Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020

01Jul 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020
  • *Kada CCM ataka mgombea binafsi

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza mfumo na utaratibu wa kupata viongozi wa kisiasa-rais, wabunge na madiwani.

Thomas Ngawiya akichangia hoja bungeni enzi hizo. PICHA ZOTE: MTANDAO

Kwa mujibu wa ibara ya 39(1) (c) mgombea yeyote wa nafasi hizo ni lazima awe amependekezwa na chama cha siasa. Kwa hiyo hakuna mgombea nje ya utaratibu huo.

Aidha, ibara ya 67(1)(b) ya katiba hiyo inasema mbunge ni lazima apendekezwe na chama chake na hakuna mgombea anayepatikana tofauti na maelekezo hayo.

Halikadhalika, Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 inazungumzia uteuzi wa wagombea na kuelekeza kuwa ni lazima watokane na vyama vya siasa vilivyosajiliwa na kutambulika kisheria.

Hata hivyo, mmoja wa makada wa CCM, inaona kuwa utaratibu huo unatakiwa kuangaliwa upya, akieleza kuwa unasababisha baadhi ya wanachama wenye uwezo wa kuongoza kukosa nafasi hizo hasa wale ambao hawapendwi na viongozi wakuu wa vyama vyao wanaosimamia uteuzi na kupendekeza wagombea.

Ni maoni ya Thomas Ngawaiya, anayeshauri kuwapo kwa mabadiliko, ambayo yatawezesha Tanzania kuwa na mgombea binafsi ili kuondoa mfumo huo.

Mwanasiasa huyo anasema, si jambo la ajabu kutoa ushauri huyo, kwa vile unalenga kusaidia kila Mtanzania mwenye sifa za kuongoza aweze kupata nafasi hiyo, kupitia chama au nje ya mfumo huo.

Anasema, hiyo ndiyo njia pekee ya kuwezesha Watanzania kushika nafasi mbalimbali za uongozi, vinginevyo wengi wataendelea kukwama kupata uongozi kwa sababu ya mfumo wa kupitia kwenye vyama vya siasa.

Mwanasiasa huyo, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (Cegodeta), anafafanua kuhusu hoja yake katika mahojiano na gazeti hili, jijini Dar es Salaam.

SWALI: Imekuaje leo umeibuika na hoja hii ya mgombea binafsi?

JIBU: Hii hoja siyo ya leo wala juzi. Kwenye miaka fulani iliyopita, nikiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji John Tendwa, tulizungumzia sana mgombea binafsi na alielekea kuona kwamba ni jambo la maana linalowezekana, lakini muda wake uliisha na mimi muda wangu wa ubunge wakati ule ulimalizika, basi hakuna aliyeendeleza tena, lakini bado ninasema kwamba, mazungumzo yangu yalikuwa yamezungumzia sana kwamba, hawa watu wanaotaka wagombea binafsi tuwapo ruhusu, uandaliwe muswada na kupelekwa bungeni na kupitishwa, haitaleta madhara yoyote.

Leo hii ninakumbushia tena kwamba, kuna hatari gani kuruhusu mgombea binafsi? Tumruhusu mgombea binafsi naye anaweza kuleta changasmoto zake, kwa sababu kama yupo wa kushinda atashinda tu.

SWALI: Msingi wa hoja yake ya kutaka mgombea binafsi ni upi?

JIBU: Ukiangalia ndani vyama vya siasa, utabaini kwamba kuna changamoto nyingi ambazo wakati mwingine zinaweza kuwa ni kikwazo kwa baadhi ya watu wanaotaka uongozi.

Hivyo njia pekee ni kuruhusu utaratibu wa mgombea binafsi. Kwanza kabisa silengi chama bali ninazungumzia changamoto zilizomo ndani ya vyama vya siasa.

SWALI: Kuna changamoto gani kwenye vyama vya siasa?

JIBU: Kwenye baadhi ya vyama vya siasa kuna viongozi ni kama miungu watu hawataki kuguswa, hivyo wako tayari kumfanyia mtu mizengwe asiweze kugombea nafasi katika chama na pia kukiwakilisha chama dhidi ya vyama vingine.

