Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mhandisi Mkazi wa mradi wa JNHPP, Lutengano Mwandambo wakati akizungumza na uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) uliotembelea mradi huo.
"Tunashukuru maendeleo ya mradi yanaenda vizuri mpaka kufikia mwishoni mwa Februari, mwaka huu, mradi ulikuwa umefika asilimia 83.3 na utakamilika kwa wakati kama ilivyokuwa imepangwa,” alisema.
Awali, Mkurugenzi wa Mitambo wa TRC, Heriel Makange aliyekuwa ameambatana na Meneja wa Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Umeme (SGR), walisema wamefurahishwa kuona kazi hiyo ambayo bwawa hilo litakwenda kuwa mkombozi kwenye upatikanaji wa nishati ya uhakika.
Akieleza umuhimu wa mradi wa JNHPP kwa TRC alisema kukamilika kwa mradi huo unaokwenda sambamba na reli ya SGR utasaidia kuendesha mitambo itakayotumika kwenye reli katika kuharakisha usafiri kwa Watanzania na kasi ya maendeleo nchini.
"Mradi huu ni mkubwa sana unaotekelezwa na serikali ya awamu ya sita kupitia TANESCO na hivyo tuna imani kubwa kukamilika kwake kutasaidia sana katika shughuli za uendeshaji mashine katika mradi wetu wa SGR na kukamilika kwa miradi hii kutaleta manufaa makubwa kwa taifa letu," alisema Makange.
Naye Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Elihuruma Ngowi, alitaja faida za kukamilika kwa mradi huo kuwa ni umeme wa uhakika, kuimarisha kilimo, uvuvi, utalii, miundombinu na usafirishaji.
Pia, utasaidia kuboresha huduma ya majisafi na salama ambayo yatawafikia wananchi na kuongeza kiasi cha upatikanaji wa huduma hiyo.