Kuendekeza Kuendeke kunavyoweka rehani uhai wa wachimba dhahabu wadogo

12Mar 2020
Marco Maduhu
Geita
Nipashe
Kuendekeza Kuendeke kunavyoweka rehani uhai wa wachimba dhahabu wadogo
  • Wapo waelewaji, wengine hawajui
  • Baadhi wakiri wenzao wameshaumia
  • Wakutana na serikali, Ngo shida kuacha

UNAIJUA zebaki? Hiyo ni kemikali inayotumiwa na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwa ajili ya kukamatia dhahabu wakati wa kuichenjua ndani ya mchanga wenye madini hayo.

Shughuli ya uchimbaji madini Geita.

Matumizi yake ni kwamba, kemikali hiyo huwekwa kwenye karai lenye mchanga wa madini ya dhahabu, pamoja na maji kwa ajili ya kukorogwa kwa mikono, ili ziweze kukamata dhahabu na kuisugua vizuri.

Huo ni upande wa kwanza, lakini upande wa pili, kitaalamu inaelezwa ni hatari kiafya, endapo inapenya kwenye mwili wa binadamu.

Kimsingi, wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, wengi hawazingatii usalama wao wakati wa kuchenjua dhahabu, wakitumia kemikali ya zebaki, bila ya kuvaa vifaa kinga, kama vile kofia ngumu, nguo maalumu, viatu ya usalama na glovu, baadhi kwa makusudi na wengine kutojua.

Hatari inayotajwa inatokana na kutovaa vifaa hivyo vya kinga, ni endapo wakipatwa na mchubuko wakati wa kuisugua kemikali hiyo ya zebaki, kuna uwezekano mkubwa zebaki ikaingia mwilini na kuleta madhara ya kiafya.

MZIZI WA MADHARA

Simulizi ya madhara hayo, inaenda mbali katika tukio la mwaka 1956, sasa ikitimu miaka 64 huko nchini Japan, katika Mji wa Kumamoto, ambako wafanyakazi waliokuwa kazini katika Kiwanda cha Maji Taka, wanaelezwa kuathirika na kemikali hiyo ya zebaki, ambayo ugonjwa huo ulipewa jina la Minamata.

Wafanyakazi walioathirika wanaelezwa kupatwa na maradhi ya malaria kali, kifafa na kupoteza kumbukumbu haraka, ikaishia wengi kupoteza maisha ndani ya muda mfupi.

Lakini, kinachoendelea katika migodi midogo nchini, wachimbaji madini ya dhahabu, wanapenda kutumia zebaki kuwasaidia kupata dhahabu haraka, licha ya kuwa na uelewa wa madhara yake, wengi wana kawaida ya kupuuza.
Wanaelezwa hawajali kuvaa kinga, kutokana na matumizi ya kemikali hiyo na huchukua muda mrefu kuanza kuonyesha madhara kwa binadamu.

ZIARA MIGODINI

Nipashe ilipofanya ziara katika baadhi ya migodi midogo ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Nyakagwe, Nyarugusu na Msasa, mkoani Geita hivi karibumi kushuhudia uchenjuaji madini kwa matumizi ya kemikali ya zebaki, iliona namna utendaji hatari unavyotawala.

Iligundulika, vijana wengi wakiwa hawana vifaa vya kinga wakati wa kusugua zebaki iliyochanganyika na mchanga wa madini ya dhahabu, mikono yao ikiwa mitupu, hawajavaa viatu, pasipo kujali usalama wa afya zao.

Boniphace Charles, ni mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Mtalingi, uliopo Nyakagwe Geita, anayekiri kutambua zebaki ina madhara ya kiafya na kubainisha wameshazoea kuchenjua dhahabu bila ya kuvaa vifaa kinga.

Anasema wachimbaji wadogo wengi wa dhahabu, hawana elimu ya kutosha kuhusu madhara ya zebaki, zaidi ya kusikia tu ina madhara kiafya na wamekuwa hawavai vifaa kinga, kwa sababu wameshazoea kuchenjua dhahabu kwa mikono mitupu, bila viatu miguuni.

