Kitendawili cha COVID-19 virusi vinavyoibuka inapotimu miaka 100

14Jul 2020
Michael Eneza
Dar es Salaam
Nipashe
Kitendawili cha COVID-19 virusi vinavyoibuka inapotimu miaka 100

WAKATI baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam na hata kwingineko nchini ingawa hali zao inatofautiana wanaanza kusahau woga waliokuwa nao wa baa la corona, hali inaendelea kuwa tete katika nchi nyingi duniani.

Jitihada za kufungua shughuli za kawaida zikichuliwa lakini tahadhari zinazozingatiwa hazijawa na mafanikio kama Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika zilizokuwa na maambukizi hafifu ya virusi vya corona.

Katika mataifa mengine juhudi za kufungua njia za uchumi zimekuwa kichocheo cha kupanda kwa kasi maambukizi, tofauti na ilivyo hapa Tanzania na siyo rahisi kutaja sababu ya tofauti kama hizo, labda kwa kuangalia historia ili kupata picha ya tukio hili.

Hili ni eneo mojawapo ambalo wataalamu huenda wanapata kigugumizi kulizungumzia kwani haliendani na elimu ya takwimu kwa mfano kuhusu magonjwa, kuwa magonjwa hayawezi kuzuka kwa vipindi vinavyotabirika, au maradhi kujirudia kwa kipindi maalum.

Suala la kushangaza la COVID- 19 ni kuwa ndicho kilichotokea, kuwa homa ya mapafu inayoitwa Spanish Influenza ilianza kuenea nchini Hispania na Ureno iliyozuka mwaka 1919 na kudumu kwa miaka mingi.

Historia inaonyesha kuwa iliua watu milioni 50 kote duniani na katika Bara la Afrika ilisambaa kwa kiasi baada ya vita kuu vya kwanza vya dunia, ila linalokumbukwa ni kwamba bara hilo lilipoteza watu milioni 2.5.

Bado hakuna uwezo wa kulinganisha kufariki kwa watu wakati huo na katika janga la COVID-19 hivi sasa kwa sababu siyo rahisi kupata picha ya dawa zilizotumiwa kwa wakati huo.

Ila kwa kulinganisha unawezekana kuwa nyingi kati ya dawa za kila siku za hospitalini ambazo baadhi zimetumika kutibu watu wenye maambukizi hafifu ya COVID-19 hazikuwapo na zimetengenezwa katika kipindi kilichofuata au kuanza kusambaa duniani.
Ila kama walikuwa na ufahamu wa dawa za miti, hizo zilikuwapo siku zote na huenda pia zilisaidia kuponya wengi.

Hivyo, kuna tatizo la kufuatana kwa janga la corona kutoka mwaka 1919 na kuzuka tena ugonjwa kama huo halafu kwa mapana hayo hayo mwaka 2019.

Hata kama ulianzia China na siyo Hispania kama awali. Kama ni ugonjwa peke yake, kwa maana ya mfumuko wa virusi kutoka kwa mnyama vilipogusa ngozi ya binadamu, au kuingia mwilini endapo nyama hiyo haikuiva vizuri, iweje uwe na mfuatano wa miaka 100 kamili?

Halafu mfuatano huo unaleta hisia ya kuwapo na mwingine wa kuwapo maradhi kama hayo mathalani influenza ya karne iliyopita ilivyoendelea kwa muda mrefu na kuvuruga uchumi duniani COVID-19 pia ina mwelekeo huo.

Kilicholeta wakati huo ni uchumi wa dunia kuvurugika haikuwa kukosekana kwa kazi za kufanya ila kukata tamaa kwa watu wengi, baada ya watu milioni 40 kuwa wameshapoteza maisha, miaka 10 baadaye, 1929. Ndiyo kilianza kipindi kilichoitwa cha mdororo mkuu wa uchumi au great depression, kilichodumu hadi mwaka 1932 ambako Marekani iliingia katika mwelekeo wa sera ulioitwa ‘makubaliano au agano jipya ‘new deal,’

kati ya watu na serikali kuhusu uwezeshaji kiuchumi.

Suala ni jinsi gani mdororo wa uchumi ambao umeanza kuenea duniani kutokana na COVID-19 utaipeleka dunia katika ‘makubaliano mapya’ ya kiuchumi ili maradhi hayo yaishe ndicho kinachosubiriwa.

Dhana hiyo ni mfuatano mwingine ambao unawezekana kihesabu, kuwa kutokana na kufuatana miaka 100 kwa corona ya mwanzo wa karne iliyopita na hii ya mwanzo wa karne ya 21, huenda kuna uwezekano kuwa vipengele vya mfumuko wa Spanish Influenza na corona ya sasa vitafanana.

Dhana hiyo ina umuhimu kiasi fulani kwa sababu inaondoa ‘ukungu’ au ‘utando wa buibui’ katika mijadala ya mwelekeo wa uchumi duniani katika mazingira ya maradhi hayo, kuondoa kigezo cha kufananisha na vita kuu vya pili . Havifanani.

Wataalamu wengi zaidi huko ng’ambo wanapenda kufananisha kipindi hiki na vita vya pili kwani nchi za Magharibi zilishinda na baada ya hapo makubaliano mapya ya Marekani yalianza kutumia nchi za Ulaya ili kuondoa hitilafu za kimfumo yaliyofikisha mataifa hayo katika vita, hasa Ujerumani na Ufaransa, na kusaidia Uingereza kuinua tena uchumi wa kiraia, si kuzalisha silaha.

Kutaka kutumia mfano huo kwa janga la COVID-19 ni kumalizia ‘new deal’ bila kianzio cha aina hiyo. Halafu mwaka 1945 kisayansi ni wakati wa viwanda vya ajira nyingi, wakati corona inachochea kuweka kwenye mashine-kazi ili bei zipungue na viwanda visife.

Wataalamu wana kazi mbele yao, yaani kupambana na COVID-19 wakipanga kutoka kwa utaratibu wa kuinua uchumi si kutafakari vifo vya mamilioni ya watu kwani kuna dalili kuwa corona haitamalizika kipindi cha joto katika nchi za Ulaya na Marekani.

Misitu ya Brazil ina joto mwaka mzima lakini corona inaangamiza makabila yaliyojificha ndani kabisa ya misitu hiyo.

Endapo majira ya baridi yatafikiwa halafu jitihada za chanjo nazo hazitaweza kuleta majibu chanya kama ilivyokuwa kwenye dawa za ‘hydroxyl-chloroquine’ aliyoipigia chapuo Rais Donald Trump, ambayo haitibu, labda ni mitishamba itakayosaidia, ila inafaa tu kwa kupunguza matatizo mepesi siyo mapafu yanapotoboka na damu kuganda sehemu mbalimbali za mwili.

Habari Kubwa