Kinachofanikisha wenyeji wa Kagera wasisukumwe kusaka chanjo watoto

14Jan 2021
Jaliwason Jasson
Bukoba
Nipashe
Kinachofanikisha wenyeji wa Kagera wasisukumwe kusaka chanjo watoto
  • Mratibu Chanjo: Elimu kama darasani
  • Kutishana, kuigana wenyewe kumesaidia

WIKI mbili zilizopita, safu hii ilikuwa na simulizi ya mafanikio ya huduma za chanjo katika Manispaa ya Bukoba yalivyovutwa nyuma kwa miezi kadhaa mwaka jana na kikwazo corona, iliyokuwapo nchini. Nini mzizi wa mkoa kukwea kilele? Pata simulizi ya kina.

WAZIRI aliyebeba dhamana katika Afya, Jinsia, Wazee na Watoto katika serikali ya awamu iliyopita, Ummy Mwalimu, katika hotuba yake ya makaridio ya mapato na matumizi mwaka 2018 /2019 bungeni, alianika namna ambavyo walipiga hatua katika huduma ya chanjo, kati ya Julai, 2018 hadi Machi, 2019.

Waziri alitamka, Mpango wa Taifa wa Chanjo unaohakikisha kuwapo vifaa vyote kwa kila mikoa na lengo ni kuhakikisha walengwa watoto wa umri chini ya mwaka mmoja wapatao 2,013,744 wanapata chanjo zote zinazotakiwa.

Alisema, takwimu zilizotolewa na mkoa au wilaya yoyote iliyoripoti kuishiwa chanjo au vifaa vyake, Wizara ya Afya ilichukua hatua na kuhakikisha huduma ya chanjo ya watoto chini ya mwaka mmoja, hata ikafanikiwa kwa asilimia 98 ya lengo lake.

Alisema, wizara iliendelea na ukarabati wa maghala ya kutunza vifaa chanjo yaliyopo Dar es Salaam, ikiwa sehemu ya kuanzisha uzalishaji chanjo nchini.

Katika hotuba hiyo, wizara ilitumia Sh. bilioni 13.9, kununua majokofu yanayotumia nishati ya jua 1,385 na kusambazwa katika halmashauri zenye uhitaji, pia vifaa vya kielektroniki (tablet) kutunza taarifa za chanjo katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya nchini.

Waziri Ummy alitaja mikoa iliyonufaika na majokofu ni Dodoma, Geita, Kigoma, Lindi, Tanga, Mtwara, Mbeya, Shinyanga, Songwe, Singida, Mara, Mwanza, Pwani na Kagera.

HALI ILIVYO KAGERA

Takwimu za kitaifa za mwaka 2015 zilionyesha Mkoa wa Kagera ulitoa chanjo kwa watoto asilimia 87.5 huku kitaifa kundi hilo walikuwa asilimia 75.7.

Mratibu wa Huduma ya Mzazi na Mtoto wa Mkoa wa Kagera, Neema Kyamba, anataja siri ya mafanikio ya chanjo, ni wanavyofuata ratiba za chanjo na kuzingatia wakati.

Neema anataja mzizi mwingine wa mafanikio ni huduma za mikoba wanazotumia kwa kuwafuata walioko mbali na anawasifu kinamama wa mkoa kuwa waelewa wa chanjo, wanaozingatia upatikanaji wake.

Pia mtaalamu huyo ambaye anatoa elimu ya chanjo, anataja kingine kichachoukweza mkoa ni kuwafikisha vijijini watoa huduma.

Anasema, katika eneo hilo wanajitahidi kwa zaidi ya asilimia 90 wakizingatia watoto kupata chanjo pasipo kusukumwa na wataalamu, kazi kuu ikiishia kukumbushana chanjo.

Mratibu Neema anaeleza ushuhuda, wazazi wanaosaidia wenzao kwa kutoa elimu ya chanjo inayomwepusha mtoto na madhara ya magonjwa hatari, vivyo hivyo kila kituo kimejiwekea ratiba ya madarasa ya kinamama kufanikisha chanjo za watoto.

Neema anadokeza maeneo muhimu ya masomo, yanagusa stadi za usafi, chanjo, lishe na namna mama anamwachia mtoto muda, kabla ya ujauzito mwingine.

Anasema huwa wanafanya tathmini kila mwezi, wakishirikiana na watoa huduma kwa kukagua mafanikio ya mikakati ya iliyowasaidia na kupanua wingi wa ufuatiliaji. Unapotokea mkwamo, wanadadisi chanzo chake.

