Kuelekea uchaguzi mkuu Kenya 2022

25Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kuelekea uchaguzi mkuu Kenya 2022
  • *Uhuru amwambia Naibu Ruto ‘out’

BAADA ya Mahakama ya Rufani nchini Kenya kutupilia mbali mchakato wa mabadiliko ya katiba uliopendekezwa na BBI, ulioasisiwa na Rais Uhuru Kenyata na mwanasiasa wa upinzani Raila Odinga, Kenyata ameanza kumfukuza naibu wake.

Watetezi wa mkakati wa BBI, Rais Uhuru Kenyata (kulia) na Raila Odinga, wamepingwa na Mahakama ya Rufani kuhusu kubadili katiba ili kuweka mapendekezo ya mkakati huo. PICHA: MTANDAO.

Amemtaka Naibu William Ruto, aondoke serikalini badala ya kuendelea kuishambulia akiwa yuko ndani yake.

Uamuzi huo wa mahakama wa kukataa kubadili katiba ili kuingiza mapendekezo ya Kenyata na Raila ni furaha kwa Ruto, ambaye tangu mwanzo alikuwa akipinga BBI

Kwa mujibu wa BBC, uamuzi huo unaonekana ushindi kwa wanasiasa waliokuwa wanapinga mchakato huo, wakiongozwa na Naibu Rais Ruto ambaye ametangaza nia ya kugombea urais mwakani kwenye uchaguzi utakaofanyika Agosti 9, 2022, kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA).

BBC inasema iwapo hakutakuwa na rufaa nyingine kwenda  kwenye Mahakama ya Juu, ratiba ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Agosti 9 mwaka 2022 itabakia kama ilivyo kwa sababu hakutakuwa na kura ya uamuzi.

MCHAKATO WA BBI

Mchakato wa kutaka kuibadilisha katiba ya nchi hiyo iliyopatikana mwaka 2010, ulianza baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kumaliza uhasama wao kisiasa na kuungana ili kubadilisha mfumo wa uongozi nchini humo, kwa kuanzisha kile walichokiita ‘Building Bridges Initiative’ –BBI.

Siku tano baada ya kutolewa hukumu hiyo, Rais Uhuru anamtaka Naibu Ruto, aondoke serikalini badala ya kushambulia serikali ambayo yuko ndani yake.

Naibu amefurahishwa na uamuzi wa mahakama hiyo, kwa sababu tangu mwanzo, Ruto alivurugwa na BBI, mkakati wa Kenyata na Odinga wa kujenga Kenya mpya uliokuja na mapendekezo ya kubadilisha katiba ili kuunganisha kiungozi makabila ya nchi hiyo na kuleta umoja.

Ruto na washirika wake waliamini kuwa kumleta hasimu wao Odinga kwenye meza ya pamoja kupitia mkakati wa BBI ni mpango wa kugawana madaraka baina yake na Kenyata ambaye waliona atamuunga mkono Odinga kwenye kugombea urais na kumtosa Ruto wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

KUFUKUZWA SERIKALINI

Jumatatu wiki hii Kenyata amewasha moto jijini Nairobi, akiwaambia wahariri nchini humo kuwa amekasirishwa na ukosoaji uliotolewa dhidi ya utawala wake na kambi ya Ruto.

Rais huyo anasema hakuwa na ufahamu wowote kwa nini upande wa Naibu Ruto umechagua mashambulio dhidi ya utawala wake.

Anawaambia waandishi wa habari kwamba hana shida na Ruto kujenga ngome yake kisiasa lakini alihoji mbinu anazotumia akitumia chama kipya alichokiunda cha United Democratic Alliance (UDA).

"Sijui nini kimetokea isipokuwa ukweli ni kwamba anajaribu kujenga ngome yake ya kisiasa. Ninahisi ni bahati mbaya jinsi anavyofanya… ni vibaya," anasema.

Uhuru anaongeza kuwa anashangaa kwanini naibu wake alikuwa akipinga mchakato wa BBI akisema "masuala yaliyopelekea kuundwa kwa BBI ndiyo yaleyale yaliyowaleta pamoja".

"Ikiwa ninataka sasa kuboresha zaidi kuna tatizo gani? Tukirudi nyuma hadi mwaka wa 2013 imekuwa ajenda yangu ya kuleta watu pamoja," anasema.

