Kinamama waliohamishia ofisi nyumbani wana simulizi kibao

22May 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Kinamama waliohamishia ofisi nyumbani wana simulizi kibao
  • •Mengi wasiyoyajua, watoto nao ofisi
  • Mtihani mkuu; kutenga mtoto na kazi

MACHI 17 mwaka huu, ndiyo siku serikali ilitangaza kuwapo ugonjwa wa Corona nchini baada ya kuripotiwa kisa cha mgonjwa wa kwanza wa ugonjwa huo.

Maisha halisi ya wazazi katika zama za ‘Likizo ya Corona.’ PICHA: MTANDAO.

Miongoni mwa hatua za kwanza zilizochukuliwa na serikali ni pamoja na kufunga kwa muda shule na vyuo vyote ili wanafunzi warudi na kutulia majumbani.

Baadhi ya ofisi pia zilichukua hatua ya kufunga ofisi zao na kulazimia kufanyia kazi nyumbani. Kuna wafanyakazi waliolazimika kufanyia kazi zao majumbani, wanasema wanalazimika kufanya kazi hizo ndani ya tishio la ugonjwa huo wa corona.

Wazazi wanasema, kama ilivyo kawaida ya watoto wengi wanapokuwa na wazazi karibu, hupendelea zaidi wacheze nao hususani wanaokuwa na umri mdogo.

Ni hali inayowapa wakati mgumu kumudu kufanya shughuli zao za kiofisi wakiwa nyumbani.

MASHUHUDA

Hannah Mwandoloma, ni miongoni mwa wanaofanya shughuli zao nyumbani katika kipindi cha tahadhari ya ugonjwa Corona.
Anasema yeye ni mama wa watoto watatu, wote wanafunzi walioko nyumbani kwa kipindi ambacho shule zimefungwa na inamlazimu agawane muda na watoto wake.

“Ni changamoto kwa kweli, unapokuwa uko bise na kazi zako, lakini wakati huohuo na watoto nao wanataka mcheze na vituko vingine vingi, kwa hiyo ni changamoto kwa kweli,”anasema Hannah.

Pia, anasema kipindi inambidi kufuatilia masomo yao kwa muda mwingi tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Anasimulia: “Yaani kipindi hiki ni ‘Corona vs parenting and home schooling’ (mpaka wa uzazi na shule nyumbani). Mimi nimejifunza kucheki homework (kazi za shule) kila siku.

“Ukweli ni kwamba mambo ni magumu, stress zinazidi ila mzazi ni mlezi, tusizembee tufuatilie watoto kwa karibu ili waendelee kujifunza kila siku.”

Mzazi mwingine anayeitwa Ana Ngisyem, anasema si rahisi sana kufanya kazi na kuangalia watoto watoto kwa wakati mmoja. Anasimulia: “Si rahisi sana kufanya kazi na kuangalia watoto, wakati mwingine mwanangu huwa anataka ‘attention’(umakini) zaidi umsikilize yeye tu.

Mzazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Alfac, anasema kunawakati kazi zake anafanya kupitia ‘video’, hivyo akiwa katikati ya mazungumzo, mtoto huingilia kato mazungumzo yake kikazi.

“Kusema kweli nimejifunza uvumilivu. Yaani katikati ya ‘call’ (simu) mtu ghafla anajipenyeza anadai chapati,” anasema na kuongeza kuwa changamoto hizo za watoto zimemsaidia kujifunza mapishi ya aina tofauti kutokana na mahitaji ya watoto wake.

Pia, anasema amezoea kuwasaidia watoto wake kufanya kazi za shule tofauti na ilivyokuwa hapo awali akifafanua: “Ila kutokana na hali hii nimejifunza na kupika, ‘homework’ nimezoea, maana kila siku lazima niangalie na kwa sasa ‘nime –advance’ (kupiga hatua) maana nawafundisha kabisa,”anasema Alfacj.

Mama huyo anasema kutokana na majukumu mengi, aliyonayo hivi sasa za kazi za ofisi nyumbani, kusimamia watoto wake kusoma pamoja na kuhakikisha wanapata chakula yeye hajijali tena.

