Kuelekea siku 100 za Rais Magufuli Ikulu na angalizo la Wabunge

10Feb 2016
Beatrice Shayo
DAR
Nipashe
Kuelekea siku 100 za Rais Magufuli Ikulu na angalizo la Wabunge

BAADHI ya wabunge wamemsifu utendaji kazi wa Rais John Magufuli wa siku 100 tangu alipoingia madarakani, huku wengine wakisema ameshindwa kudhibiti hali ya kisiasa Zanzibar.

Rais Magufuli leo ametimiza siku 98 tangu aingie Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam na kesho kutwa atatimiza siku 100.

Dk. aliapishwa Novemba 5 mwaka jana na baada ya hapo aliingia lango la Ikulu kwa ajili ya kuanza kazi ya kuwatumikia wananchi.

Licha ya Rais Magufuli kuhsindwa kumaliza mgogoro wa ksiasa Zanzibar, lakini ameweza kuanzisha utaratibu wa kubana matumizi ya fedha za serikali ikiwemo kufuta safari za nje ya nchi ambazo zilikuwa zinagharimu mabilioni ya fedha kila mwaka.

Utaratibu huo wa Rais Magufuli ulipokelewa kwa furaha na wananchi wa kawaida na baadhi ya watumishi wa umma ambao ni waaminifu na wenye uchungu na nchi yao.

Zikiwa zimebaki siku tano, Rais Magufuli kutimiza siku 100 za utawala wake, ameonyesha mfano nzuri ambao unatakiwa kuigwa na Marais wengine ambao watafuata baada ya yeye kumaliza kipindi chake.

Wanasiasa wameazungumzia utendaji kazi wa Rais Magufuli na kusema ni mzuri lakini ameshindwa kushughulikia mgogoro wa kisiasa uliopo Zanzibar ambao unaweza kuleta madhara makubwa kwa nchi.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe anasema Rais ameshindwa kudhibiti hali ya kisiasa Zanzibar.
“Hii itakuwa na madhara makubwa sana kwenye uchumi wa nchi yetu,” anasema Zitto.

Zitto anasema suala hilo linatakiwa kuangaliwa kwa upana ili pasiwepo na madhara katika nchi.

Aidha, anasema Rais anatakiwa kujenga mfumo wa uwajibikaji katika nchi ili haya anayoyafanya sasa yaweze kufanywa na Rais mwingine.

Zitto anasema kuwa vita ya ufisadi anayoifanya Rais Magufuli lazima iungwe mkono na Watanzania wote wenye mapenzi na nchi yao, lakini isiwe ni vita vya visasi au kuvunja sheria.

“Lazima aendeleze ukali lakini aweke utu mbele mpaka sasa Rais ameonyesha uwezo wake mkubwa wa kupambana na 'majizi' lakini hajaanza kuongoza bali anatawala,” anasema Zitto

Zitto anasema kuwa Rais Magufuli anabadili watu kwa mfumo ule ule akitolea mfano kuwa Takukuru ipo vile vile japo kambadilisha Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.

“Mamlaka ya Mapato (TRA) ipo vile vile na hata kwa upande wa Bandari ipo vile vile,” anasema Zitto

Anasema mapato ya mwezi Desemba mwaka jana yaliongezeka na kufikia Sh. trilioni 1.4 ilipofika Januari mwaka huu yameshuka mpaka Sh. trilioni 1.04. hii maana yake ni kwamba makusanyo yale yalikuwa siyo mabadiliko yaliyofanyika,” anasema Zitto

Aidha, Ziito anasema hadi sasa Rais hajatangaza mali zake ama madeni aliyonayo na hata Mawaziri wake hawajulikani wanamiliki nini na kwa maana hiyo bado anaendeleza mfumo ule ule.

Zito ambaye ni Mbunge pekee kupitia Chama ACT-Wazalendo katika jimbo la Kigoma mjini anasema, ili Rais Magufuli aisaidi nchi ni lazima aweke miiko mizuri ya uongozi ambayo itasaidia kudhibiti mianya ya rushwa.

Naye Mbunge wa jimbo la Busega (CCM), Dk. Raphael Chegeni anasema kupitia uongozi wa Rais Magufuli amejifunza mambo mengi kwani ni kiongozi mwenye dhamira safi anayetaka kuiona Tanzania inakuwa mbali kiuchumi na kimaendeleo.

Anasema kuwa ahadi zake wakati wa kampeni amefanikiwa kuzifanyia kazi japo ameingia madarakani akiwa anakabiliwa na changamoto ya nchi kuwa na madeni makubwa.

Dk. Chegeni anasema Rais amekabidhiwa nchi ikiwa na madeni makubwa, lakini anajitahidi kupambana nayo ili kuhakikisha Tanzania inakuwa mfano wa maendeleo na hili linawezekana.

