Kujenga viwanda na Runali, vitachakata mbaazi, ufuta

09Nov 2019
Sabato Kasika
Lindi
Nipashe
Kujenga viwanda na Runali, vitachakata mbaazi, ufuta

SEPTEMBA mwaka huu Shirikisho la Vyama vya Ushirika la China (ACFSMC), lilivialika vyama vya ushirika kutoka Tanzania, Zimbabwe, Msumbuji, Congo na Kenya.

Mwenyekiti wa Runali, Hassan Mpako (kulia), akizungumza kwenye moja ya mikutano ya chama hicho.

Lengo la mwaliko huo lilikuwa ni kujadili shughuli mbalimbali za ushirika na jinsi ya kusaidia kuhakikisha njia hiyo muhimu ya kufikia maendeleo inaimarika ili kukuza uchumi kwa wanachama na nchi zao.

Kwa upande wa Tanzania, Chama Kikuu cha Ushirika kinachoundwa na wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale mkoani Lindi (Runali) kilipata mwaliko huo na kuwakilishwa na mwenyekiti wake Hassan Mpako.

Muda mfupi baada ya kurejea Mpako anazungumza na Nipashe kueleza kile kilichojiri kwenye mkutano huo akitaja baadhi ya mambo kuwa ni pamoja na uwekezaji wa pamoja kwenye kuongezea mazao thamani.

KUJENGA VIWANDA

Pamoja na mikakati mbalimbali waliyojadili, Mpako anaiambia Nipashe kuwa Runali ililiomba shirikisho liangalie uwezekano wa kujenga kiwanda cha kuongezea thamani mbaazi na ufuta ili kuziongezea thamani kabla ya kusafirishwa kwenda kuuzwa nje ya nchi.

Anasema, katika ziara hiyo alifanya mazungumzo na uongozi wa ACFSMC na kujikita zaidi kwenye nyanja za masoko na viwanda, hatimaye wakafikia makubaliano hayo ya ujumbe wa shirikisho hilo kwenda mkoani Lindi.

ACFSMC KUJA NCHINI

"Katika mazungumzo yetu tulikubaliana kuwa ujumbe wa ACFSMC utakuja nchini mwezi huu kufuatilia makubaliano hayo ili hatimaye mtambo huo uletwe kwa ajili ya kuchakata mazao hayo," anasema Mpako.

Kwa mujibu wa Mpako shirikisho hilo lilikubali kuangalia ushirikiano kati ya uwekezaji wake na Runali kwenye uchakataji wa mazao hayo ili kuyapatia masoko ya uhakika duniani.

Anasema shirikisho hilo liliahidi kuagalia kile ambacho Runali inakifanya, ili hatimaye wafikie makubaliano ya kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao yanayokusanywa na chama hicho kabla hayajauzwa.

"Wenzetu China wako juu sana kimaendeleo katika masuala ya viwanda na masoko. Tulizungumza nao na kuwaeleza mahitaji yetu, hasa kwenye masoko ili kuondokana na kuuza malighafi," anasema.

MATARAJIO YA CHAMA

Mwenyekiti wa Runali anasema, uimara wa shirikisho hilo utasaidia kuimarisha Runali, ambayo katika bajeti yake ina mpango wa kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya wanachama wake kabla ya kuyapeleka katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

"Runali tuna mpango wa kujenga kiwanda cha kubangua korosho kule Liwale na kingine cha kuchakata mbaazi, hivyo tunaamini malengo yetu yanaweza kutimia iwapo ujumbe huo shirikisho hilo utakapokuja nchini," anasema.

Anasema, hadi nusu ya mwaka huu wa 2019, mauzo ya shirikisho hilo yamefikia dola 319.6, yakiwa yamepanda kwa asilimia 6.6 na kutengeneza faida ya asilimia 3.1 katika viwanda vya bidhaa za kilimo.

Mpako anasema, shirikisho hilo linawakilisha vyama vya ushirika vya China, ambavyo ni chachu kubwa ya mabadiliko ya uchumi kwa familia hasa zinazoishi vijijini, hivyo hata Runali inataka kupata uzoefu huo.

Anasema, shirikisho hilo lina mchango mkubwa katika kuhakikisha kilimo kinafanyika kwa tija, ujenzi wa viwanda vya mazao yatokanayo na kilimo na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwamba kwa uzoefu wake, Runali inaweza kufanikiwa kuwa na viwanda vya kuchakata mazao hayo na kupata mapato kutoka kwa wanachama wake na kuwa katika nafasi ya kuisaidia serikali kuwa na viwanda.

ACFSMC wanataka kuhakikisha Runali inakuwa na uwezo wa kusafirisha korosho kwenda kwenye masoko ya kimataifa zikiwa zimechakatwa, hivyo anaamini hayo yakifanyika, chama hicho kitaimarika zaidi.

HISTORIA NA MALENGO

Akizungumzia historia Mpako anasema, chama hicho kilianzishwa mwaka 2013 kikiwa na wanachama 52 baada ya kujiengua kutoka katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Lindi (Ilulu).

"Wanachama wanaounda Runali ni vyama vya ushirika vya msingi kutoka wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale, na hadi sasa wapo zaidi ya 100 na wanaendelea kuongezeka," anasema.

Mwenyekiti huyo anasema, tangu chama hicho kianzishwe kimepata mafanikio, ikiwamo kuanzisha miradi ikiwamo ujenzi wa ofisi ya chama iliopo mjini Nachingwea, ghala la kuhifadhia magunia na pemebejeo.

"Runali pia inaendelea kujenga vituo vya maandalizi ya malipo ya wakulima wilayani Nachingwea, ambavyo vitagharimu Sh. milioni 280, huku ujenzi wa ghala kuu mjini Ruangwa nao ukiendelea," anasema.

Aidha, anataja mikakati zaidi ya chama hicho kuwa ni kununua eneo la eka 500 kwa ajili ya shambadarasa la mikorosho ili wanachama wa Runali waweze kujifunza kilimo bora cha korosho, hatimaye wanufaike nacho.

Mpako anaongeza kusema kuwa, chama hicho kina mpango wa kuhamasisha kilimo cha alizeti, ili kiwe na umaarufu mkoani Lindi kama ilivyo kwenye baadhi ya mikoa hapa nchini.

"Unajua huku kwetu, wakulima wanategemea korosho, ufuta na mbaazi kama mazao makuu ya biashara, lakini sasa tunaongeza alizeti, kwani ni zao ambalo halitegemei soko la nje," anasema.

Akizungumzia mkakati wa kuhamasisha kilimo cha alizeti, Mpako anasema, Runali ikiwa na mapato ya ziada, itanunua mbegu za zao hilo na kuzigawa katika shule za msingi, sekondari na kwenye ofisi za serikali za vijiji.

Mbegu hizo zitagawiwa, ili kuanzisha mashamba darasa, ambayo yatasaidia wakulima wetu kujua namna ya kulima zao hilo na kupata mavuno mengi na kuifanya Lindi kuwa juu kwa kilimo cha alizeti," anasema.

Habari Kubwa