Kinyesi cha kuku lulu mpya katika ufugaji

10Oct 2021
Sanula Athanas
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Kinyesi cha kuku lulu mpya katika ufugaji
  • Lulu mpya katika ufugaji wa samaki na kilimo cha mboga *Mnufaika: Nina gari na nyumba za kisasa kwa wake zangu wote...

UNAPOKANYAGA Mtaa wa Kiebikiri ulioko Kata ya Turwa wilayani Tarime mkoani Mara, katika orodha ya wajasiriamali wake, hakosekani Christopher Mwita mwenye umri wa miaka 48.

Mahali hapo ni umbali wa Km 4.3 kusini mashariki mwa Mji wa Tarime na safari yake kutoka mjini ni mwelekeo wa kufuata barabara ya lami ya Nyamwaga, kisha unachepuka kushoto ukipita kwenye barabara ya vumbi umbali wa mita 400 kulifikia shamba lake kutoka Shule ya Sekondari Mwera Vision inapoanzia barabara hiyo ya vumbi.

Kwa mbali anaonekana Mwita akiwa katika harakati za kuhudumia mifugo yake kwenye eneo ambalo maji yake ni ya chemchemi. Uso wake umejawa tabasamu lenye mzizi wa mafanikio aliyoanza kuyashuhudia miaka 14 iliyopita katika shughuli zake za ufugaji mseto unaojumuisha kuku, samaki na bustani ya migomba na mboga (mchicha, sukumawiki, chinese na kunde).

Kinachoshuhudiwa katika mradi wake huo ni ujasiriamali usiozoeleka kwa wengi, kuku, samaki na bustani vinaendeshwa kwa wakati mmoja, eneo moja, vinategemeana na kila kimoja kikiwa na mazao maradufu ya kawaida.

Leo hii maisha ya Mwita, ambaye awali alikuwa akiendesha uzalishaji wa bidhaa hizo kienyeji, baadaye akapata darasa na kuthubutu kujitosa kwenye teknolojia hiyo mpya, yamekuwa yenye kicheko cha kudumu.

Uzalishaji wa samaki na kuku sasa umemwongezea theluthi mbili ya ilivyokuwa awali. Jicho zaidi likizama kwenye uchumi huo penye ubia wa samaki na bustani, penyewe pametikisa zaidi pakiwa na ongezeko linalokita asilimia 300.

Maisha yake kwa ujumla si haba. Pato lake kwa mwaka lina wastani wa mara mbili ya alivyokuwa zamani, huku akijidai kwa miliki ya nyumba mbili mpya, kila mama mtoto na yake, mwenyewe akizunguka hapa na pale akiwa ameshikilia usukani na kupiga honi mitaani, jambo ambalo awali lilikuwa tamthilia isiyo na ushuhuda halisi kwake.

 

YAMEWEZEKANAJE HAYO?

Mjasiriamali Mwita anasimulia kwamba ni matokeo ya kile alichokianza mwaka 2004, lakini sura kubwa ya mafanikio ilijitokeza mwaka 2007 baada ya kupata darasa lililojitosheleza na kuibua majibu chanya yaliyoangukia hata kubadili haiba ya maisha yake ya kawaida.

Hiyo ilianza pale Mwita alipokuwa mnufaika wa mafunzo maalum ya ubunifu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), hata yakamwezesha kupanua ufugaji wake kwa haraka pale mwaka 2004 yalipomwondoa kutoka kwenye ufugaji wa kienyeji, akiwa na bwawa la samaki lenye ukubwa wa mita za mraba 30 (mita tano kwa sita) na ndani ya mwaka mmoja akapanua kufikia mita za mraba 120 (mita 10 kwa 12), ambazo ni mara nne ya awali.

Mwita mwenye wake wawili na watoto sita (watatu wa kike), anasema alizidi kusonga mbele, akiainisha kutoka mwaka 2005 alipojitanua zaidi hadi kufikia bwawa lenye ukubwa wa mita za mraba 380 (mita 19 kwa 20). Hatua hiyo ya upanuzi wa mradi wa mabwawa, aliifanya kwa mtindo tofauti kidogo wa kuongeza mabwawa mengine mawili mapya, kila moja likiwa ni kubwa zaidi kuliko ya awali.

