Kinamama wa Vingunguti 'uswahilini' walivyoingia kwenye uchumi digital

30Jul 2021
Zuwena Shame
Dar es Salaam
Nipashe
Kinamama wa Vingunguti 'uswahilini' walivyoingia kwenye uchumi digital
  • Teknolojia yapaisha ghafla ujasiriamali wao
  • Mwenye mafanikio miaka 5 ageuzwa darasa
  • Mabinti Shujaa; mtaani hadi soko la mbali

DUNIANI hivi sasa kumetawaliwa na harakati za kuwainua kimaendeleo katika nchi nyingi, mataifa mengi yakipigania shughuli za maendeleo kama vile siasa, biashara na kijamii, malezi na kuelemishana mfumo wa kidigitali.

Wana semina ya ujasariamali iliyonadaliwa na asasi ya Ladies Joint, wengi wakiwa wakazi kutoka Kata ya Vingunguti, Dar es Salaam, wakiwa darasani kunolewa biashara ya kiteknolojia hivi karibuni. PICHA: ZUWENA SHAME.

Ni zao la mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika zama zilizopoa kwa kufanya shughuli mbalimbali kwa njia ya digitali, kukiwa na mafanikio kwa hatua kubwa sana.

Aina hiyo ya mapinduzi yamerikodiwa kuwapo kwa kiasi kikubwa hata inawasaidia wanawake katika biashara zao kwa msaada wa mitandao ya kijamii, hasa aina za ‘Facebook’ na ‘Instagram’ zinazorahisisha biashara mitandaoni, hata hatua kubwa inashuhudiwa kwa kinamama watumiaji.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia, Uwezeshaji wa Wanawake (UNWOMEN), liliripoti kuwa wasichana na wanawake wengi duniani wanatumia teknolojia kutatua shida zao sasa katika kuiunganisha jamii, kujikuza kielimu na kiuchumi.

Kinamama katika mfumo wote wanawakilishwa chini katika uwanja wa Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM).
Duniani kupitia uchumi unaotanuka kwa nguvu za kidigitali, pia mgawanyiko wa kijinsia, una athari kubwa kwa haki za wasichana na wanawake.

Ili kuziba pengo hili, kunatajwa hitaji la walau vitu vitatu vinavyohitajika kutokea: kuwezesha upatikanaji usawa wa teknolojia za mtandao kwa wasichana na wanawake;

BINTI SHUJAA

Faidha Peter (35), ni mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam, mama mwenye familia inayomtgemea na mfanyabiashara wa juisi ya ubuyu mtaani kwake, anayoitegemea kulisha familia, pia kuwasomesha.

Mafanikio ya mama huyo katika uchumi wenye mzizi katika biashara zake, yanaanzia mfumo wa mitandao ya kijamii darasa alilolipata kupitia taasisi ya Ladies Joint Forum ya jijini Dar es Salaam.

Mama huyo anasema, kabla ya mafunzo ya kufanya biashara ndogo kidigitali, alipata ugumu kujiendeleza katika kipato chake binafsi, hata afanikiwe kujikimu kimaisha. Anasimulia zaidi;

“Kabla ya kupata mafunzo ya kutumia mitandao ya kijamii kama ‘Facebook’ na ‘Instagram’ kwa kutangaza biashara yangu ya juisi, kwa siku nilipata wateja wengi kutoka maeneo mbalimbali.”

Mama huyo anaendelea kufafanua:“Kwa sasa nimekuwa najulikana kwa wateja wengi wanaotoka maeneo mbalimbali na hapa Vingunguti ninakoishi.”

Anaendeleza ufafanuzi wake kwamba, wateja wa juisi anaowapata sasa ni kutoka maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, yakitajwa kadhaa mbali na anakoishi; Mikocheni na Chanika.

Faidha anasema, kutokana na eneo analoishi kuwa vigumu kwa wanawake na wasichana kufikiwa na elimu ya digitali kwa kuwa na sura ya kushaulika, baadhi ya wadau wa maendeleo wanashindwa kupafikia, hata kupasaidia kielimu na kiuchumi.

“Wanawake tumekuwa na changamoto nyingi, mfano mmojawapo mkubwa ni kuweza kuendana na mabadiliko ya mwenendo wa kidunia, hasa upande wa kupiga hatua kimaendeleo,” anasema.

Kwa mujibu wa Faidha, maeneo wanakoishikilia mara hayafikiwi kirahisi, hivyo mafunzo ya kidigitali ni muhimu kwao na sasa anaona faida nyingi, baada ya kuanza kujikimu kiuchumi anamudu kusomesha watoto wake kutokana na kipato cha juisi anazouza.

Anakiri dunia sasa kwa kiasi kikubwa inatumia mitandao hata kuwezesha mengi kufanyika, akijumuisha ufanyaji biashara kupitia mitandao na amefaidika.

