Korea Kusini yapendekeza mazungumzo na Kaskazini

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Korea Kusini yapendekeza mazungumzo na Kaskazini

KOREA Kusini imetoa ombi la kutaka kufanyika mazungumzo ya juu na Korea Kaskazini Januari 9, kujadili ikiwa kuna uwezekano wa jirani yake huyo kushiriki mashindano ya Olimpiki ya msimu wa baridi mwaka huu wa 2018.

Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in (kushoto) akiwa na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un. PICHA: MTANDAO

Hii ni baada ya kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un kusema kuwa alikuwa anafikiria kutuma timu kwenda Pyeongchang nchini Korea Kusini kwa mashindano hayo mwezi Januari.

Alisema kuwa nchi hizo mbili zinahitaji kukutana kwa dharura kuzungumzia uwezekano huo wa kushiriki mashindano hayo.

Mapema Rais wa Korea Kusini alisema kuwa ameiona hiyo kama fursa ya kuboresha uhusiano ulioharibika kati ya nchi hizo.

Waziri wa mahusiano wa Korea Kusini Cho Myoung-gyon alipendekeza jana kuwa wawakilishi wakutane katika kijiji cha Panmunjon.

Kijiji hicho kilicho eneo lenye ulinzi mkali la DMZ mpakani ndipo mazungumzo kati ya nchi hizo yamekuwa yakifanyika.

Bado haijulikani ni nani atahudhuria mazungumzo hayo na pia bado Korea Kaskazini haijajibu.

Mazungumzo ya mwisho kati ya nchi hizo yalifanyika Desemba mwaka 2015 katika eneo la pamoja la viwanda la Kaesong.

Yalimalizika bila makubaliano yoyote na ajenga ya mazungumzo haikutangazwa.

Ni wanariadha wawili tu wa Korea Kaskazini waliofuzu kwa mashindano ya mwaka huu ya msimu wa baridi nchini Korea Kusini. BBC