Korea Kaskazini yafunika kombora 'masafa ya juu,' mageuzi yanukia

06Dec 2017
Michael Eneza
Nipashe
Korea Kaskazini yafunika kombora 'masafa ya juu,' mageuzi yanukia

UTAWALA wa kiimla wa Korea ya Kaskazini inaelekea sasa umeridhika na hatua iliyofikiwa na jeshi lake katika kutengeneza makombora ya masafa marefu, baada ya jaribio la Jumatano, Novemba 29.

Nchi hiyo ilirusha kombora lililoenda juu kilomita 4,500 na kuruka umbali wa kilomita 960, umbali na urefu ambao ungekuwa sambamba na anga la dunia ingekuwa ni umbali wa takriban kilomita 13,000, kuweza kutua kokote duniani.

Marekani ilikiri hivyo, Rais Donald Trump akasema atashughulikia suala hilo.

Nchi za Magharibi pamoja na majirani wa Korea ya Kaskazini wanaolengwa zaidi na majaribio yake ya silaha za maangamizi, Korea ya Kusini na Japan, hazikuonekana kutaka hatua za haraka kuchukuliwa.

Diplomasia kuhusu suala hilo hivi sasa inalenga zaidi China, iweke vikwazo zaidi kwa utawala huo wa kiimla wa familia moja ambako mjukuu sasa yuko madarakani, hali ya umwinyi wa Kikomunisti ambayo haijawahi kutokea duniani.

Kiongozi mkuu Kim Jong-un amekuwa akitupiana madongo na Rais Trump, ambaye ameahidi kumaliza suala la tishio la nchi hiyo, lililowashinda marais wanne.

Mchambuzi wa masuala ya ulinzi na diplomasia wa BBC nchini Uingereza, Jonathan Marcos, alisema kuwa inavyoelekea, suala hilo halina jawabu, suluhisho.

Alisema jaribio hilo la hivi karibuni limeonyesha kuwa mdororo wa kujaribisha makombora uliochukua miezi takriban miwili ulikuwa wa kawaida, na haukutokana na vitisho vya Rais Trump au shinikizo la China kwa utawala wa Pyongyang.

Kimsingi Marekani inaisukuma China kuibana zaidi Korea ya Kaskazini iache mpango wake wa silaha za nyuklia, amani ije.

Hivi karibuni Marekani imeirudisha Korea ya Kaskazini katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi kutokana na majaribio yake ya silaha za nyuklia na makombora ya kubeba silaha hizo.

Moja ya vikwazo vipya vinavyotokana na kuwekwa katika orodha hiyo ni kubana shughuli za meli za Korea ya Kaskazini, na makampuni ya China yanayofanya biashara na nchi hiyo.

Jaribio hili litaifanya Marekani itafakari kwa nguvu, kwani kimsingi eneo lake lote liko katika dira ya kuweza kutua makombora ya nyuklia kutoka huko.

Jaribio la Novemba 29 lilikuwa la sita muhimu mwaka huu, kila wakati ubora na kiwango cha umbali wa makombora kikiongezeka.

Mara mbili makombora yanayojaribiwa yaliruka juu sana ya anga ya Japan, hali ambayo ilileta wasiwasi mkubwa wa Marekani kuchukua hatua za nguvu dhidi ya Korea ya Kaskazini.

Ila hatua hiyo haikufikiwa kwa sababu hakuna asasi au mali za Japan au Korea ya Kusini zilizofikiwa na makombora hayo.

Wasiwasi ni kuwa endapo siku moja, kwa makosa fulani bomu likaangukia asasi fulani, ya kiraia au ya kijeshi, mlipuko wa aina yake lazima utatokea.

Wataalamu wa Marekani na Korea ya Kusini bado walikuwa wanajiuliza kama kombora la hivi karibuni ni lile la mwezi Julai au ni jipya, lakini hisia kuwa ni jipya na la umbali mkubwa zaidi iliendelea kukubalika.

Hata James Matis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, alisema lilienda juu zaidi kuliko jaribio lolote lingine la awali.

Suala ambalo halikuwa wazi ni kama kulikuwa na haja ya kuchukua hatua zozote mpya, huku maofisa wa Marekani wakisema kuwa jaribio haliondoi nia ya kutafuta muafaka kidiplomasia, inayoendelea.