“Madhara haya ya matumizi ya zebaki tunayajua kwa kusikia tu, lakini hatujawahi kumshuhudia mchimbaji ameathirika na zebaki. Utasikia tu fulani sasa hivi anaumwa kweli na wengine kufa, lakini kuwaona kwa macho bado ndio maana tunaendelea kuitumia zebaki bila ya hofu kuwa hatuwezi kuugua.

“Ukiangalia hapa, karibu wachimbaji wote wadogo hatujavaa vifaa kinga, kwa sababu tumeshazoea kufanya kazi tukiwa tupu na hatuoni madhara yoyote ya zebaki,” anaeleza mchimbaji huyo.

Shida Lupanga ni mchimbaji mdogo wa dhahabu, katika mgodi wa Msasa, wilayani Chato, mwenye ushauri kwamba kinachopaswa kwa wachimbaji wadogo, ni kujikinga na madhara ya matumizi ya zebaki kwa kutolewa elimu ya kuvaa vifaa kinga, ili wabaki salama.

Anasema, wachimbaji wengi kwenye migodi midogo, wanatoka sehemu mbalimbali kufuata riziki mahali hapo penye uchimbaji na hawajui madhara ya zebaki, wanaishia kufanya kazi kwa mazoea, baada ya kuwakuta wenzao wanachenjua dhahabu bila ya kinga.
Lupanga ana ufafanzi: “Kitu kikubwa tunachokiomba ni utolewaji elimu juu ya madhara haya ya matumizi ya zebaki,”

Joseph Shindika, ni mchimba madini mdogo katika mgodi wa Nsangano, anasema hivi sasa wamebadilika, baada ya kupewa elimu ya afya dhidi ya zebaki na sasa wanavaa vifaa kinga.

Anasema mgodini, hivi sasa kuna taasisi inayojishughulisha na uwezeshaji wachimbaji wadogo, walifika kwenye mgodi huo na kutoa elimu juu ya madhara ya zebaki, hasa wanakochenjua dhahabu bila ya kuvaa vifaa kinga, ndipo wakaona umuhimu wa kuvaa vifaa hivyo ili wawe salama.

MMILIKI MGODI

Mmilikiwa wa mgodi mdogo wa madini ya dhahabu, Mtalingi, uliopo Nyakagwe, Mtalingi Hamzeh, anakiri kutambua madhara ya matumizi ya zebaki katika kuchenjua madini ya dhahabu, lakini wanashindwa kuepuka, kutokana mbadala una gharama kubwa zaidi.

Anasema, kutokana na kutambua madhara hayo ya zebaki wamekuwa wakitoa elimu kwa wafanyakazi wao, wanawagawia vifaa kinga na wanapochenjua dhahabu, lakini baadhi yao hawavai wamekuwa wakikaidi kwa kuendelea na mazoea ya siku zilizopita.

“Umaskini nao unachangia wachimbaji wadogo kuitumia zebaki katika shughuli zetu za uchenjuaji madini ya dhahabu. Hatuwezi kumudu gharama za teknolojia nyingine za kukamatia dhahabu ambazo ni salama.

“Ili tupate kuwa salama tunaziomba taasisi za kifedha zitukopeshe wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, tumudu gharama za kutumia teknolojia nyingine ya kuchenjua dhahabu na kuondokana na matumizi ya zebaki ambayo ni hatari kwa afya zetu,” anaongeza.

Ibrahim Makala, Meneja wa Mgodi wa Nsangano Gold uliopo Nyarugusu, anasema kwa sasa wapo kwenye hatua ya kuacha matumizi ya zebaki kuchenjua dhahabu, na wanatumia njia mbadala anayoiita ‘gold culture’ ambayo wako katika majaribio.

Anasema, baada ya kupewa elimu ya madhara ya matumizi ya zebaki, kwa sasa wanawajali sana wafanyakazi wao na wamekuwa wakiwapatia vifaa kinga, pamoja na kufuatilia matumizi yake, ili kuepukana madhara ya zebaki.

