Kinamama thibitisheni uwezo wenu mnapopewa majukumu

16Mar 2019
Reubeni Lumbagala
Dodoma
Nipashe
Kinamama thibitisheni uwezo wenu mnapopewa majukumu

KALAMU ya mwalimu bado inawapenda kinamama na ina neno la kuwaambia wanawake wa Tanzania. Ikumbukwe kuwa juma lililopita katika safu hii tuliandika makala iliyokuwa na kichwa “Elimu ni mkombozi fikra za wanawake”.

Sasa ni wiki nyingine tangu dunia iadhimishe Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Machi 8.

Kwa mwaka huu 2019, Siku ya Wanawake Duniani ilichagizwa kwa kauli mbiu isemayo “Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu.”

Katika makala iliyopita tulieleza kwa kina kuhusu umuhimu wa wasichana na wanawake kujielimisha ili kupata ukombozi wa fikra ambao ni nguzo muhimu katika kujikomboa wao wenyewe na hatimaye kufanikisha mapambano ya kuleta usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu.

Pia nifafanue kuwa wanawake kujifunza kwa wanawake wenzao ambao wana uwezo mkubwa na waliofanikiwa katika kutimiza majukumu yao kikamilifu ni jambo la msingi.

Wanawake kama wadau muhimu wa maendeleo ya nyanja zote, ni vizuri kutumia kikamilifu fursa wanazozipata ili kubadilisha dhana potofu ambazo jamii imekuwa nazo kwamba hawana uwezo wa kusimamia majukumu mbalimbali ya kijamii na kitaifa.

Njia mojawapo ya kuwakosoa wanaobeza uwezo wa wanawake ni kuhakikisha kuwa katika nafasi walizopo wanatimiza wajibu ipasavyo na kuvuka malengo waliyojiwekea au waliyowekewa na viongozi wake tena kwa kuzingatia muda.

Kuzingatia muda ni jambo la msingi katika kutekeleza majukumu ya aina yoyote. Tena sambamba na hilo, katika maeneo yao ya kazi, wanawake wanapaswa kuchapa kazi kwa juhudi, nidhamu na uwajibikaji wa kutosha ili matokeo chanya yaweze kupatikana.

Kazi ni msingi wa maendeleo. Kama wanawake watajibidiisha jamii itanufaika kwa kupata matunda bora yatokanayo na kazi bora ifanywayo na wanawake katika taifa hili.

Katika majukumu ya kiuongozi, wanawake wahakikishe wanaitendea haki heshima kubwa ambayo viongozi wamewapa kwa kukidhi malengo yanayotarajiwa kufikiwa kupitia utendaji kazi wao wa kila siku.

Kama wanawake wataonyesha utendaji kazi uliotukuka, wataongeza imani kwa jamii na serikali kuhusu uwezo wao, na hii itakuwa chachu ya kuongeza fursa kwa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Kwenye nafasi za kuchaguliwa, wananchi wataweza kuwapigia kura wanawake wengi kwa kuwa watakuwa tayari wamejionea uwezo mkubwa ulioonyeshwa katika kutimiza majukumu yao.

Lakini kama wanawake wataonyesha kupwaya na kuyumba katika nafasi za uongozi, jamii itaendelea na dhana potofu kuwa hawatoshi kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi. Na kama hili likitokeza, litawapa wakati mgumu wale ambao wana uwezo mkubwa wa uongozi linapokuja suala la kuaminika mbele ya jamii.

Katika nafasi za uteuzi, wanawake wahakikishe kuwa wanatumia uwezo, maarifa na juhudi zao zote katika kutimiza wajibu wao kazini.

Rais, mawaziri na maofisa mbalimbali wanapowateua wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi huwa na imani na uwezo wao ndiyo maana huwateua na kuwapa majukumu ya kutekeleza.

Ni jukumu la wanawake kuhakikisha wanazitendea haki nafasi walizopewa kwa kuhakikisha uongozi bora unaonekana katika maeneo yao ya kazi. Kwa kutotimiza majukumu yao ipasavyo, itafunga milango ya wanawake kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Hivyo basi, wanawake wapatapo fursa za kuonyesha karama, vipawa na uwezo wao wa kiuongozi, wahakikishe nafasi hiyo wanaitumia vizuri ili jamii iwe na imani ya kutosha kuhusiana na uwezo wa wanawake kiutendaji.

Katika nyanja ya elimu, wasichana na wanawake hawapaswi kubaki nyuma ili kuionyesha jamii uwezo walionao katika taaluma. Fursa ya kupata elimu ambayo wasichana na wanawake wanapaswa kuitumia vyema ili iwasaidie na jamii katika kupata maendeleo. Wasichana waliopo katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu waongeze juhudi katika kusoma na kujiepusha na vishawishi na tamaa ambazo zinaweza kuhatarisha mustakabali mwema wa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Wasichana waitumie fursa iliyotolewa na serikali ya kutoa elimu msingi bila malipo kuanzia shule za msingi hadi kidato cha nne. Kwa kupata fursa ya kusoma, waonyeshe namna ambavyo wanaweza kuongoza katika ushindani wa kitaaluma na hatimaye kuwabwaga wavulana ambao jamii inadhani wana uwezo mkubwa kuliko wasichana.

Pia, katika masomo ya hisabati na sayansi ambayo yana mchango mkubwa kwenye kujenga nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati, wasichana na wanawake waendelee kuonyesha mafanikio ili jamii inufaike na mchango wa wanasayansi wanawake.

Hii inamaanisha kuwa wakisimama vizuri katika nafasi zao, hakutakuwa na wa kupinga kuhusu uwezo wa wanawake. Wanawake tafakarini na kuchukua hatua.

Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Maoni: (+255) 764 666349.

Habari Kubwa