Kompyuta yaanza kufikiri kibinadamu

23Mar 2019
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Kompyuta yaanza kufikiri kibinadamu

“KITAALAMU teknolojia hii huitwa Artificial Intelligence (AI) ambayo ni jihudi za wanasayansi wa kompyuta kuifanya kompyuta iweze kujifunza kama binadamu wanavyojifunza.

Niseme hivi: “It is an attempt to build computing machines or programs that mimic reasoning of human.”

Ni maelezo ya Dk. Katule Ntwa-pichani, ambaye ni mhadhiri katika Idara ya Mifumo ya Kompyuta na Hisabati ya Chuo cha Ardhi, jijini Dar es Salaam, anapozungumza na Nipashe kuhusu utaalamu huo mpya wa kuifanya ‘kompyuta kuwa kama mtu.’

Awali Dk. Ntwa alitoa maelezo yake kwenye Siku ya Maadhimisho ya Miaka 55 ya Ushirikiano wa Kiufundi na Kiuchumi baina ya India na Mataifa ya nje ikiwamo Tanzania, hafla ya ushirikiano huo unaojulikana kama India Technical and Economic Cooperation (ITEC) , ilifanyika katika Ubalozi wa India Dar es Salaam na kuwapa nafasi walionufaika na mpango wa ushirikiano kuelezea wananchi jinsi walivyonufaika.

Dk. Ntwa, akiwa miongoni mwa waliosoma utaalamu wa kisasa wa kompyuta baada ya kueleza kwa ufupi kwa washiriki, anafanya mahojiano na Nipashe na kueleza zaidi juu ya utaalamu wa ‘Artificial Intelligence’ na jinsi unavyoweza kutumika hapa nchini.

Anaendelea kueleza kuwa kawaida wanasayansi wanapotaka kompyuta ifanye kazi fulani lazima waiwekee programu. Ndiyo maana kuna msemo kuwa ‘garbage in garbage out’.

Na programu huandaliwa na wataalamu wa programu za kompyuta, kwa njia hii hawaifunzi kompyuta bali wanaiwekea maelezo ya nini cha kufanya.

“Kwenye Artificial Intelligence badala ya kuipa kompyuta maelezo ya nini cha kufanya, tunaipa mifano ya kitu fulani halafu kupitia hiyo mifano kompyuta inapata maarifa ya jinsi ya kufanya kitu hicho tunachokikusudia,” anafafanua Dk. Ntwa.

Mtaalamu huyu anafafanua kuwa lengo ni kuiwezesha mashine hiyo inapokutana na mfano ambao haijawahi kufundishwa au kuonyeshwa, iweze kutumia utaalamu ‘knowledge’ iliyonayo kusema na kuona kwamba hiki ni kitu fulani au hapa kuna uwezekano wa kuwepo kitu fulani.

Moja ya maeneo maarufu ya ‘artificial intelligence’ ni kwenye utaalamu wa ‘machine learning.’

Hapo wataalamu wanaweza kuifundisha kompyuta kwa kutumia data ambazo ni taarifa mbalimbali ili iweze kufanya utabiri. Mfano mtaalamu anaweza kuwa na data zinazoonyesha hali ya mvua kwa miaka kadhaa pengine mwaka juzi, jana na sasa ambayo inaonyesha, nyuzi joto, kiasi cha unyenyevu na kiasi cha mvua zilizonyesha kwa kila siku.

Sasa unaweza ukaifundisha kompyuta na data za nyuma, kiasi kwamba ikawa na uwezo wa kutabiri kama mvua itanyesha kwa kiasi gani, sababu imeshaonyesha mifano mingi ya kwamba nyuzi joto ikiwa hivi na unyevu nyevu ukiwa hivi, matokeo ya mvua huwa hivi.

Kwa hiyo kama nyuzi joto na unyevunyevu vina uhusiano na kunyesha au kutonyesha kwa mvua, basi ukipata nyuzi joto ni ngapi, na unyevu nyevu ni kiasi gani, inaweza kutabiri kunyesha au kutonyesha kwa mvua.

Dk. Ntwa anasema hilo linaweza kufanywa kwa sababu kompyuta hiyo imeshaonyeshwa mifano mingi. Mathalani, imefundishwa kwamba nyuzi joto zikiwa hivi na unyevunyevu ukiwa hivi, matokeo ya mvua huwa pengine ya namna hii. Kwa hiyo kama nyuzi joto na unyevunyevu vina uhusiano na kunyesha au kutonyesha mvua, ukipata nyuzi joto ni ngapi na unyevunyevu ni kiasi gani, kompyuta inaweza kutabiri kunyesha au kutonyesha mvua.