“Sasa tupo kwenye hatua ya kuachana kabisa na matumizi haya ya zebaki kuchenjulia dhahabu. Tupo kwenye hatua ya kutumia ‘gold culture’… tupo kwenye hatua ya majaribio, japokuwa mashine hizi nazo zina gharama kubwa takribani Sh. milioni 10 na ukiangalia sisi wachimbaji wadogo mtaji wetu ni mdogo,” anasema.

WADAU WAELIMISHAJI

Theonestina Mwasha, Mkurugenzi wa taasisi ya kiraia FADeV inayojishughulisha na kuendeleza wachimbaji wadogo nchini, ikiwamo kuwapatia elimu, namna ya kujikinga na madhara ya matumizi ya zebaki, vifaa kinga wakati wa kuchenjua dhahabu au kutumia njia salama ya kisasa ya ‘gold culture.’

Anasema, walifanya utafiti kwenye baadhi ya migodi midogo ya madini na waligundua wachimbaji kukosa elimu kabisa, kuhusu madhara yanayowakabili, ikiwamo uchenjuaji kwa zebaki na bila ya kutumia kinga, kwa athari ya miili yao.

“Mchimbaji anavyochenjua dhahabu, mikono yake ikiwa tupu, ambapo akipatwa na mchubuko na zebaki ikiingia ndani ya mwilini wake, tayari inaanza kumletea madhara ya kiafya taratibu, ikiwamo kichwa kuuma, kupoteza kumbukumbu, kutosikia, kuathiri figo na hatimaye kupoteza maisha,” anasema.

Mwasha anasema, kwa sasa wanajikita kutoa elimu hiyo ya madhara ya matumizi ya zebaki kwenye migodi midogo iliyopo mkoani Geita, ili wanaoelimishwa wabadilike na kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao wajikinge, ili kuondoa athari ndani ya jamii na hata vizazi vyao.

SERIKALI MKOA

Katibu Tawala Msaidizi, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Hermani Matemu, anasema sekta ya madini ni muhimu na serikali imeboresha Sheria ya Madini, ili wachimbaji wanufaike na rasilimali zao, wainuke kiuchumi bila ya kuathiri afya zao.

Anasema taasisi hiyo ya Fadev imejitokeza katika wakati muafaka wa utoaji elimu dhidi ya madhara ya zebaki, hasa kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu na wamekuwa wakiitumia kwa kiwango kikubwa bila ya kujua madhara yake.

Matemu anaahidi, serikali itashirikiana na shirika kutoa elimu inayohusu madhara ya zebaki.

Ofisa Madini wa Mkoa Geita, Daniel Mapunda, anasema serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali, imeshatoa elimu kwa wachimbaji wadogo juu ya madhara ya matumizi ya zebaki, kupitia kwenye mikutano na warsha na imeshauri utumiaji vifaa kinga kuchenjua madini hayo, ili wawe salama.

Anasema, hadi sasa serikali imeshaingia mkataba wa kimataifa kufuta matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo na kuhamia mbadala wa kuchenjua dhahabu, lakini ni njia zenye gharama kubwa na wachimbaji wadogo hawazimudu, hivyo kinachofanyika ni kuwabadilisha taratibu.

Mapunda anafafanua: “Tukisema leo tuzuie kabisa matumizi ya zebaki, nadhani tutaathiri sekta ya uchimbaji kwa sababu zebaki ina gharama ndogo na rahisi kupatikana na ina uharaka wa kukamata madini kuliko njia zingine.”

“Unakuta mchimbaji ana mifuko miwili ya mawe ya dhahabu, ukimwambia atumie teknolojia ya kemikali ya (cynide) ambayo ni nzuri zaidi kwa ukamataji wa dhahabu, hawezi kuimudu sababu ya gharama, hivyo tuendelee kutumia zebaki ambayo ina gharama ndogo, licha ya kujua ina madhara kiafya,” anafafanua.

Pia, anasisitiza azma ya serikali kuendelea na utoa elimu kwa wachimbaji wadogo, kuhusu madhara yaliyoko kutoka kwenye zebaki, pamoja na kuwa na mpango wa kuwarasimisha, ili waone namna ya kuwasaidia kutumia teknolojia mbadala katika kuikamata dhahabu, na siyo hatari ya zebaki kwa afya zao.

Habari Kubwa