Kukata tamaa kunavyodhuru wengi wakati wa kutibu ugonjwa saratani

17Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kukata tamaa kunavyodhuru wengi wakati wa kutibu ugonjwa saratani

NIKIWA mwenye umri wa miaka 29 nilipimwa hospitalini nikabainika kuwa ninaugua saratani ya mlango wa kizazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Shujaa Cancer Foundation, Gloria Kida, alipozungumza kwenye sherehe za Siku ya Mashujaa wa Saratani, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja Bidhaa wa Benki ya KCB na wa kwanza kulia, Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Mark Mseti na Sheikh Yakubu Bakari. PICHA ZOTE: MPIGAPICHA WETU

Ni taarifa zilizonishtua kuliko matukio yote yaliyowahi kunipata maishani mwangu. Hata ndugu na jamaa walipopokea kwa tafsiri kwamba siku zangu za kufa zimekaribia.

Kwa sababu hiyo, maelekezo na ushauri ulikuwa mwingi, miongoni wakiniasa nisithubutu kupata matibabu hospitalini, kwa madai hiyo itakuwa ni tiketi ya kuniua mapema.

Baadhi walinishauri nikapate matibabu kwa waganga wa kienyeji, wengine wakataka nikaombewe kanisani wengine kwa sheikh, wengine niendelee na ushauri hospitalini na baadhi kushauri nifanye hayo yote kwa pamoja.

Ni maelezo ya Amina Moleli, mkazi wa Arusha akisimulia yaliyomkuta mara baada ya kuchunguzwa na kudhihirishiwa na wataalamu wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), kuwa ana saratani ya mlango wa kizazi mwaka 2013.

Anaelezea ni mazingira ambayo yalimfanya achanganyikiwe na kuona ndio mwisho wa maisha yake na hata kuona kuwa ndoto mbalimbali za kimaisha alizokuwa amejiwekea hazina tena maana.

Mama huyo akiwa kwenye wimbi hilo la mawazo, akakumbuka daktari aliyemthibitishia kuwa ana saratani alimshauri awe mtulivu, azingatie tiba na awe na imani kwa uwezo wa Mungu, atapona na kurejea tena kwenye maisha yake ya kawaida.

Hata hivyo, alikata shauri kwamba afuate ushauri wa daktari wake licha ya vitisho wagonjwa wengi wa saratani waliofuata taratibu za kihospitali walipoteza maisha.

“Nakumbuka niligundulika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi mwaka 2013 na nikaanza matibabu (ORCI) Agosti 11, 2014 na nashukuru sasa nimepona kabisa,” Amina anatamka, akiwa na ufafanuzi zaidi kuwa:

“Kwa kweli matibabu ya saratani ni makali sana, yanaandamana na maumivu na changamoto nyingi sana kiasi kwamba, kama hauko imara, unaweza kukata tamaa. Nashukuru madaktari na wauguzi walinipa moyo.”

Anasimulia katika kipindi cha matibabu, alipata fursa ya kubadilishana mawazo na wagonjwa wa muda mrefu zaidi ya miaka mitano, wakamshauri asishawishike kupata tiba za asili kwa sababu miongoni mwao waliofanya hivyo tayari wameshapoteza maisha.

“Wakati nikipata tiba nilimtumainia Mungu na kumuomba anisaidie tiba nilizokuwa napata zinisaidie. Nashukuru hivi sasa nimepona kabisa,” anasimulia Amina.

“Kwa sasa naishi vizuri na mwenza wangu wa ndoa na nafanya kazi zangu vizuri na sina wasiwasi na ndoto zangu za kijasiriamali zinaenda vizuri,” anaeleza.

BINGWA OCEAN ROAD

Namna ilivyo kuhusu tiba za saratani, Mkurugenzi wa Tiba ORCI, Dk. Mark Mseti, anasema huwa wanawahamasisha wagonjwa wao kuwa na moyo wa uvumilivu na kufuata kile wanachowaelekeza iwapo kweli wameazimia kupona.

