Kinamama kurudi nyuma kunawaengua kutoka uongozi wa soko wanakotumikia

11Jun 2021
Yasmine Protace
Dar es Salaam
Nipashe
Kinamama kurudi nyuma kunawaengua kutoka uongozi wa soko wanakotumikia

KATIKA ngazi ya juu ya uongozi wa nchi, kuna ujumbe mzuri kwa umma pengo la uwiano wa uongozi kwa nafasi ya wanawake kitaifa; linapunguzwa kwa kasi katika zaka za uongozi uliopo sasa. Hata wenyewe wanakiri na kupigia makofi.

Kinamama wakiwajibika katika ujasiriamali sokoni. PICHA: MAKTABA

Wasifu huo unaporejeshwa katika uongozi wa kugombea katika soko la darajani lililopo Mtaa wa Matangini Kimara katika kata ya Saranga, jijini Dar es Salaam, una picha yake.

Nipashe ilifanya uchunguzi kugundua katika kipindi cha uchaguzi wa viongozi wa soko hilo na kugundua kinamama wamekuwa wakirudi nyuma kuwapisha kinababa katika jukumu hilo, katika namna ya kujishusha pasipo sababu ya msingi.

Ndio hali ya baada ya wafanyabiashara wanawake kuogopa kugombea nafasi katika soko hilo na kusema kuwa wao hawana uwezo kulisimamia soko na hivyo kutaka wanaume ndio wagombee nafasi hizo.

Inaelezwa kuwa, ni hali inayowaondoa wanawake katika uongozi kutokana na tabia yao wenyewe kutojitokeza kuwania, ingawa ipo historia za baadhi kujitokeza kuwania fursa hizo.

Juliana Juma, mfanyabiashara katika soko hilo, anasema wanawake wanaogopa kugombea nafasi kwa kukosa uwezo wa kuliendesha soko hilo la Darajani.

"Tatizo sisi wanawake hatupendani, tupo wengi sokoni lakini hawezi mwanamke akaomba nafasi na akapigiwa kura na wanawake wenzake," anasema.

Juliana analalamika kwamba kila uchaguzi unapotangazwa imekuwa vigumu kinamama kushirikiana sokoni Darajani, kuliko kuwapa nguvu wagombea kinababa wawania nafasi za uongozi.

Mama huyo anaasa haja ya elimu ya kujiamini kutolewa sokoni, ili kuwajengea fursa kushika nafasi ya kutumikia uongozi wa nchi.

Hawa Juma, mfanyabiashara mwingine ndani ya soko hilo, anasema wanawake wana uwezo wa kuongoza sikoni vizuri, ila shida inayowakabili inaangukia katika dhana ya kutojiamini.

"Hili soko, wanawake hawataki kujitokeza  kugombea nafasi yoyote na kama mwanamke kajitokeza kugombea, hawezi kupigiwa kura za wanawake wenzake," anasema Hawa.

MWENYEKITI UCHAGUZI

Mwenyekiti wa Machinga Kata ya Saranga, Ibrahim Ally, aliyeendesha uchaguzi katika soko hilo, anawataka wafanyabiashara sokoni, wajenge tabia ya kuwahoji maswali ili wawajue, kisha ndio wanagombea fursa kwenye uchaguzi ufanyike.

Ally anawataka wapigakura sokoni kutotekwa na ushabiki, wafanyabiashara wachague mtu kwa ajili ya maendeleo ya soko na kamwe sio kumchagua mtu kwa ushabiki. Anasema: “Msifanye mzaha, chagueni watakaowaletea maendeleo na sio kumchagua kwa ajili ya ushabiki."

Hamisi Juma, mfanyabiashara wa soko hilo na mgombea uongozi, anataka kupata majibu kwa mgombea uenyekiti sokoni, namna atakavyohakikisha anakomesha rushwa ya pesa na udhalilishaji.

Ni swali lililotoka kwa mgombea uenyekiti sokoni, Haji Waziri, anasema majukumu ya kila atakapopata changamoto, atazifanyia kazi.

MWENYEKITI MPYA

Msafiri Gwakisa, aliyepata nafasi ya uenyekiti anaahidi kuleta maendeleo sokoni, kwa ushirikiano na wafanyabiashara kuleta umoja ndani ya soko la jumla ya wafanyabiashara 300 na atahakikisha kusimamia masuala ya usafi na michango ya wanaofiwa, ili waipate kwa wakati.

Anasema kila siku wafanyabiashara wanatoa shilingi 500 kwa ajili ya usafi na atahakikisha usafi utafanywa na kuondokewa kwa wakati sokoni.

Gwakisa anaahidi utaratibu utafuatwa mgeni anapokuwa anaenda kuomba nafasi ya kufanya biashara atahakikisha haki inatendeka, ili kuondoa rushwa.

Ahadi yake ni kupambana na rushwa ya ngono, ili kuhakikisha anavitokomeza sokoni hapo. Anaendelea: "Nimesikia mmoja wa wajumbe anasema ukitaka kizimba cha biashara kwa wanaume utatoa rushwa ya pesa kwa mwanamke utatoa rushwa ya ngono."

Anasema, kutokana na soko hilo kuwa karibu na hifadhi ya barabara, wameshindwa kujenga choo na hivyo wanatumia wafanyabiashara choo cha mtu binafsi.

Pia anazungumzia wanawake kushindwa kugombea  nafasi sokoni, shida kuu iko kwao wenyewe kujirudisha nyuma.

KIONGOZI KIMARA

Angela Mfinanga, Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Saranga, anasema kuwa mfumo dume upo wazi na inaonyesha jinsi wanawake wanavyotengenezwa na kuonyesha wao hawawezi kugombea nafasi yoyote.

Anasema, elimu inabidi itolewe ili kuwawezesha wanawake waweze kujitambua itasikitisha wanawake wanashindwa kuomba nafasi na wamekuwa wanawake hao wanawafanyia kampeni wanaume ili waendelee kushika madaraka.

Habari Kubwa