Hivyo njia pekee ni kuwapo kwa mgombea binafsi, ili kama mwanachama atawekewa mizengwe katika chama chake, basi awe mgombea huru.

Hivyo ninaiomba serikali iangalie upya uwezekano wa kuwa na mgombea wa kujitegemea wasiofungamana na vyama.

SWALI: Kuna manufaa gani zaidi ya kuwa na mgombea huru kuliko kupitia vyama?

JIBU: Mifumo yote miwili ina umuhimu wake ila tatizo ni mizengwe ambayo imekuwa ikifanywa na baadhi ya viongozi wa vyama na kusababisha hata wagombea ambao wananchi wanawataka wanaachwa, kwa sababu tu wenye madaraka katika vyama hawawataki.

Hivyo mfumo wa mgombea huru au binafsi utaondoa changamoto hizo na unaweza kusaidia kupata viongozi wazuri. Ndiyo maana ninasema, wasinyimwe hiyo nafasi kwa sababu ya mfumo wa kupitia katika vyama. Nirudie kuishauri serikali iangalie uwezekano wa kuruhusu mgombea binafsi, kwani Tanzania inajengwa na watu wote hata wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa.

SWALI:

Unadhani kwamba utaratibu wa mgombea binafsi ukiruhusiwa nchini, wapo watu ambao wanaweza kuutumia?

JIBU: Watu wapo na ndiyo ambao wamekuwa wakilalamikia mchakato wa kupata wagombea katika vyama vyao. Kwa hiyo kama ambavyo Katiba anatambua haki ya mtu kuchagua au kuchaguliwa, ninaamini hata katika hili suala la mgombea binafsi ni haki, kwa sababu lengo ni kuchaguliwa.

Kama kupitia chama mgombea atawekewa mizengwe, basi awe mgombea huru kwa sababu ni haki yake ya kikatiba kuchaguliwa. Mtu akiwa mwanachama au hayupo katika chama, anayo haki inayotokana na uraia wake kupiga kura na ya kupigiwa kura.

SWALI: Suala la mgombea binafsi halikuanza leo, unadhani ni kwa nini halijafanyiwa kazi?

JIBU: Ni kweli halikuanza leo, ndiyo maana nilikuambia kuwa nililianza mwanzoni mwa mwaka 2000 nikiwa mbunge, lengo ni kupanua demokrasia yetu.

Ninaamini kwamba kinachokwamisha ni uamuzi tu, ndiyo maana ninaiomba serikali iangalie uwezekano wa kuruhusu mgombea binafsi. Ikumbukwe kuwa suala hili ni miongoni mwa mambo muhimu, kwani hata katika Rasimu ya Katiba Mpya ilizingatia jambo hili ingawa Bunge Maalum la Katiba halikuona umuhimu wake.

SWALI:

Kuna jambo ambalo mara nyingi huwa huliweki wazi, nalo ni kugombea ubunge. Je, utakuwa miongoni mwa wana CCM wanatakaochukua fomu kuwania nafasi hiyo?

JIBU: Mimi kugombea ubunge nasema hapana, kwa sababu, kwanza umri wangu, nawaachia vijana , halafu kazi nimefanya nyingi sana za utumishi, ni vyema kukaa nielekeza wenzangu, tushirikiane kuchagua na kuangalia ambao wanafaa tuwapigie debe. Tuwape maelekezo, kuliko mimi tena kwenda kugombea.

Nimeshakuwa Mwenyekiti wa Jumuiya wa Wazazi ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro, mbunge Moshi Vijijini. Nimeshafanya kazi kwenye Kurugenzi ya Makumbusho ya Taifa kwa miaka mitano, kwa kweli utumishi huu pia na umri wangu, napaswa kuheshimu umri wangu, naona nina mawazo mengi ya kushauri hao watakaoingia kwenye utawala kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu.

 

Habari Kubwa