"Ikiwa mgawanyiko wa 2007 ulituleta pamoja, kuna shida tukiwaleta watu wengine ndani?" anahoji
Rais huyo anasema hatua yake ya kuiunganisha nchi hiyo haimaanishi kupunguza nafasi za mtu yeyote kumrithi.

"Haikunyimi nafasi zako siyo Uhuru anayechagua, ni Wakenya wanaopiga kura."

Anawaambia wahiriri kuwa masuala kadhaa yaliyosababisha mgawanyiko unaotikisa utawala wake yanatokana na ari yake ya kuleta umoja.

HANA LA KUFANYA

Licha ya mchakato wa kurekebisha katiba unaotokana na BBI kuleta mgawanyiko kati ya Rais Kenyatta na Naibu Ruto ambao walishinda uchaguzi mara mbili wakigombea kwa tiketi moja ya Jubilee, Kenyatta hana la kufanya.

Kwa mujibu wa katiba Rais hawezi kumfukuza Naibu wake, hatua hiyo ndiyo inayosababisha amtake Ruto kuondoka serikalini.

Licha ya kuendelea na kampeni zake za urais mwakani, Ruto amekuwa akieleza mafanikio ya serikali ya Jubilee huku wakati mwingine akikosoa baadhi ya sera na uamuzi unaofanywa na serikali.

Miongoni mwa mambo hayo ni mchakato wa BBI na ushirikiano wa karibu wa Rais Kenyatta na viongozi wa upinzani hasa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Hata hivyo kambi ya Ruto au chama cha UDA hakijasema lolote kuhusu tamko hilo la Rais la kumtaka aondoke serikalini .

NITAONDOKA NIKITAKA

Kwa mujibu wa gazeti la the Standard la Kenya, mwanzoni mwa mwezi huu, Naibu Rais William Rutto, alitangaza kuwa ataondoka serikali kwa wakati atakapoamua.

Baada ya Ruto kuunda UDA, anawaambia washirika wake kuwa wamepata makazi mapya, wana vitu vyao ikiwamo bendera zao na kwamba makazi ya zamani ya Muungano wa Jubilee, yamebomoka.

“Sisi siyo wageni wa mambo haya. Tunachagua kujiunga na vyama kwa hiari yetu, kadhalika tunaamua kuondoka tukiona inafaa. Hakuna wa kutuuliza mbona bado tunaendelea kubaki si kazi yake,” anasema Ruto, anapoulizwa kwani haondoki anaendelea kuwa king’ang’azi kwenye serikali anayoamini kuwa imefeli kutimiza ahadi za uchaguzi.

Ruto anamtuhumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kushirikiana na kambi ya ODM ya Raila Odinga na kutembelea ajenda zao na sasa serikali yake imeshindwa na haina cha kujivunia.

HISTORIA YA MAFARAKANO

Pamoja na BBI, iliyoonekana kumtenga Ruto na kumkumbatia Odinga, tatizo lilikolea zaidi mwaka 2019 baada ya Uhuru na Kenyatta kuonekana kuwa hawaivi kufuatia hatua ya kukamatwa kwa Waziri wa Fedha Henry Rotich, kwa tuhuma za ufisadi.

Rotich, alijisalimisha kwa maofisa wa upelelezi Julai 2019 baada kutuhumiwa kulipa zaidi ya dola milioni 450 kugharamia ujenzi wa mabwawa mawili nchini humo kwa kampuni ya Italia.

Anatuhumiwa kukiuka mwongozo wa utoaji wa kandarasi iliyoopewa kampuni ya Italia CMC de Ravenna yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 450 kwa ujenzi wa mabwawa hayo, hatua ilimchukiza Ruto.

Rotich, ni mshirika mkubwa wa Ruto , eneo la Kaskazini la Rift Valley na aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha kwa mapendekezo ya Ruto kwa Kenyatta.

Mgawanyiko ndani ya Jubilee, ulikolezwa na kampeni ya Kenyata ya kupambana na ufisadi uliowatia kashkash Rotich na maofisa wenzake 20 wa hazina kwa madai ya upotevu wa bilioni 21 (Dola milioni 203) kwenye ujenzi wa mabwawa hewa ya Arror na Kimwarer.