Kimiti asimulia Mwalimu Nyerere alivyonusuru Muungano kuvunjika

15Oct 2023
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kimiti asimulia Mwalimu Nyerere alivyonusuru Muungano kuvunjika

MIAKA 24 imetimia tangu mwasisi wa taifa la Tanganyika na baadaye Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alipofariki dunia katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas , London nchini Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kuondoka kwa kiongozi huyo aliyejitolea kwa moyo wote kupigania ukombozi wa taifa hili kujitawala kutoka katika makucha ya wakoloni, lilikuwa pigo kwa Tanzania. Pia Afrika na dunia nzima iliomboleza ndiyo maana mazishi yake yalikuwa makubwa na yalivuta watu wengi.

Wakati leo ikiwa ni kumbukumbu ya kifo chake, jina la Nyerere limekuwa katika akili na mioyo ya watu kutokana na ama kufanya kazi naye alipokuwa Rais wa nchi au mwenyekiti wa chama tawala TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Miongoni mwa watu ambao bado wana kumbukumbu ya mambo kadhaa yaliyofanywa na Nyerere ni Paul Kimiti ambaye alishika nafasi mbalimbali zikiwamo uwaziri, ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ubunge na ukuu wa mkoa. Kimiti alitumika katika nafasi hizo kwa awamu tofauti kuanzia awamu ya kwanza chini ya Nyerere hadi awamu ya tatu, Benjamin Mkapa akiwa Rais na mwenyekiti wa CCM.

Yako mengi ambayo mwanasiasa huyo mkongwe anayakumbuka lakini kubwa zaidi ni tukio la mwaka 1993 lililoibuka bungeni (wakati huo vikao vya Bunge la Bajeti vikifanyikia Karimjee, Dar es Salaam). Tukio hilo ni la kuibuka kwa kundi la wabunge 55, maarufu kama G-55. Kundi hilo liliundwa na wabunge waliokuwa machachari wakati huo wakiongozwa na Njelu Kasaka (marehemu) aliyekuwa Mbunge wa Chunya na baadaye Lupa mkoani Mbeya.

Wabunge hao waliibua hoja ya kutaka kuundwa kwa serikali ya Tanganyika na waliwasilisha hoja bungeni kuhusu azma hiyo huku wakitia saini kuwa wanataka mchakato huo kufanyika haraka.

Mbali na Kasaka, wabunge wengine walikuwa Lumuli Kasyupa, William Mpiluka, Mateo Qaresi, Jared Ghachocha, Dk. Mganga Ole Kipuyo, Philip Marmo, Arcado Ntagazwa, Patrick Qorro, Japhet Sichone, Jenerali Ulimwengu, Abel Mwanga, Prof Aron Massawe, Shashu Lugeye na Sebastian Kinyondo.

Wengine ni Phares Kabuye, Mbwete Hombee, Kisyeri Chambiri, John Byeitima, Mussa Nkhangaa, Abdallah Saidi Nakuwa, Edward Ayila, Dk. Ndembwela Ngunangwa, Mathias Kihaule, Adamu karumbeta, halimenshi Mayonga, Dk. John Katunzi, Ismail Iwvata, Tobi Mweri, Aidan Livigha, Tabitha Siwale, Obel Mwamfupe, Othman Mpakani, Evarist Mwanansao, Paschal Degera, Erasto Losioki, Charles Kagonji, Nassoro Malocho, Venance Ngula na Benedict Losurutia.

Katika kundi hilo walikuwapo pia Dk. Degratius Mwita, Phineas Nnko, John Mwanga, Chadiel Mgonja, Guntram Itatiro, Paschal Mabiti, Edith Munuo, Luteni Kanali John Mhina, Raphael Shempemba, Balozi George Nhigula, Christian Fundisha, Samuel Kinuno, Rajab Kombo, Samuel Luangisa na Maria Kamm.

KUMBUKUMBU YA KIMITI

Akizungumza katika mahojiano maalum nyumbani kwake, Dar es Salaam, hivi karibuni Kimiti alisema kipindi hicho kilikuwa cha mtikisiko kwa taifa na baadhi ya Watanzania waligawanyika na kutokuwa na uhakika kuhusu nini kitatokea.

