KUELEKEA TANZANIA YA VIWANDA..Hivi ndivyo zilivyo haki,wajibu wa mlaji

03Nov 2017
Sanula Athanas
Nipashe
KUELEKEA TANZANIA YA VIWANDA..Hivi ndivyo zilivyo haki,wajibu wa mlaji
  • Profesa Mlimani alia biashara bado ‘ovyo ovyo’
  • FCC yaeleza nchi ilipo, ‘madudu’ wayakutayo mtaani

MACHI 15, 1962, Rais wa Marekani kwa wakati huo, John Kennedy aliasisi haki nne za mlaji (mtumiaji wa mwisho wa bidhaa au huduma) kutokana na hotuba yake juu ya utetezi wa walaji wa bidhaa na huduma.

kariako.

Katika hotuba yake siku hiyo, Rais Kennedy alisema: “Kama mteja anatumia bidhaa zenye viwango duni, kama bei ni kubwa, kama dawa ni si salama na ina thamani kama mteja hawezi kuchagua bidhaa ambazo amepewa taarifa zake za kutosha, basi dola (pesa) zake imetumika vibaya, afya na usalama wake unakuwa umetishiwa na maslahi ya nchi yanakuwa yametetereshwa.”

Ni kutokana na kauli hiyo ya Rais Kennedy kila Machi 15 imekuwa ikiadhimishwa kuwa ‘Siku ya Walaji Duniani.” Hiyo ni tangu mwaka 1983 ilipoadhimiwa na Shirikisho la Walaji Duniani (CI), ambayo ni miaka 21 baada ya kauli ya Rais Kennedy.

Hayo ni maadhimisho yanayotumika kuwaunganisha walaji wote duniani na kuwakumbusha haki na wajibu wao, wakibadilishana uzoefu na changamoto zinazowakabili.

Haki 4 za Rais Kennedy

Kuna haki nne za walaji zilizoasisiwa na Rais Kennedy, kutokana na hotuba yake ya Machi 15, 1962. Hizo ni; Haki ya Usalama, Haki ya Kuchagua, Haki ya Taarifa na Haki ya kusikilizwa.

Hata hivyo, kilichoanzishwa mwaka 1960, kiliongeza haki tatu na kuzifanya haki za walaji kuwa saba, hata Aprili 9, 1985, Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Azimio Namba 39/148 liliridhia kinachoitwa ‘Mwongozo wa Sera za Kimataifa za Kuwalinda Walaji’ au inavyotamkwa 'Guidelines for Consumer Protection' (UNGCP).

Mwaka 1999, haki nyingine iliongezeka kutokana na marejeo ya UNGCP na kufanya uwapo wa haki nane zinazotambulika na kuridhiwa kimataifa hadi sasa.

Haki hizo za walaji ni: Kupata mahitaji muhimu; Usalama; Kupata taarifa; Uchaguzi; Kusikilizwa; Kulipwa fidia; Kupatiwa elimu; na Mazingira mazuri na endelevu.

Tanzania ya Viwanda

Wakati Tanzania ikiwa katika mkakati wa kuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati katika miaka nane ijayo, mtaaluma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja, anasema kuna haja nchi kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha inawalinda walaji kwa kudhibiti bidhaa bandia.

"Bidhaa zinazoingia pasipo kuzingatia sheria, siyo rahisi kushindana na zinazozalishwa kwa kufuata sheria kwa sababu hizo zisizofuata sheria zinakuwa hazina ubora na bei yake ni ya chini, kwa hiyo, wananchi ni rahisi kukimbilia hizo kuliko hizo za ndani ambazo zinauzwa kwa bei ya juu,” anasema Profesa Semboja.

Msomi huyo anaongeza: "Mbaya zaidi, bidhaa hizo kuwapo katika kipindi hiki ambacho Tanzania inapigana kujenga nchi ya viwanda, huwezi kujenga au kuinua viwanda vya ndani kama mianya ya uingiaji wa bidhaa feki haijazibwa vya kutosha kwa sababu utazalisha, lakini hautapata soko maana limechukuliwa na bidhaa feki.

"Tunachotakiwa kufanya ni kujenga mifumo bora ya biashara kuhakikisha mamlaka zote zinashirikiana kuziba mianya inayotumika kuziingiza, lakini pia kujenga mfumo bora kwa wafanyabiashara wadogo ambao utawasaidia wasitumike katika uuzaji wa bidhaa hizo."

Wakati Profesa Semboja 'analia' na bidhaa bandia kuelekea Tanzania ya viwanda, Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Tume ya Ushindani (FCC), Frank Mdimi, anabainisha mambo kadhaa ya kulalamikiwa.