Mratibu anadokeza baadhi ya magumu yanayowakwamisha, ni usafiri katika nyendo zao, pale wanapokutana na jiolojia ya milima, mabonde, pia adha ya mvua na maeneo yasiyofikika kirahisi.

WAZAZI WAFUNGUKA

Mkazi wa Mtaa wa Nyakanyasi mjini Bukoba, Katushabe Rwekaza, anasema katika jamii ya wenyeji hao sasa kuna mwamko mithili ya mila, mama hata anapojifungulia kijijini, mtoto anawahishwa kwenye chanjo.

Anasema, ni wajibu unaochukuliwa na jamii inayomzunguka wakimpeleka mtoto kwenye kituo cha afya akapatiwe chanjo.

Katushabe anaendelea: “Tunaogopa sana kukaa na mtoto bila kupatiwa chanjo tunafikiri atapata magonjwa ndio maana tunamkimbiza mtoto zahanati."

Anaeleza zamani wazazi walipuuza kuwajibikia huduma ya chanjo iliyopo kwa watoto wao, lakini ushuhuda wa matukio ya vifo katika jamii yao na elimu inayotolewa na wahudumu wa afya, sasa imeleta mabadiliko ya kitabia sasa wanawahi zahanati kupata chanjo.

Diana Richard, mkazi wa Kibeta Bukoba, anaunga mkono uhalisia kwamba hivi sasa kuna mafanikio kwenye chanjo, kwa kuwa wataalamu wa afya wanawapatia elimu ya kutosha.

Anasema, licha ya chanjo za watoto zinafanywa kwa sindano zenye maumivu makali makali kwao, bado haijawa kigezo cha kuwakatisha tamaa, kwani wanatambua vyema thamani yake kiafya.

Mama huyo anataja faida mojawapo ya chanjo, ni kuimarisha afya ya mtoto asipate magonjwa, akisifu
tabia kuwa wazazi wengi wa sasa wanarithishwa na watangulizi wao, kwa kujifunza kuwaona na safari za kliniki wakiwa na watoto wao.

Mkazi wa Katoma, Bantulaki Kalikawe, anatamka kwamba ‘suala la chanjo katika jamii halina ubishi’ akiwa na ufafanuzi linagusa afya ya mtoto na kumwandalia msingi imara kwa afya yake.

Kalikawe anatumia fursa hiyo kuishukru serikali kwa kutoa fursa za chanjo kwa watoto wao kwa wakati sahihi na anaikumbusha kwamba, isisahau pembezoni wanakoishi jamii za wafugaji wa Kagera, kwa huduma kuwafikia watoto wao.

Mkazi wa Kashai, John Magezi, anasisitiza suala la chanjo lina ulazima anaouita wa asili, hivyo wanajamii wana ulazima kupeleka watoto zahanati, vituo vya afya na hospitalini kwa ajili ya chanjo.

Kemilembe Rwegasira, mkazi wa Bugabo Bukoba, anataja mzizi wa mafanikio Kagera kufanya vizuri kwenye chanjo, ni kuwatumia watoa huduma wanaosaidiana na wataalamu afya wa zahanati, vituo vya afya na hospitalini.

Pia, anataja msukumo mwingine kutoka simulizi za mitaani kwamba “Watu huambizana kuwa ukienda nchi jirani ukakosa, kitambulisho Watanzania wengi hutambuliwa kwa ile chanjo begani,” kutokana na alama yake.

ASASI ZA KIRAIA

Mratibu wa Shirika la Community Development Initiatives (KCDI), Christine Nyangoma, anasema katika uboreshaji chanjo kwa watoto, huwa wanahamasisha kinamama kufikisha watoto wao kliniki.

Anasema, huwa wanaenda kliniki kuwapima watoto wakishirikiana na wataalamu afya. Hapo wanahoji kuhusu afya za mtoto na anapogundulika kupungua au kuongezeka uzito, wanadidisi mabadiliko hayo kwa ajili ya kuyafanyia kazi katika utoaji elimu afya.

Ofisa huyo anasema, kuna kipindi asasi yao iliamua kujenga zahanati katika Kijiji cha Kikukwe, Kata ya Kanyigo, wilayani Misenyi, lengo ni kuwasogezea karibu huduma za afya.
 

Habari Kubwa