Kinapa kudhibiti vyanzo vya moto

11Jun 2021
Jenifer Gilla
Nipashe
Kinapa kudhibiti vyanzo vya moto

KINAPA pamoja na wa wadau wa hifadhi hiyo wanashirikiana kuhakikisha vyanzo vyote vya moto vinadhibitiwa.

Ofisa Mhifadhi Mkuu anayesimamia Idara ya Sayansi na Uhifadhi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Imani Kikoti. PICHA: JENIFER GILLA

Mhifadhi Mkuu Kikoti anathibitisha kuwa wanatoa elimu kwa wasaidizi wa watalii kuwa wasiwe chanzo cha kuwaka moto na pia wahakikishe wawalinda watalii.

“Tunawaelimisha kuwa walinzi wa watalii na wao wenyewe, kwamba moto unaowaka na kuthibitishwa kuwa wao au watalii waliokuwa nao ndio wamesababisha moto huo basi watawajibishwa ipasavyo, pia tunawakagua watalii kabla ya kuanza safari kuhakikisha kuwa hawapandi na vifaa vyovyote vinavysababisha moto” anasema Kikoti.

Kauli inayothibitiswa na Munguatosha Mosha (32), msindikiza watalii kupitia geti la Marangu, akikiri kuwa kwa sasa majanga ya moto yamepungua kwa kazi kubwa wanayoifanya .

“Kwa sasa tunalindana wenyewe kwa wenyewe wasaidizi, ukimuona msaidizi wa mtalii yoyote anavuta sigara kiholela au kupika sehemu ambayo si husika tunamripoti, lakini hata watalii nao tunawaelimisha kuwa hawaruhusiwi kuvuta sigara eneo njiani mpaka tufike kwenye kituo cha kupumzikia”, anasema Mosha.

Kupanda miti 

KINAPA kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira wanapanda miti katika maeneo yanayouzunguka Mlima huo ili kukabiliana na joto linalosababiusha theluji kupungua.

Kwa upande wao  Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inahamasisha upandaji wa miti kuanzia ngazi ya familia hadi kitaifa  ili kuwa na uoto wa asili wa kutosha ili kusaidia kupatikana kwa hewa ya oksijeni ya kutosha ili kupunguza joto.

“Kupanda miti kwenye hifadhi pekee hakusaidii kupunguza joto, hivyo tunahitaji kuwa na miti ya kutosha katika mikoa mitatu hii inayozunguka mlima huu ikiwamo, Kilimanjaro, Arusha, Manyara.

“Mwezi huu wa Aprili tunafanya kampeni ya kupanda miti na tunaanzia hapa Arusha Aprili, 1, chini ya ofisi ya mkuu wa mkoa.Lengo ni kupanda miti ya kutosha ili kupunguza joto” anasema Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Lewis Nzali.

TIGO NA KAMPENI YA KUPANDA MITI

Nao kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, kwa miaka 6 mfululizo imekuwa ikifanya kampeni ya upandaji miti mkoani humo kupitia kampeni ya TIGO GREEN FOR KILI katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro miti hupandwa  pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro lengo likiwa ni kurudisha theluji ya mlima huo.

Machi mwaka huu, Kwa kushirikiana na taasisi ya VOEWPOFO, Tigo ilipanda miti 10,000 katika wilaya ya Hai, huku Lengo likiwa ni kupanda miti 28000 kabla ya mwisho wa Mwaka.

“Tunatambua umuhimu wa Mkoa wa Kilimanjaro katika katika uchangiaji wa  ustawi wa uchumi kwa wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla, ndio maana tumejikita kuilinda theluji ya Mlima

Kilimanjaro ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii nchini Tanzania, barani Afrika na ulimwenguni kote”, Alisema Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo katika uzinduzi wa kampeni hiyo.

NEMC YAJIONGEZA KIKANDA

Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Lewis Nzali, anasema wamekuwa wakisimamia mazingira ya kanda hiyo ya Kaskazini ili kuhakikisha kunakuwa na uoto wa asili wa kutosha kukabiliana na joto.

Mojawapo ikiwa ni kuhakikisha viwanda vikubwa vinakuwa na mfumo mzuri wa kutoa hewa ya carbon na kuhakikisha kila kiwanda kinapanda miti ya kutosha kukizunguka. 

Vilevile imekuwa ikitoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuilinda hifadhi hiyo pindi wanapokutana kwenye vikao.

 “Mfano tulishauri wapanda mlima wafanyiwe upekuzi kuhakikisha hawapandi na kifaa kinachosababisha moto, na tumeona yamefanyiwa kazi na kwa kiasi kikubwa majanga ya moto nyamepungua katika hifadhi hiyo” anasema

Vilevile kutokana na mamlaka walionayo NEMC imekuwa ikikagua miradi yote inayoelekezwa katika hifadhi hiyo ili kujiridhisha kama ni rafiki kwa mazingira.