Kwa mujibu wa Kimiti, kundi hilo la G55 lilikuwa na hoja kuu ya kutaka iundwe serikali ya Tanganyika na iwe na madaraka kamili kama Zanzibar, hivyo kuwe na serikali tatu badala ya muundo wa serikali mbili ulioanza mwaka 1964 baada ya Zanzibar na Tanganyika kuungana na kuanzishwa kwa taifa la Tanzania.

“Kwa asiyejua faida za Muungano alitaka iwe hivyo lakini hawakujua athari gani zingetokea kama mchakato ungefanyika na hatimaye azma hiyo kutimia. Kwa kweli wengi hawakujua mpaka Nyerere alipokuja kulisemea. Aliitisha NEC na kueleza athari zake,” alisema.

Kimiti alibainisha kuwa katika mkutano huo wa NEC uliofanyika Dodoma, Nyerere aliweka wazi kwamba kuwapo kwa serikali tatu ilimaanisha kuvunjika kwa Muungano kwa kuwa Zanzibar ingebaki peke yake na Tanganyika ingebaki peke yake.

“Nyerere alikwenda mbali zaidi aliposema baada ya kuvunjika kwa Muungano, dhambi hiyo yas ubaguzi ingeendelea kwa Zanzibar pia kutengana kwa misingi ya Pemba na Unguja. Kwa Tanganyika pia ingekuwa hivyo. Watu wangejitambulisha kwa njia za ukabila na ukanda, hivyo Tanganyika isingekuwapo,” alisema.

Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Mbunge (wakuu wa mikoa walikuwa wabunge wa taifa kutokana na nafasi zao) alisema Nyerere katika mkutano uliofanyika Kilimani Club, Dodoma, aliweka wazi kwamba mpango wa kuanzishwa kwa serikali ya Tanganyika ambalo Bunge lilipitisha azimio, ulikuwa unavunja Muungano moja kwa moja, hivyo suala hilo halikubaliki. Alisema Nyerere aliendelea kulikemea mara kwa mara na hatimaye kuzimika kabisa.

UCHAGUZI 1995

Mwaka 1995 Tanzania ilifanya uchaguzi mkuu wa kwanza wa Rais na Wabunge uliohusisha vyama vingi vya siasa ikiwa ni takriban miaka mitatu tangu kuasisiwa kwa mfumo huo nchini, mwaka 1992.

Wakati wa vuguvugu la uchaguzi huo, Kimiti alisema Nyerere alikuwa mgeni rasmi katika moja ya sherehe za kitaifa zilizofanyikia Mbeya wakati huo yeye akiwa mkuu wa mkoa huo.

“Nakumbuka mwaka ule aliyekuwa Rais, Mzee Ali Hassan) Mwinyi, alikuwa anamaliza muda wake wa uongozi wa vipindi viwili vya urais, hivyo ilikuwa nafasi kwa wana CCM kujitokeza kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kugombea ili kumpata mtu wa kumrithi Mwinyi. Kwa kweli wanachama wengi kiasi (walikuwa 15) walijitokeza kuchukua fomu kuomba ridhaa ya chama kuteuliwa kugombea urais ili kuchuana na wale wa kutoka vyama vingine.

“Nyerere alipofika Mbeya nakumbuka aliniuliza ‘Paul kwa nini hujachukua fomu kuomba kugombea urais?’ Nilimjibu kwamba kamkono kangu (uwezo) kadogo maana watu wanahonga. Lakini kingine nilichomwambia ni kwamba nimejipima na kuona hiyo nafasi ni kubwa kwangu na nimefikiria kwenda kugombea ubunge Sumbawanga Mjini.

“Wakati ule pia alikuwapo Njelu Kasaka na bila kusita alimwuliza kwa nini amechukua fomu kugombea urais. Hakuishia hapo alimwuliza kama amefanya hivyo ili akatimize azma yake ya kuvunja Muungano kwa kuanzisha Tanganyika,” alisema huku akibainisha kuwa jina la Kasaka lilikatwa mapema kama Nyerere alivyomwabia kuwa hatafanikiwa katika azma hiyo.

  • Kesho, katika mwendelezo wa mahojiano na Kimiti, anafichua alichoambiwa na Nyerere alipomteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.