Anafafanua hali ya mabwawa hayo kwamba moja lina ukubwa wa mita za mraba 400 (mita 20 kwa 20) na lingine lenye ukubwa wa mita za mraba 450 (mira 15 kwa 30), ambayo kwa ujumla wake yameunda tafsiri mpya ya mafanikio yake kwenye ujasiriamali huo, yakiwa na muundo na mfumo wa uzalishaji mpya.

 

UNAVYOENDESHWA

Kuhusu namna ya uzalishaji anaouendesha, Mwita anasema: "Kinachofanyika hapa unakuwa na bwawa la samaki, juu yake unajenga banda la kuku na pembeni ya bwawa unakuwa na bustani. Kinyesi cha kuku kikidondoka kwenye maji, kinakuwa chakula adhimu kwa ajili ya ukuaji wa samaki. Maji nayo yanapata rutuba inayomwagiliwa kwenye bustani.

"Muhimu hapo, hakikisha banda lako la kuku halisogei sana kwenye maji, walau mita moja na nusu au mbili kutoka kwenye maji maana usiku kunakuwa na baridi sana kwenye bwawa. Kuku wakipigwa na baridi kali, wanakonda. Wakikumbwa na hali hiyo, hutapata mayai. Pia ni muhimu kuweka uzio kuzungushia bwawa kwa ajili ya usalama wa samaki na kuku.

"Wakati ninaanza ufugaji mseto mwaka 2004, baadhi ya majirani waliniona kama nimepatwa na kichaa, lakini baada ya mafanikio wamekuwa miongoni mwa watu wengi wanaofika hapa kuja kujifunza na hata kununua kuku, samaki, mboga na ndizi.

"Nimekuwa nikipata wageni wanaokuja kujifunza kutoka mikoa ya Tabora, Arusha, Shinyanga, Dar es Salaam, Pwani, Mbeya na hata wanaotoka Uganda, na nimeitwa maeneo mengi kwenda kutoa elimu hii.

"Kwa kifupi, huu ni ufugaji wa gharama nafuu sana. Ninalisha kuku, kuku wanalisha samaki! Maji haya yenye rutuba yanatumika kumwagilia bustani, mazao ya bustani nayo yanakuwa chakula kwa hao wawili (kuku na samaki) na vyote hivyo unaweza kuvuna na kuuza. Shughuli inajiendesha yenyewe bila ya gharama kubwa.

"Wateja wangu ni wa hapa hapa Tarime, huwa ninauza bidhaa hapa hapa shambani kwangu. Wanunuzi wa jumla wa samaki na kuku huwa wanakuja ninawauzia, wao wanakwenda kuuza huko wanakojua."

Ndani ya falsafa ya kila mafanikio kuna magumu yake, hilo pia linajitokeza kwenye uzalishaji huo ambao Mwita anautolea ufafanuzi:

"Kikwazo katika mradi huu kwa sasa ni kwenye upatikanaji wa mbegu. Vifaranga vya samaki vinapatikana Arusha, Kenya na Uganda. Pia kunapokuwa na ukame, wale 'ndege mwarabu' wanakuja kwa ajili ya kusaka chakula, wanatua kwenye bwawa na kuchukua samaki.

"Kunapokuwapo kenge pia ni tatizo. Kuna shida ya vyura na nyoka, kunapokuwa na vyura ndani ya bwawa, lazima nyoka utawakuta, vinginevyo uweke samaki aina ya kambale, lakini sisi tunafuga zaidi samaki jamii ya sato.

"Usumbufu wa nyoka uko kwenye bwawa, wanaingia kwa ajili ya kula vyura. Ukipanda mchaichai kuzunguka bwawa, nyoka haingii. Pia tunatumia mbinu ya kuweka bata wadogo kwenye bwawa, kamwe nyoka haingii kwenye bwawa lenye bata hao."

Mjasiriamali Mwita bado anajifariji kwa madhila ya magumu hayo ndani ya ufugaji, akigeuzia shingo kwenye ulingo wa majumuisho ya mafanikio yake anayoyawasilisha kwa lugha ya tabasamu kwamba:

"Nilianza mradi huu nikiwa na mtaji wa Sh. 15,000 tu. Sasa nina uhakika wa kusomesha watoto wangu wote sita (mmoja chuo kikuu na wengine wanasoma sekondari binafsi) na nimejenga nyumba za kisasa kwenye miji yangu miwili (wake wawili)."

