Kodi za majengo, laini za simu na miamala zifafanuliwe kwa umma

13Jun 2021
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Kodi za majengo, laini za simu na miamala zifafanuliwe kwa umma

KESHO wabunge wataanza mjadala wa bajeti ya serikali katika maeneo ya vipaumbele, kodi zilizoondolewa, kupunguzwa na kuongezwa kwa mwaka 2021/22.

Wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi, watazungumza kwa niaba ya wananchi wa majimbo na makundi mbalimbali kisha kama watakubali watapitisha bajeti hiyo ambayo itaanza kutekelezwa Julai Mosi, mwaka huu.

Kwa ujumla, bejeti imeuma na kupuliza kwa maana ya kwamba yako maeneo yenye maumivu kama kwenye kodi mpya kwa laini za simu, miamala na ulipaji wa kodi ya ardhi kupitia luku za umeme pamoja na nyongeza ya kodi kwenye mafuta ya magari kwa ajili ya barabara.

Yako maeneo yenye kicheko hasa kwenye makosa ya usalama barabarani kwa bajaji na bodaboda na bidhaa za zinazozalishwa nchini kama za ujenzi  ambazo zinatumiwa na wananchi wengi.

Pia kuna ubunifu katika kuwa na vyanzo vipya vya mapato kama kodi za majengo kulipwa kwa kutumia luku kila mwezi maana yake serikali ina uhakika wa kupata fedha kila mwezi kwa kuwa umeme ni hitaji la lazima kwa kila aliyeunganishiwa.

Ni jambo zuri ila linahitaji kufafanuliwa vyema hasa kwa kuwa ziko nyumba ambazo wanaishi wapangaji ambao wana wajibu wa kulipa bili za umeme wenyewe na ziko nyumba kwenye paa moja lakini wanaishi wapangaji wengi kulingana na muundo wa ujenzi wa mhusika.

Pia ziko nyumba za ghorofa wanaishi watu wengi, lakini ziko nyumba za wananchi wa hali ya chini sana kule vijijini ambao hata kununua umeme ni changamoto bali hununua pale wanapota akutumia yaani kuwashataa kwa muda mfupi sana usiku na kuzima ambaye atalipa sawa na mwenye nyumba ya biashara.

Pamoja na ubunifu huu ambao ninauunga mkono, bado kunahitajika ufafanuzi ili kuondoka mkanganyiko na usumbufu.

Lakini sasa ni wakati wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme kwa kuwa bado kuna wananchi wengi wameshalipia lakini bado hawajafikishiwa huduma hiyo na wengine wanatamani iwafikie lakini haiwezekani kwa kuwa wanahitaji kugharamia nguzo nyingi.

Kwa tafsiri rahisi ni kiwa bajeti imefunganisha makazi na huduma ya umeme kwamba kwa kadri wananchi wengi watakavyopata umeme ndivyo serikali itaendelea kupata kodi nyingi.

Lingine ni laini za simu kutozwa kodi kulingana na matumizi kwamba ni Sh. 10 hadi 200 kwa siku. Hili linapaswa kufafanuliwa kwa kuwa wako ambao hawaweki fedha kabisa kwenye laini zao bali hupigiwa tu. Lakini  kuna ambao simu ni sehemu ya kazi lazima wawe hewani muda wote kama waandishi wa habari.

Kuhusu kutoza kodi kwenye miamala ya simu kuanzia Sh. 10 hadi 10,000 kwa kadiri ya matumizi ni muhimu sana nalo likamulikwa kwa kuwa wako watakaoumia au inaweza kupunguza matumizi ya kutuma na kupokea fedha mtandaoni.

Lakini wako mawakala wanaotoa huduma ya kutuma na kupokea fedha ambao wanalipa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kodi za halmashauri walizomo ambayo si chini ya Sh. 200,000 kwa mwaka. Je, hawa nao watatozwa kodi ya laini za simu na miamala?

Ikiwa watatozwa kodi ya laini ya simu kwa kadiri ya matumizi ni wazi kuwa matumizi yao yatakuwa ya Sh. 200 mwa siku maana yake ni Sh. 6,000 kwa mwezi na 72,000 kwa mwaka, hivyo kama ana laini nne maana yake ni Sh. 288,000 kwa mwaka.

Mtu huyu bado hajatozwa kodi ya miamala na kwa kuwa kazi yake ni kutuma na kupokea fedha maana yake anamzunguko mkubwa wa fedha hivyo anatakiwa kulipa Sh.10,000 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh.120,000 kwa mwaka.

Ukijumlisha kodi hizi zote maana yake anayefanya biashara ya fedha mtandaoni akiwa na laini nne anapaswa kulipa kodi ya zaidi ya Sh. 600,000 kwa mwaka, ndiyo maana nawaza kwa sauti bila ufafanuzi wa kina kuna uwezekano wa watu kuumia na kufunga biashara.

Hakuna ubishi kasi ya ukuaji wa biashara za fedha mtandaoni kutokana na kodi zilizopo faida yake imepungua sana kiasi cha watoa huduma kutopata faida kama iliyopatikana zamani,lakini sasa zimekuja kodi nyingine mpya.

Ufafanuzi wa serikali utasaidia kustawisha biashara nchini, kwa kuwa kila mtu atajua matumizi yake kwa mwezi ni kiasi fulani basi analipa kiasi fulani, lakini kodi nyingine kama TRA na halmashauri bado zitaendelea kuwepo au la, kama atazilipa maana yake huyu mwananchi ana mzigo mzito wa kubeba.

Habari Kubwa