“On top of that (zaidi ya hapo), nimezidi kujisahau, ‘time for myself’ (muda wangu) umezidi kwisha kabisa,” anasema Alfacj, anayesema amebuni ratiba binafsi, baada ya kubanwa na mambo mengi, ili kuhakikisha kila kitu kinafanyika.

“Kwa sasa muda ambao nakuwa bize na kazi na wao pia wanakuwa ‘ bize’ na shule, wanasoma vitabu au kufanya homework, hii ni kuanzia saa tatu asubuhi baada ya chai,”anasema Alfacj.

“Baada ya hapo saa saba mchana tunapumzika kwa ajili ya chakula cha mchana, hapo nawapatia ruhusa ya kucheza wakati mimi namalizia kazi zangu za mchana.

“Ila hata wakati wanaendelea na masomo kabla ya kuanza kucheza huwa nalazimika kuwa nawachungulia mara kwa mara kuona wanafanya nini.

“Ila wakati wa kuwasimamia kwenye ‘home work’ mara nyingi huwa inanilazimu niwe nao karibu kwa sababu mtoto wangu mmoja ni mdogo sana na anasoma online,” anasema.

Anasema kila siku huwa inamlazimu kuamka mapema zaidi ili kuwaandalia watoto wake chai kabla ya kuanza kazi zake.

Penina Malundo, ni mama wa mtoto mmoja, anasema wakati mwingine hulazima kuacha kufanya kazi zake na kuanza kumbembeleza.

“Kwa kweli kufanya kazi nyumbani ni tofauti na kufanya kazi ukiwa ofisini. Nyumbani hata ujifungie vipi ili watoto wasikuone, lakini ukisikia sauti analia utalazimika tu kutoka ili usikie kimetokea nini na wakati huo itakuchukua muda hata wa nusu au robo saa kumbembeleza,” anasema Malundo.

Anaongeza: “Na hiyo ni mojawapo ya changamoto ya kukupotezea ‘concentration’ (umakini) ya kazi na inaonyesha ni namna) gani ilivyo ngumu kufanyia kazi nyumbani wakati na watoto wapo.”

Mama huyo anataja mbinu mbadala, kwamba umakini ni mpaka pale mtoto anapolala usingizi. Anaendelea: “Mimi nyumbani nina msaidizi wa kazi ambaye ndiye pia huwa ananisaidia kulea mtoto.

“Lakini, pamoja na hayo akiwa ananiona huwa anataka akae na mimi muda wote na wakati pekee ambao huwa nafanya kazi vizuri ni pale anapolala usingizi, hapo huwa inabidi nifanye haraka haraka kabla hajaamka.

“Na hii wakati mwingine inachangia usifanye kazi kwa kasi ile ambayo tumezoea ukiwa ofisini. Sisemi kwamba kwa sababu ya kufanyia nyumbani unaweza kuharibu kazi.

“Lakini,. ni kweli kwamba kutokana na harakaharaka za kukimbizana umalize kabla ya mtoto hajaamka wakati inachangia usiifanye kwa ufanisi zaidi.”

Anasema, katika kipindi kilichopo, anafanyia kazi zake nyumbani na kupunguza safari zisizo za lazima na amepata muda wa kutosha kufahamu vitu vingi kutoka kwa mtoto wake ambavyo katika kipindi cha nyuma hakuvifahamu.

“Kwa kweli mbali na changamoto ninazoziona za kusumbuliwa na mtoto kwa kufanyia kazi nyumbani, lakini pia kwa sababu sina mizunguko tena, imekuwa kama fursa nzuri pia ya kujifunza mambo mengi kutoka kwa mtoto wangu,” anasema Malundo.

“Nimekuwa kama mwalimu wake kwa baadhi ya vitu vingi, pamoja na kwamba mtoto wangu ni mdogo na hajaanza shule bado, lakini tayari nimeanza kumfundisha baadhi ya vitu na nimegundua kwamba ni mwepesi sana wa kuelewa na ni mtundu.

“Nimefahamu kwamba anaelewa sana kujifunza kupitia katuni, kwa hiyo natumia njia hiyo kumfundisha vitu mbalimbali.”

Habari Kubwa