Kuna vianzio kadhaa vya kuonyesha mwanga jinsi hali hiyo tete ilivyo katika mahusiano ya kimataifa Mashariki ya Mbali.

Mojawapo ni vikwazo vya uchumi kuanza kubana mazingira katika ustawi wa jamii na hata miongoni mwa jeshi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Mwanadiplomasia mmoja aliyetoroka kutoka nchini Uingereza akiwa naibu balozi alisema mwezi mmoja uliopita kuwa hali inaanza kuwa ngumu kwa kila mtu, hata wale ambao wamekuwa wakipuuzia vikwazo kwani haviwagusi kwa kina.

Akifanya mahojiano ya kina na Kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza laWawakilishi nchini Marekani, naibu balozi huyo wa zamani alisema utawala wa Kim Jong-un unaanza kuyumba.

Alishauri kuwa Marekani ielekeze nguvu zake katika ''soft power,' yaani njia za mawasiliano na upokeaji taarifa, habari na maoni ambazo kwa jumla zinaweza kubadilisha fikra nchini Korea Kaskazini.

Hali ya uchumi ikiendelea kuzorota endapo China itaanza kuchukua hatua za dhati zaidi kumaliza tatizo hilo, utawala huo utaanguka.

China imekuwa ikijitahidi kwa kiwango fulani kuwezesha mabadiliko Korea ya Kaskazini, lakini haijataka kuingilia kwa nguvu, ila kushawishi.

Wakati fulani ilikuwa inategemea kuwa mjomba wa Kim Jong un aitwaye Jang Song-thaek ambaye alikuwa mume wa shangazi wa Kim (dada wa kuzaliwa kwa baba yake, Kim Jong-Il) angemvuta mtawala huyo kijana kufuata njia ya China kuleta mageuzi.

Ilipoanza kufahamika ushauri wa Jang ni kubadili mwelekeo kuleta ufanisi zaidi kiuchumi, Kim akahisi kuwa njia hiyo itaifikisha Korea ya Kaskazini katika demokrasia na kuondoa utawala wa kifamilia.

Hivyo akaagiza mashtaka ya uhaini yafunguliwe, Jang akauawa.

Njia mojawapo ambayo China inaweza kutumia kuhakikisha mageuzi yanaingia Korea ya Kaskazini ni kuruhusu wananchi wa eneo hilo dogo kutumia mpaka wa China kuondoka huko ili kukimbilia Korea ya Kusini ambako wanakaribishwa.

Ndiyo njia iliyoleta mabadiliko (mapinduzi) kutoka ukomunisti huko Ujerumani Mashariki kuelekea mwisho wa 1989 wakati jeshi la nchi hiyo lilipokataa kuingilia kati watu wakivunja kipande cha ukuta wa Berlin kuingia upande wa Magharibi wa jiji, ili kuwa huru.

Wakati Rais Trump amekuwa na mwelekeo wa kutaka 'moto na ghadhabu' vitumike kuondoa tishio la silaha za nyuklia za Korea Kaskazini, maofisa wa ngazi za juu wa utawala wa Marekani wanajua kuwa nguvu za China za kuibana nchi hiyo ndogo kiuchumi zinatosha kuleta mabadiliko.

Ndiyo maana utawala huo sasa umerudishwa katika orodha ya nchi au vikundi vinavyounga mkono ugaidi, kwani umewahi kufanya mashambulio kadhaa nje ya nchi, kwa mfano kuuawa kaka yake Kim, aitwaye Kim Jong-nam aliyeuawa kwa kutumia kipulizo cha manukato ya sumu, 'nerge gas' katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kuala Lumpur nchini Malaysia mnamo Februari 13 mwaka huu.

Mwanafunzi wa Kimarekani aliteswa na polisi kwa madai ya kipuuzi ya kutaka kuiba picha ya propaganda, akarudishwa kwao akiwa amepoteza fahamu, akafa punde.

Raia wa Japan, Korea ya Kusini wanakamatwa mpakani, wanazuiliwa miaka mingi; raia wanazuiliwa kupata chakula ikisikika kuwa kuna tetesi kuwa baadhi hawaupendi utawala huo.