Anasema Rais Magufuli ameshughulikia suala la ulegevu katika uendeshaji wa serikali, kwani kiwango cha uwajibikaji kilikuwa kimeshuka.

Kuhusu nidhamu ya watumishi wa umma katika kipindi cha siku 100, anasema Rais Magufuli ameweza kuwabadilisha na kuachana na kufanya kazi kwa mazoea.

Kada huyo wa CCM ambaye ni Mbunge wa jimbo la Busega anasema, suala la rushwa bado limepamba moto kwa kuwa wapo watumishi wa umma ambao wanajinufaisha rasilimali za nchi badala ya kuangalia maslahi ya taifa.

Katika kipindi cha siku 100 ambazo zinakamilika wiki ijayo, Rais Magufuli amejitahidi kutatua kero mbalimbali zilizokuwa zinaikabili nchi ikiwemo kuwaajibisha viongozi wala rushwa.

Mapato ya serikali yameongezeka kutokana na Rais Magufuli kuwa mkali na kubana mianya ya rushwa ambayo ilikuwapo katika serikali ya awamu ya nne.

Dk. Chegeni anasema Rais hakutakiwa kukutana na matatizo makubwa likiwemo lile la Zanzibar, hivyo anatakiwa kuangalia namna bora ya kushughulikia suala hilo ili lisilete madhara.

Anamshauri Rais Magufuli kuendelea kujenga mfumo bora wa utawala wa kisheria ambao utakuwa na ufanisi , kuchochea ukuaji wa uchumi na kulinda rasilimali za nchi.

Mbunge wa Donge Juma Sadifa (CCM), anasema siku 100 za Rais Magufuli amefanikiwa kuongeza mapato ya serikali pamoja na kurudisha nidhamu ya utendaji wa serikali.

Kuhusu sekta ya elimu anasema, Rais ametimiza ahadi yake ya wanafunzi kusoma bure jambo ambalo limesaidia kuihamasisha jamii kuongeza kasi kuwapeleka watoto wao shule.

Anasema kwa sasa nchi imepata viongozi waadilifu ambao watasaidia kupunguza rushwa kwa kuwa watumishi wa serikali wanawajibika.
Anasema siku 100 za Rais Magufuli zimewaliza watu wengi hivyo ni vizuri busara ikatumika hasa kwenye suala la ubomoaji wa nyumba za wakazi wa mabondeni.

Sadifa anasema kuwa wananchi hao wakati wanajenga nyumba zao serikali ilikuwepo siyo kwamba ilikwenda likizo, hivyo inatakiwa kuwasaidia.

“Wale ambao walikatazwa na kujenga wachukuliwe hatua lakini hao wengine inatakiwa busara itumike kwa kuwa wakati wanajenga serikali ilikuwapo na ilikuwa inaona siyo kwamba ilikuwa likizo,” anasema

Baadhi ya wanasiasa ndani ya CCM na upinzani wanakiri kwamba utendaji wa Rais Magufuli unakwenda vizuri ingawa wamekuwa wakitoa angalizo.

Angalizo wanalotoa kila mmoja anapozungumza ni kuhusu mgogoro wa Zanzibar ambao wanaeleza kwamba umeweka dosari katika serikali yake ya awamu ya tano.

Wanasema ukiondoa dosari hiyo, mambo mengine Rais Magufuli ameendelea kufanya vizuri tangu alipoingia Ikulu.

Mbunge wa Jimbo la Temeke (CUF), Abdallah Mtolea, anatoa angalizo kwamba anakifanya Rais ni kama kampeni ili wananchi wampigie makofi badala ya kutatua kero za wananchi.

Anasema Watanzania wana matatizo mengi ya msingi ikiwamo suala la ukosefu wa maji, dawa, umeme, elimu na miundombinu, hivyo walitegemea kuona amejipanga vipi kuyatatua kwani wapo waliomchagua kwa ajili ya kuona kero zao zinashughulikiwa.

“Wananchi wanataka kujua Rais mpya anakuja na mkakati gani wa kushughulikia kero za wananchi na siyo kuwatimua kazi wafanyakazi,” anasema Mtolea

Anasema siku 100 za Rais amezitumia kwa ajili ya kutaka sifa za kisiasa, kwani hajaanza kazi kwani anatakiwa kuleta mipango ya kutatua matatizo ya wanannchi.

Mbunge huyo ambaye ameingia bungeni kwa mara ya kwanza anasema, Watanzania hawahitaji kuona viongozi gani wameachishwa kazi kwani jambo hilo ni la kawaida kwa serikali yoyote kuwatimua watumishi wasiozingatia maadili ikiwamo kuiba.

Habari Kubwa