Anasema, kati ya mwezi Januari na Julai mwaka huu, tume hiyo kupitia Sheria ya Alama za Bidhaa ya mwaka 1963, ilikamata bidhaa feki zenye thamani ya Shilingi milioni 441.4 katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Mtwara.

Anasema, bidhaa bandia zilizokamatwa ni spika 59 za muziki zilizokuwa na nembo ya kughushi zenye thamani ya Sh. milioni 53.1; spika 30 za muziki zilizokuwa na nembo ya kughushi, zikiwa na thamani ya Sh. milioni 15; kofia ngumu za waendesha pikipiki 1,246 zilizokuwa na nembo ya kughushi zenye thamani ya Sh. milioni 18.64 na pikipiki nane zilizokuwa na nembo ya kughushi, pia njini saba za pikipiki.

Mdimi anataja thamani kuwa vyote vilikuwa na thamani ya Shilingi milioni 19.4; vijiko vitatu vya kubebea mizigo vilivyokuwa na nembo ya kughushi vyenye thamani ya Shilingi milioni 167.6 na jozi 5,889 za viatu zilizokuwa na nembo ya kughushi, zenye thamani ya Shilingi milioni 235.56.

Mdimi anasema wafanyabiashara waliokamatwa na bidhaa hizo bandia, wapo kwa sasa wako katika hatua mbalimbali za kukamilisha matakwa ya sheria kuhusiana na adhabu walizopewa, kwa mujibu wa Sheria ya Alama za Bidhaa na kanuni zake ambazo zinataja adhabu ya kifungo jela, kupigwa faini au vyote kwa pamoja.

Wajibu wa mlaji

Ofisa Mwandamizi Utetezi wa Mlaji wa FCC, Joshua Msoma, wajibu wa mlaji ni kwamba anapaswa kuzingatia mambo manane katika kufanya manunuzi ya bidhaa au huduma.

Anayataja mambo hayo kuwa : Mdadisi na makini katika manunuzi; kuhakikisha matumizi bora na sahihi ya bidhaa na huduma kwa maslahi mapana, kujijengea uwezo na ushawishi katika kukuza na kulinda maslahi yake, na kusoma maelekezo ya bidhaa na huduma kwa makini na kuchukua hatua stahiki.

Msoma anataja wajibu mwingine ni kutafuta taarifa za bidhaa au huduma na kuzitumia kabla ya kufanya manunuzi, kutoa maoni yake kupitia vyama huru vya walaji, kupigania upatikanaji wa bidhaa na huduma bora pamoja na kuwa na matumizi endelevu ya bidhaa na huduma.

"Mantiki ya kumlinda mlaji imejengwa katika misingi mikuu mitatu; Elimu, Utatuzi wa migogoro na Utekelezaji wa sheria," anafafanu Msoma na kuongeza:

"Mlaji kwa sehemu kubwa duniani, hajaweza kutumia vyema fursa za kukabiliana na changamoto katika manunuzi na matumizi ya bidhaa na huduma mbalimbali.

"Changamoto kubwa zaidi kwa mlaji kukosekana kwa mifumo na vyombo huru vilivyo madhubuti vya kutetea na kusimamia maslahi na haki za mlaji."

Msoma anaeleza zaidi kuwa, nchi nyingi zinazoendelea ziko nyuma katika kutambua na kudai haki za mlaji, ikilinganishwa na haki nyinginezo, akitoa mfano wa haki za siasa na jinsia.

Anasema changamoto nyingine kwa mlaji, ni kukosekana mpango mkakati wa kuielimisha jamii juu ya tasnia ya kumlinda mlaji, hususan elimu rasmi kwa walaji katika nchi zinazoendelea.

Mitaala ya Elimu

Msoma anasema, elimu ya mlaji katika nchi zilizoendelea imepewa kipaumbele kikubwa na walaji wana maarifa mapana yahusuyo haki zao na mifumo ya kimasomo, ambayo elimu hiyo hufundishwa katika shule na vyuo.

Msoma anasema, katika nchi zinazoendelea, elimu ya mlaji haijapewa kipaumbele, licha ya kuleta athari hasi katika jamii, zikiwamo za kiafya na uchumi wa walaji.

Anasema, elimu kwa walaji inafundishwa kwa mfumo ulio rasmi katika nchi chache barani Afrika, akitoa mfano wa Afrika Kusini iliyoanza kutoa elimu hiyo mwaka 2006, katika shule za sekondari na vyuo.

Pia, nchini Nigeria kulikoanza kutoa elimu hiyo mwaka 2012 kwenye shule za msingi, sekondari na vyuo.

Anasema elimu ya mlaji inafundishwa katika vyuo vichache nchini, akitoa mfano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule kuu ya Biashara na Uchumi (UDBS).

Habari Kubwa