“Si hayo bali tu, hata ufahamu wangu umeongezeka, kwa sababu mwanzo sikuwa na elimu hii ya kufanya biashara mtandaoni. Nilikuwa nafanya tu kuuza juisi hapa mtaani na nilikuwa sipati wateja wengi sana kama sasa hivi,” anasema.

Samia Hussein (25), mkazi wa Vingunguti Mtaa wa Kombo, ni mjasiriamali mdogo anayesimulia yake kwamba aliazia biashara zake mtandaoni, lakini hakuwa na elimu sahihi ya namna sahihi ya kuiendesha, apate wateja wengi.

Anasimulia namna alivyoweka tangazo lake la biashara mtandaoni, lakini aliishia kukosa wateja, hali iliyomfanya aanze kukata tamaa.

Hata hivyo, baada ya kupatiwa semina kutoka asasi ya ‘Ladies Joint Forum’ ameshajifunza vingi, ikijumuisha elimu sahihi kuhusu mitandao ya kijamii yanayompa matumaini mapya.

“Kwa sasa ninajiamini na kupata matumaini mapya katika biashara yangu. Nitabadilika na kuwa mfanyabiashara mwingine kabisa. Naomba semina kama wadau wengine waweze kusadia wanawake na wasichana,” anasema.

MKURUGENZI MUASISI

Mkurugenzi wa shirika la Ladies Joint Forum , Fransisca Mboya, anaeleza kuwa walianza kazi yao mwaka 2019 na lengo kuu ni kuwaaidia kinamama walio katika mazingira magumu kimaisha, kielimu, kuinua usawa wa jinsia na kuzijua haki zao.

Mboya anasistiza kwamba, kinamama wana vipaji vyao, ila huwa wanakwama ashindwa kujiendeleza kutokana na kutokufikiwa kirahisi na kwa sababu ya uhalisia wao kiuchumi, hata wanashindwa kujitegemea.

Anasema mradi wao uliopewa jina la ‘She Goes Digital; kwa mana aya meanamama anaenda kidigitali, una lengo la kuwahamasisha wanawake na wasichana, kufanya kazi zao kidigitali wakitumia fursa za kijamii na kiuchumi katika mawasiliano ya masoko.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, lengo mojawapo ya mradi ni kwamba utajikita kuwaanda kinamama wa umri mbalimbali, kufanya biashara mitandaoni, pia kujua sheria za mitandao kwa kuzitumia kwa usahihi bila kuvunja sheria za mitandao.

Mboya anasema wameshirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), akiwa na ufafanuzi:“Tulitaka pia wanawake na wasichana hawa wawe na taarifa sahihi za sheria na taratibu za mitandao ili kuepukana na changamoto ya kuvunja sheria hizo wanapokuwa katika biashara zao.”

Anatoa mfano wa kuwapo mama wa kuigwa mfanyabiashara mbobezi katika biashara ya mtandao kwa miaka mitano sasa, Angela Maundio, amegeuzwa kivutio kwa wanawake na wasichana wa Kata Vingunguti na maeneo jirani, hata akawa mahali pa wengine kuvuna ujuzi.

Mkurugenzi anaamini kinamama wengi wa umri tofauti wana uwezo wa kumiliki ‘simu janja’ kununua muda wa maongezi, lakini wanaishia kutumia mitandao hiyo kwa matumizi binafsi kama kujipiga picha na kuziweka mitandaoni na sio biashara na faida.

Anasema, walifikia hatua kupachagua Vingunguti na maeneo mengine kama Buguruni, Dar es Salaam, kwa sababu ni kata kubwa na kumezungukwa na viwanda, mito na dampo la maji machafu, mrundikano, pia kuna watu wengi kuliko maeneo mengine katika Wilaya ya Ilala.

Vilevile, msongamano wa nyumba nyingi, zisizo katika mpangilio, inawafanya wanawake wengi na wasichana washindwe kumaliza elimu ya juu kama vyuo vikuu.

“Tulifanya mradi huu kwa kushirikiana kwa karibu pia na serikali za mitaa ambao waliweza kutusaidia kupata idadi wa wasichana ambao wengi wao wameishia darasa la saba au kidato cha nne na wameshindwa kuendelea na masomo ya juu hasa vyuo vikuu” anasema Mboya.

Mama huyo anasistiza kuwa, mradi huu utaweza kuwasaidia wasichana wengi kuondokana na vitendo hatarishi, kama utumiaji dawa ya kulevya na biashara haramu za ngono, kwa sababu wengi wao hawana ajira rasmi.

Anashauri umuhimu wa kuwatenga wasichana mapema zaidi na kuwawezesha kinamama wanaolea watoto, wafahamishwe undani wa malezi bora ya watoto, huku wakiendesha biashara zinazowapandisha kiuchumi.