Kisimiri; shule bora ya kata inayopambana kuvunja rekodi yake

09Aug 2016
John Ngunge
Arusha
Nipashe
Kisimiri; shule bora ya kata inayopambana kuvunja rekodi yake

KUIBUKA kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza kati ya shule 10 bora nchini katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, kumeinyenyua shule ya kata ya Sekondari ya Kisimiri mkoani Arusha, katika namna ya kushtua, kushangaza na kuwavuta wengi nchini.

shule ya Sekondari ya Kisimiri mkoani Arusha.

Wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wanahabari, ni miongoni mwa watu wengi wanaovutika kutembelea shule hiyo tangu matokeo ya mitihani hiyo yalipotangazwa na serikali hivi karibuni.

Hii ni kutokana na mazoea yaliyojengeka kuona au kusikia nafasi ya kwanza inashikwa na shule binafsi au zile za taasisi za dini.

Matokeo ya shule hii, iliyoanza mwaka 2002 yamefungua ukurasa mpya na kuzibeba shule za kata (serikali) ambazo kwa muda mrefu zimekuwa hazionyeshi kufanya vizuri.

Pamoja na wengi kustaajabu, lakini walimu 68 wanaofundisha shule hiyo wanasema ni kawaida kwao kufanya vizuri.
Katika matokeo ya mtihani yaliyotangazwa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa, Dk. Charles Msonde, licha ya shule hiyo kuongoza, bado hayajakata kiu ya Mkuu wa Shule Mwalimu Emanuel Kisongo na walimu wenzake kufanya vizuri zaidi.

Matokeo hayo yanaonyesha wanafunzi 50 wa shule hiyo wamepata daraja la kwanza na 13 daraja la pili.

“…Kuwa ya kwanza (Kisimiri) kwetu sisi siyo jambo geni. Tumekuwa katika kundi la 10 bora kwa miaka sita sasa,” anasema Mwalimu wa Taaluma, Valentine Tarimo.

Hakuna uchawi katika suala la taaluma anaweka bayana kuwa taaluma ni mipango, mkakati na kutekeleza mipango hiyo.

Anabainisha matokeo mazuri ya kitaaluma ya muda mrefu ndiyo yaliyoipaisha shule hiyo hadi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuipandisha hadhi na kuwa miongoni mwa shule maalum.

Uamuzi huo ulichukuliwa mwaka 2011.

“Maendeleo yetu kitaaluma ni mazuri.

Mwaka 2013 tulishika nafasi ya tano kitaifa, mwaka 2014 nafasi ya tatu, na mwaka 2015 tulishika nafasi ya nane kitaifa wakati mwaka huu (2016) tumeshika nafasi ya kwanza kitaifa.” Alifafanua na kuendelea.

“Matokeo ya mwaka huu yamedhihirisha hatuhitaji fedha kufanya vizuri bali akili. Shule yetu ni ya kata kwa maana halisi lakini tumeweza kufanya maajabu kitaifa,” anatamba.

Pamoja na kuyakubali matokeo hayo, Tarimo anasema wameanzisha mradi wa ‘Kisimiri Sawazisha,’ baada ya kubaini changamoto katika kufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne.

“Tulijipa miaka mitatu kuanzia 2014 kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza ili matokeo yao yawe sawa na ya wanafunzi wa kidato cha sita.

“Kabla ya hapo kulikuwa na daraja sifuri kwa wanafunzi 145 hii ilikuwa hatari sana. Kitaifa ilishika nafasi ya 1,554 lakini baada ya kuanzisha mradi huu tulihama kutoka daraja sifuri la wanafunzi 145 hadi 13 na tulipanda na kushika nafasi ya 422 mwaka 2014,” anaeleza.

Matokeo hayo yaliwawezesha kupeleka wanafunzi 35 kidato cha tano waliochaguliwa kwa shule za serikali tu licha ya wengine walioenda vyuo mbalimbali na shule binafsi.

“Kwa mara ya kwanza matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2015 wanafunzi tisa walipata daraja la kwanza na tuliweza kupunguza daraja sifuri 13 hadi 12.

“Mwaka huu ni kivumbi, hatutakuwa na daraja sifuri katika matokeo ya mwakani kwa kidato cha nne na sita pia. Mtakuja hapa kutuhoji (waandishi wa habari) mara mbili kwa mwaka, yaani baada ya matokeo ya kidato cha nne kutoka na safari ya pili ni baada ya matokeo ya kidato cha sita,” anatamba.

Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Kisongo, anakoleza pale anaposema, “sisi hatushindani na shule bali tunashindana kuvunja rekodi yetu wenyewe.”

Anasema shule yake itaendelea kufanya vizuri miaka yote hata yeye asipokuwepo hapo.

Akitaja siri za kuongoza, Kisongo anasema inatokana na uongozi, ujuzi, kujituma na uwezo walionao walimu hali ambayo imezaa timu nzuri ya walimu.