Anasema wanawaweka wazi wagonjwa kuwa wakati mwingine matibabu huchukua muda mrefu na kuna wakati wanafanya mabadiliko ya aina ya tiba au yanachanganywa kwa pamoja.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Mseti anasema maumivu na tiba za muda mrefu, huweza kumfanya mgonjwa anakata tamaa.

“Mgonjwa anayetibiwa saratani akiruhusu tu kukata tamaa inakuwa rahisi kupoteza maisha. Ukishinda kwenye hii vita wewe ni shujaa,” Dk. Mseti anatoa agalizo la kisaikolojia.

Anasema matibabu ya saratani ni vita vya muda mrefu, inayobeba mapigano mengi na walioshinda kwenye vita hiyo, wanapaswa kushangilia na kujiita mashujaa.

Dk. Mseti anasema, saratani ni ugonjwa unaojumuisha magonjwa mengi ambayo yanafanana kwa kuwa na  chembe hai za mwili zinazozaliana kwa haraka bila ya udhibiti na zinasafiri mwili na kwenda kuzaliana katika eneo jingine.

Anafafanua kuwa chembe hai hizo za kawaida za mwili, haziwezi kuhamishiwa kwenye kiungo kingine tofauti na cha awali na kuendelea kuzaliana kama zilivyo za saratani.

“Mfano ukichukua seli za ulimi ukiziweka kwenye mkono haziwezi kuendelea kuishi. Lakini, seli ya saratani popote utakapoziweka mwilini zitaendelea kuishi na kuzaliana,” anafafanua upekee wa maradhi hayo.

Kuhusu visababishi vya saratani, Dk. Mseti anasema vipo vya aina nyingi na miongoni ni kemikali, mionzi, urithi wa vinasaba na mtindo wa maisha kwa maana uwiano wa vyakula anavyokula na suala zima mwili unavyojishughulisha.

INAVYOKUJA NA KUKABILIWA

Kula kwa wingi vyakula vyenye sukari, wanga, mafuta, protini na kutofanya mazoezi, anaelezea ni moja ya chanzo cha kunenepa na kuwa na uzito kupita kiasi hivyo kuwa rahisi kupata magonjwa yasiyoambukiza mfano saratani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Shujaa Cancer Foundation (SCF), Gloria Kida, anasema kuanzia mwaka huu kila Jumapili ya kwanza ya Juni Tanzania itakuwa inaadhimisha Siku ya Mashujaa wa Saratani.

Dhumuni la kuadhimisha siku ya mashujaa, ambayo imekuwa ikiadhimishwa na mataifa mengi duniani kwa miaka mingi, ni kuwatambua watu waliopo kwenye tiba na hata waliopona.

“SCF inamtambua shujaa wa saratani kuwa ni yule ambaye amepata matibabu na amepona au aliyemaliza matibabu ya awali na anaendelea na hatua nyingine,” anasema Gloria.

Hii ni kwa sababu wanajua kwamba tiba wanazopitia siyo nyepesi na zinaandamana na kupata maumivu makali na shida mbalimbali.
 
Anasema hata baada ya tiba kuna athari ambazo huwa zinajitokeza na kuzidi kumweka mgonjwa katika wakati mgumu.

“Ni siku ya kufurahia maisha wakati na baada ya tiba kama ilivyo kwa watu wanaofanya sherehe ya kukaribisha ndugu jamaa na marafiki katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa au kukamilisha jambo muhimu katika maisha,” anasema.
 
Anailezea SCF kuwa ni asasi ambayo lengo lake kuu ni kuwahudumia mashujaa wa saratani ya via vya uzazi, yaani ya matiti, tezi dume na mlango wa kizazi mara wanapomaliza tiba ya awali.
 
SCF analenga katika kuainisha changamoto wanazopitia mashujaa wa saratani ya via vya uzazi na kuratibu njia mbalimbali za kuwasaidia namna ya kukabiliana na vikwazo hivyo.
 
Anasema uzoefu wa SCF unaonyesha kwamba wagonjwa wa saratani wanahitaji kupewa ushauri nasaha wakati wote wa tiba na hata baada ya kupona kabisa.
 

Habari Kubwa