Mwita ambaye kielimu aliishia elimu ya msingi, anabainisha kuwa wakati anaanza ufugaji wa samaki kwa njia ya kawaida mwaka 2004, alikuwa anapata faida ya Sh. milioni 2.5 kwa mwaka, lakini sasa kwenye ufugaji mseto anavuna faida ya Sh. milioni sita kwa mwaka, sawa na ongezeko la zaidi ya mara mbili.

 

THAMANI YA KINYESI

Katika hali ya kawaida, sifa ya kinyesi cha wadudu na mifugo huangukia katika kurutubisha udongo. Lakini wanazuoni wataaluma husika wanasonga zaidi ya hapo, wakiangaza lishe kwa samaki, kurutubisha maji na yanayofanana nayo.

"Ndege wanakula vitu vingi vyenye rutuba lakini kiasili miili yao haina uwezo wa kufyonza virutubisho vyote, hivyo vinapodondoka kwenye bwawa vinakuwa na manufaa makubwa kwa ukuaji wa samaki," anafafanua Dk. Amon Shoko, Mtafiti kutoka TAFIRI.

Mbobezi mwenzake, Musa Ngematwa, aliyezama katika stadi ya ufugaji samaki, anaenda mahususi kwenye kinyesi cha kuku, akibainisha kuwa mbali na kuwa chanzo cha mbolea kilichozoeleka, pia kinaangukia kwenye urutubishaji wa bwawa la samaki, hasa panapofanyika ufugaji mseto baina ya pande hizo mbili zikitegemeana.

Ngematwa anasema ili kupata chakula cha asili kwa samaki ndani ya ufugaji huo mseto, kinyesi cha kuku hufanywa chanzo cha mbolea kwa sababu huwa kina kiasi kikubwa cha virutubisho vya urea, ambavyo vinahitajiwa kwa samaki kama lishe na mchango muhimu kwa afya yao.

Namna kinavyotumika, mtaalamu huyo wa mifugo anabainisha kwamba ni ama kinaliwa moja kwa moja na samaki pindi kinapodondoshwa bwawani au huwa chanzo cha rutuba kwenye bwawa lao.

"Hiki huwapa samaki afya nzuri kwani huwa na chembechembe nyingi za urea ambazo ni sehemu kubwa ya madini ya Naitrojeni na Fosforasi, ambayo huhitajika kwa wingi kwenye chakula cha samaki," anafafanua.

Lingine analolitaja mtaalamu huyo, ni kwamba mfugaji anapotumia utajiri wa kazi yake kama lishe, moja kwa moja anavuna manufaa mengi kiafya kutokana na viini lishe vya protini vinavyopatikana kwa mlo wa kuku, mayai, samaki na mboga, vyote vinapatikana kutoka mzunguko wa ufugaji huo tajwa.

Pia anadokeza katika eneo la uchumi kilimo kwamba ni aina ya ufugaji inayobeba chanzo cha pesa kama ilivyoshuhudiwa kwa mfugaji Mwita, na kuna pato la kutosha kukidhi mahitaji mengine ya maendeleo binafsi kutoka kwenye kila kilichofanyika ndani ya ufugaji huo.

Mtaalamu Ngematwa anahitimisha uchambuzi wake wenye wajihi wa afya na uchumi katika eneo hilo la ufugaji na kilimo, akipigia debe ufugaji huo wa kuku na mseto wake uliotajwa, kwamba unafanyika kirahisi na wa gharama nafuu kulinganisha na wanyama wakubwa kama ng’ombe, nguruwe, mbuzi na kondoo ambao wana kawaida ya kuhitaji mitaji mikubwa na wasimamizi wengi.

MBOLEA IZIDI

Kuhusu upimaji wa kiwango cha mbolea kinachohitajika kwenye bwawa kwa ajili ya ustawi wa samaki, Dk. Shoko ana ufafanuzi wa kitaalamu, akisema:

"Unaingiza mkono wako kwenye bwawa, hakikisha mkono unazama hadi usawa wa kiwiko, kisha ukunje kidogo, kama usipofanikiwa kukiona kiganja chako, ujue mbolea hiyo imezidi na ina hatari ya kuwaua samaki.

"Cha kufanya baada ya kubaini hali hiyo, ondoa hayo maji kwa kuyamwagia kwenye shamba lako, usifungulie bwawa maana maji hayo yana thamani kubwa, yana rutuba. Ukishayaondoa, weka maji mengine kwenye bwawa. Kama kiganja chako kitaonekana kirahisi, hapo ujue mbolea haitoshi kwenye bwawa."