“Nina walimu wazuri na hii imetokana na kuwapa moyo na kuwahimiza kujiendeleza. Baada ya miaka mitatu shule yetu itakuwa na walimu 20 hivi wenye shahada ya uzamili kutoka vyuo vikuu mbalimbali,” anasema.

Sababu nyingine ya mafanikio ni mfumo alioutengeneza unaomwezesha kusimamia uendeshaji wa shule kitaaluma hata kama anakuwa safarini.

“Kwa kutumia mfumo huo ninaweza kujua shughuli za kitaaluma zinazofanyika kwa juma husika na mimi kutoa majawabu ya ziada pale inapohitajika. Hakuna mwalimu anayeweza kudanganya au hata kupika matokeo ya wanafunzi.

“Unajua kuna tofauti kati ya mwalimu mkuu na mkuu wa shule. Mwalimu mkuu hufanya kazi zote. Kwa mfano, manunuzi, kutunza stoo na kadhalika, wakati mkuu wa shule ni taasisi yenye mgawanyo na kushirikisha walimu wengine katika uendeshaji wa shule.

“Shuleni kwetu hakuna wajibu mdogo, kwa mfano, kiranja wa darasa, mwalimu wa zamu hadi mkuu wa shule kila mmoja anao wajibu wake wa kufanya,” anasema.

Anasema kutokana na mfumo alioujenga, shule yake haishindani na shule zingine isipokuwa mashindano yao ni kuvunja rekodi yao wenyewe.

Anasema kwa mfano, hakuna mtu aliyevunja rekodi ya Filbert Bayi au Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.

Siri nyingine ya mafanikio anasema ni mahusiano mazuri na wananchi na wakuu wake wa kazi.

Lugha za kejeli na matusi zilizokuwa zikitolewa na watu wa kada mbalimbali kwa shule za kata, licha ya kumsikitisha zilimpa moyo zaidi.

“Matusi tuliyokuwa tukipata siyo ya kawaida. Wapo waliokuwa wanatuita ‘yebo yebo’, wengine wakituita walimu wa ‘vodafasta’ na kadhalika.

“Lakini matusi haya yalikuwa fursa ya kufanya vizuri zaidi na ndiyo maana katika kipindi cha miaka 10 tumefanya mapinduzi makubwa kwa elimu.

“Sasa hivi kwa ada ya Sh. 70,000 tu tumeweza kuzipiku shule ambazo zinatoza ada hadi shilingi milioni 10 kwa mwaka…hii inaonyesha fedha siyo msingi pekee wa elimu,” anasema na kuongeza siri nyingine ya mafanikio ya shule hiyo ambayo ni uthubutu wa walimu na wanafunzi.

“Wanafunzi wanalipa shilingi 70,000 lakini akili yetu ni shilingi milioni 10,” anasema.

Anasema ni dhambi kwa mtoto kukaa miaka minne shuleni kisha anaambulia daraja sifuri.

“Matarajio yetu yalikuwa wanafunzi wote wangepata daraja la kwanza.

“Yupo mwanafunzi mmoja amepata alama (points) sita lakini sijafurahi sana kwa sababu alitakiwa kupata alama tatu,” anasema.

Hata hivyo, anasema: “Namshukuru Mungu kwa matokeo hayo kwa sababu lengo langu limetimia, wale watoto wengi wao wanatoka familia za wazazi ambao hawana uwezo hata wa kuongea na Ofisa Tarafa.

“Shule ile ipo kijijini, tena kijijini hasa. Kijiografia ipo Kata ya Uwiro yenye vijiji viwili vya Kisimiri Chini (iliko sekondari ya Kisimiri) na Kisimiri Juu, wilayani Arumeru.

“Mazingira yake ni magumu yanahitaji roho na siyo moyo,” anasema na kuongeza, “kwa namna fulani ilikuwa ikitumiwa kama shule ya adhabu kwa walimu kutokana na mazingira yake.”

Kijiji jirani na shule hiyo Kisimiri Juu ni eneo ambalo wakazi wake wengi hujishughulisha na kilimo haramu cha bangi inayostawi vizuri, lakini Mkuu wa Shule Kisongo anasema bangi haijapata kuwa kikwazo kwa wanafunzi wake, kwani anawalea katika mazingira yanayowafanya wajitambue kwamba, bangi ni haramu na madhara yake ni makubwa.

Mzazi kutoka Vvwawa Mkoa wa Songwe, Harry Jonas Sinjela, ni mmoja wa wazazi aliyemsindikiza binti yake kujiunga na kidato cha tano shuleni hapo, anasema alifurahi sana kusikia mwanawe amechaguliwa kujiunga na shule hiyo.

Anasema alipata taarifa kwamba shule hiyo imeongoza kitaifa wakati akiwa njiani kumleta mwanawe.
Aliwapongeza walimu kwa kazi nzuri walioifanya na akawaomba wasife moyo.

Hata hivyo, aliiomba serikali kutengeneza barabara hadi shuleni kwa kuwa iliyopo ni mbovu.

Habari Kubwa