KUIFIKIRISHA KOMPYUTA

Kompyuta ina ‘memory’ au uwezo wa kutunza kumbukumbu kubwa zaidi kuliko ubongo wa binadamu kwa hiyo inaweza kufanya vitu vingi sana, vikubwa na kwa muda mfupi, anaeleza Dk. Ntwa.

“Lakini, ukilinganisha intelligence, uwezo wa akili ya binadamu na kompyuta binadamu ana akili nyingi zaidi kuliko kompyuta na ndiye aliyeiunda, lakini hana memory –kumbukumbu kubwa ya kutunza mambo kwenye akili yake. Kompyuta ina uwezo mkubwa wa kushughulikia data kubwa zaidi kwa kiwango cha mabilioni kwa muda mfupi mno hata kwa sekunde,” anaeleza.

Mwalimu huyo wa Chuo cha Ardhi, anafafanua zaidi kuwa lengo la AI ni kujaribu kutumia akili za binadamu au ‘intelligence’ yake na kuiweka kwenye kompyuta ili kurahisisha na kufanyakazi kwa weledi zaidi.

MATUMIZI YA AI

Artificial Intelligence inaweza kutumika kwenye maeneo mengi ili mradi data za kuifundisha mashine hiyo kazi na majukumu mbalimbali ziwepo, anasema mtaalamu huyo.

Anakiri kuwa tatizo ambalo linaikabili Tanzania ni upatikanaji wa data kwa ajili ya kuipa au kuifundisha mashine hiyo ili ifundishwe.

Hata hivyo, anasema sayansi hiyo inaweza kutumika katika kufanya uchunguzi wa tiba mfano, saratani. Kinachofanywa ni kuifundisha picha za seli ya kansa zinavyofanana na ikishafunzwa ikionyeshwa picha ngeni inaweza kutambua kama ni kansa au laa.

Anatoa mfano wa pili kuwa ni benki zikitaka kujua kama wanalioko watarejesha ama watakwama wanatumia AI kwa kuifundisha kompyuta data za watu ambao tayari walishawahi kushindwa kulipa na ambao hawajawahi kukimbia mkopo.

Kupitia mafunzo wataitumia kompyuta kujua iwapo mteja anayeweza kulipa au hawezi, kwa hiyo mashine inajua ni vigezo vipi na kwa kiasi gani uwezekano ni mkubwa wa kulipa au kukimbia na mkopo.

Aidha, Dk. Ntwa, anasema AI inaweza kutumiwa na Wizara ya Afya kwa kuwa inazo data za miaka mingi ambazo zimekusanywa kutoka vituo mbalimbali vya afya kuonyesha kiasi cha watu waliopimwa malaria au pengine ugonjwa wowote, na idadi gani waliogundulika na maradhi hayo.

“Kupitia AI wanaweza kutabiri wapi na kipindi gani kutakuwa na mahitaji makubwa ya dawa za malaria. Kwa hiyo kwa kupitia Artificial Intelligence, serikali na taasisi zinaweza kufanya upangaji bora wa rasilimali zilizoko,” anaeleza.

Si hivyo tu, inawezekana kutumia AI kwenye sekta ya usafiri, mfano mabasi yaendayo haraka ya UDART, kwa sababu tayari wanazo data nyingi kuhusu muundo na taratibu za wasafiri wanaweza kukadiria idadi ya mabasi yanayohitajika kupeleka abiria kwa mfano, Kivukoni, Gerezani, Kimara na Morocco kwa wakati fulani, tofauti na sasa ambapo mwendokasi imekuwa haina mfumo bora wa kuchukua abiria vituoni, anashauri mhadhiri huyo na kuongeza mifano mingine.

“Tunaweza kuwa na data kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima, na jinsi inavyotokea na tukaweza kujua uwezekano wa mgogoro kutokea pale hali fulani inapokuwapo (labda ukosefu wa mvua au picha za satelaiti zikionyesha ukame). Mifano ni mingi sana.

Hata kwenye mambo ya usalama, mashirika ya usalama yanaweza yakakusanya taarifa kwenye mitandao ya kijamii na kuweza kuzipanga kwenye viwango mbalimbali kufahamu uwezekano wa kutokea vitisho na ikasaidia kwenye kufanya maamuzi ya kiulinzi na usalama,” anaongeza kuwa AI ni muhimu sana zama hizi kwa sababu inawezesha kutumia data katika kufanya maamuzi mbalimbali.

ITAENDELEA WIKI IJAYO

Habari Kubwa