KUTOKA TAFIRI

TAFIRI kupitia matokeo ya utafiti wake uliofanyika kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka huu, inabainisha teknolojia ya ufugaji mseto wa samaki, kuku na bustani una nafasi kubwa ya kubadili maisha ya kijamii na uchumi wa mzalishaji, ikimpandisha hadhi kuelekea kwenye maisha bora akiwa kwenye mfumo mpya wa uzalishaji wenye tija maradufu.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo uliofanywa na TAFIRI kwa udhamini wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), mfumo huo wa ufugaji mseto unamwongezea mfugaji ziada ya theluthi mbili ya alichokuwa anapata kupitia ufugaji wa kawaida; wastani wa asilimia 66 kwenye ubia wa samaki na kuku, huku bustani ya mboga ikipata ziada ya asilimia 67.

TAFIRI ambao walianza na wafugaji sita, akiwamo Mwita, sasa wanatamba na mafanikio ya darasa lao hilo, wakimtaja mfugaji huyo kuwa mfano wa kuigwa na 'kioo' kinachoakisi maendeleo ya Kanda ya Ziwa.

"Tunajivunia sana mafanikio ya Mwita, tulipomtembelea mwaka 2004, yaani ni kama alikuwa na shimo la samaki, halikuwa bwawa la samaki lile (mita tano kwa sita). Sasa anafanya vizuri Kanda ya Ziwa na kitaifa kwa ujumla.

"Kwenye maonesho ya wakulima anawavutia wengi, tumekwenda naye Kenya mara mbili, tumekwenda naye Uganda mara tatu. Kote huko wafadhili wetu amewafurahisha sana kutokana na mafanikio yake.

"Sasa kila wanapotuita kwa ajili ya mawasilisho ya mrejesho wa kazi zetu, wanasisitiza 'mje na yule mfugaji wa Tarime'. Kwa kweli ametokea kuwavutia sana kutokana na juhudi zake," Dk. Shoko anasifu.

Hali kadhalika, katika kutanua uzalishaji huo, mtaalamu huyo anasema TAFIRI wanasambaza ubunifu kwa vikundi vidogo kwenye maeneo mengine nchini, tayari wakiwa wameifikia mikoa ya Mara, Songwe, Iringa na Morogoro.

Mwanazuoni huyo wa TAFIRI, anapendekeza: "Kwa manufaa ya baadaye, elimu ya ufugaji mseto wa kuku, samaki na bustani ifikishwe kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo wengi zaidi nchini."

 

WAVUVI WADOGO KITAIFA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, anabainisha uvuvi wa samaki baridi unachangia asilimia 95 ya samaki wote wanaovuliwa nchini.

Vilevile, kwenye orodha ya wakuzaji samaki inayomhusu Mwita, Waziri Ndaki anataja jumla yao wako 30,064, ilhali wenzao wanaoendesha uvuvi wa moja kwa moja katika maeneo kama baharini na ziwani jumla yao wako 195,435. Kwa lugha rahisi, kundi la kina Mwita aliyeko Tarime, ni asilimia 13 ya wavuvi wote kitaifa.

Waziri anafafanua sifa ya bidhaa samaki kwamba wanachangia kupatikana asilimia 30 ya lishe ya protini yote kutoka kwa wanyama nchini; huku kiuchumi anasema sekta ya uvuvi mwaka jana (2020) ilichangia asilimia 1.71 kwenye Pato la Taifa, kiwango kinachofanana na mwaka uliotangulia (2019).

Kwa mujibu wa waziri huyo, kasi ya kukua kwa sekta ya uvuvi mwaka jana ilikuwa ya kiwango cha juu cha asilimia 6.7 kulinganisha na iliyoshuhudiwa katika mwaka uliotangulia (2019) ya wastani wa asilimia 1.5, sawa na ongezeko la asilimia 5.2 ndani ya mwaka mmoja.

Inaporejewa Dira ya Taifa ya Maendeleo (mwaka 1999-2025), mkakati uliopo wa kiserikali wa miaka mitano inayoishia 2025, ufugaji ni eneo mojawapo linalofanyiwa kazi kwa dira ya kuzalisha ajira milioni nane mahususi kwa vijana, huku ukilihakikishia taifa kujitegemea kwa vyanzo vya chakula muhimu.

Habari Kubwa