka zao.

Kadhalika anaeleza kuwa zaidi ya watoto wa kike milioni 14.2 duniani ikiwamo Tanzania, kila mwaka wanaolewa wakiwa na umri mdogo kitu ambacho ni hatari kwa jamii hiyo.

Anayataja mataifa mengine yanayoongoza kwa unyanyasaji wa watoto na mimba za umri mdogo ni pamoja na Ethiopia, Kenya, Asia na Bangladesh.

Anasema sababu zinazochangia tatizo hili ni sheria za baadhi ya nchi hizo huruhusu mabinti kuolewa wakiwa na umri wa miaka 14, mila na desturi pamoja na umaskini.

 

 

 

Habari Kubwa