Meneja huyo anatolea mfano wa mradi wa magari ya umeme (cable cars) ambao mpaka sasa haujathibitishwa kwa kuwa bado unafanyiwa thathmini kuona kama ni rafiki kwa mazingira ya hifadhi hiyo.

“Tunatumia wataalam, tunataka tujiridhishe kama kweli zile nyaya za umeme zinazotaka kupitishwa juu kama njia ya magari hayo hazitokuwa na madhara makubwa kwa hifadhi, je, ni miti mingapi itahitajika kukatwa ili njia ipatikane, tusiporidhika hautofanyika “anasema 

Mahakama yamaliza mchezo 

Watu wanaokamatwa katika msitu huo hupelekwa kwenye vyombo vya sheria kwa kuzingatia Sheria ya Uhifadhi Misitu ya Mwaka 20O2 na nyinginezo zinazohusiana.

Rose Lyimo ni Mwanasheria wa kujitegemea kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi anayethibitisha kupokea wahalifu watatu hadi 5 kwa mwezi wanaotokana na makosa ya uvamizi wa hifadhi.

“Kwa sasa kesi za uvamizi wa hifadhi umepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma, kutokana na hukumu zilizokuwa kinatolea watu wamekuwa wanafuata sheria kwa mwezi.

 “Hapa tunapokea washtakiwa wasiozidi 5 kwa makosa madogo madogo, sio yale ya kukata miti kwa biashara, yale yamekomeshwa kabisa na huwa tunawaadhibu kulingana na Sheria ya hifadhi ya Misitu,” anasema Rose  

SHERIA YA MISITU INASEMAJE

Sheria  ya Uhifadhi wa Misitu ya mwaka 2002, kufungu namba 26-(a,b, s), inasema kuwa mtu yoyote haruhusiwi, kukata, kuangusha, kuchimba au kuondoa mti wowote katika eneo la hifadhi. Kuchimba au kuondoa mmea wowote wa msitu uliohifadhiwa, kuvuna, kuchukua au kuondoa mazao mengine yoyote ya msitu.

Kufanya shughuli zingine zozote ndani ya msitu wa kitaifa au wa serikali za mitaa, hifadhi ambayo ni marufuku na kanuni zinazotumika kwa msitu wote wa kitaifa, akiba au sheria zozote zinazotumika kwenye hifadhi maalum ya msitu wa kitaifa au sheria ndogo zinazotumika kwa hifadhi maalum ya msitu ya mamlaka ya mtaa.

Wakati kifungu namba 84-5 kinasema kuwa “(5) Mtu yeyote anayetenda kosa chini ya kifungu hiki atakuwa na hatia ya kosa na baada ya kutiwa hatiani atatozwa faini isiyopungua Sh.30,000 na isiyozidi Sh. milioni moja au kifungo cha muda isiyozidi miaka miwili au kwa faini zote mbili na kifungo.

Mafanikio 

Kudhibiti majanga ya moto katika hifadhi hiyo ni moja ya changamoto inayoelezwa na Mhifadhi Mkuu Kikoti, kwamba ulkikinganisha na miaka ya nyuma ambapo kila mwaka hifadhi hiyo ilikuwa ikiungua moto sasa hali ni tofauti.

“Kwa sasa yunaweza kukaa hata miaka 3 bila kupata kesi ya moto na hii ni kutokana na udhibiti mkubwa wa kupanda mlima na vifaa vya moto tulioufanya”, anasema.

Mkuu huyo wa idara ya ikolojia pia anajivunia kutokomeza kabisa ujangili wa miti ya mbao kwa hifadhi hiyo, akijigamba kuwa kwa muda mrefu hajapata keshi ya uvamizi huo mkubwa.

“Lengo la kuzuia shughuli za kibinadamu ili kuiacha misitu istawi yenyewe tumefanikiwa kwa asilimia takribani 90. Zamani ilikuwa ukishuka hapo kuwa unahitaji kitanda cha mbao ya mti unaopatikana hapa hifadhini unapata siku moja tu lakini sasa wanakwambia kabisa hatuna hizo mbao” anasema.

Pia elimu inayotolewa inaonekana kueleweka kwa wanakijiji hao kutokana na ushirikiano wanaoutoa kwa mamlaka ya hifadhi hiyo pale wanapoona kuna ujangili, inaelezwa na Mhifadhi huyo.

Changamoto 

Kila lilo jema halikosi changamoto, hali kadhalika katika harakati za kupambana na ujangili wa kukata miti katika hifadhi hiyo wanakutana na changamoto kadha wa kadha ikiwamo kuzidiwa na idadi ya watu. 

“Unajua  hifadhi hii imezungukwa na vijiji 92 kwa hivyo ‘kucontrol’ wakazi wote wasivamie hifadhi ni kazi kubwa, hivyo inabidi askari wafanye kazi usiku na mchana” anasema Mkuu wa Idara ya Ulinzi na uokoaji wa KINAPA, Mapinduzi Ndesa.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada WA Intenews, Earth Journalism Network. 

Habari Kubwa