Kumekucha Nachingwea mnada wa ufuta

06Jul 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Kumekucha Nachingwea mnada wa ufuta
  • *DC awaonya wakulima, wasigomee bei, tani  milioni 1.8 zanunuliwa

MSIMU wa ufuta umeanza katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Lindi, huku tani 1,884,000 za zao hilo zikinunuliwa kwenye mnada uliofanyika hivi karibuni katika kijiji cha Mbondo, wilayani Nachingwea.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango

Kampuni tatu kati ya tisa ambazo ziliomba kununua ufuta katika wilaya za Ruangwa, Nachingwe na Liwale mkoani Lindi kwa njia ya mnada zinatarajiwa kuwa zitanunua jumla ya kilo milioni 1.8.

Katika mnada huo unaosimamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Runali, bei ya juu ya ufuta ilikuwa Sh. 2,860 huku bei ya chini ikiwa ni Sh. 2,852 kwa kila kilo moja.

Mnada huo ni wa kwanza kufanyika mwaka huu kupitia chama cha Runali, ambacho kinaundwa na vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) kutoka wilaya za Ruangwa, Nachingwe na Liwale.

Wakati mnada huo ukiendelea Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango anatoa neno kwa wakulima ambalo linaweza kuwasaidia kunufai na zao hilo.

USHAURI WA DC

Akizindua mnada huo katika kijiji cha Mbondo, wilayani Nachingwea, Rukia Muwango, anawatahadharisha wakulima wa ufuta kutogomea bei hali, ambayo inaweza kusababisha wakwame hapo baadaye.

Kabla ya kuendelea kuwaonya anawashukuru kwa kukubali kuuza ufuta wao kwa bei hizo, na kisha anawatahadharisha kuhusu madhara ambayo yanaweza kuwapata wanapogomea kuuza mazao yao.

''Mwaka jana kulifanyika mgomo ambao wakulima wengine walifuata mkumbo bila kuamua wenyewe. Matokeo yake yalikuwa kama mtego wa panya wakajikuta wakinasa wenyewe,'' anasema Muwango.

Anafafanua kwamba madhara ya mgomo huo ni kuathiri vyama vya msingi, vyama vikuu vya ushirika, serikali kuu, halmashauri na baadhi ya wakulima, kwa vile wanakosa wanunuzi wa mazao yao.

"Hivyo kabla ya kushiriki mgomo ni vyema wakulima muanze kufikiria madhara yanayoweza kusababishwa na hatua hiyo ya kugomea bei na kisha mchukue hatua za kuachana nao," anasema.

Anasema serikali mkoani Lindi imekuwa ikitangaza bei elekezi ya ufuta ambayo kimsingi inatakiwa kusimamiwa kwa kuzingatia kwamba inalenga kunufaisha wakulima kulingana na hali halisi ya soko.

Anasema serikali iliamua kuuza ufuta kwa mfumo wa mnada, lakini zikatokea changamoto za baadhi ya wakulima kugomea bei, hali ambayo ameikemea na kutaka isijitokeze katika msimu huu.

"Hatua ya baadhi ya wakulima kugomea bei ilikuwa ni kama mtego wa panya kwani hata wenyewe walijikuta wakikwama, hivyo sitarajii kuona hayo yakijirudia msimu huu," anasema.

KILIMO CHA UFUTA

Ufuta ni moja ya mazao ya biashara yanayolimwa kwenye mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara an kuwaingizia kipato wakulima wa mikoa hiyo, huku zao kuu likiwa ni korosho.

Hata hivyo, kama ilivyo kwenye korosho, baadhi ya wakulima wamekuwa wakiuza ufuta kwa mitindo wa 'kangoma au chomachoma', ambayo imepigwa marufuku na serikali.

Serikali inapiga marufuku mitindo hiyo, kwasababu inawanyonya wakulima bila wao kujijua na kutajirisha wajanja wachache wanapoenda kujinufaisha kwa jasho la wengine.

Pamoja na juhudi hizo za kuzuia kangoma na chomachoma, bado wapo wakulima wachache ambao hawajaona umuhimu wa kuuza mazao yao kwenye minada huku wakisimamiwa na vyama vya ushirika.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha viongozi wa vyama vya ushirika kuitisha mikutano ya mara kwa mara kwa ajili kuwakumbusha kujiunga na ushirika ili kuepuka kuuza mazao yao kwa bei ya hasara.

  USHAURI WA RUNALI

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Runali, Hassan Mpako, anasema viongozi wa vyama vyote vinavyounda Runali walishapewa maelekezo kwa ajili ya kuwakumbusha wakulima jinsi ya kuuza mazao yao.

"Wanapouza kwenye mnada unaosimamiwa na Runali hawawezi kuibiwa kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa baadhi yao, ambao hawazingatii maelekezo ya kutoka kwa viongozi wao," anasema Mpako.

Anasema, katika msafara wa mamba, hata kenge nao hawakosekani, hivyo anaamini kwenye vyama vya ushirika vya msingi, bado kuna wakulima ambao wanakwenda kinyume na utaratibu wa mnada.

Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa katika mnada uliofanyika kwenye vijiji mbalimbali vya wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale, msimu wa mwaka jana, ufuta uliuzwa kati ya Sh. 2,940 hadi Sh. 2,935.

Katika msimu huo kampuni nyingi zilijitokeza na kushinda kununua zao hilo kupitia chama cha Runali huku baadhi zikifanikiwa kushinda tenda hiyo ya ununuzi wa zao la ufuta.

FAIDA KIAFYA

Wataalam wa afya wanasema kuwa mafuta yana virutubisho muhimu na yamekuwa yakitumika tangu miaka 5,000 iliyopita na kwamba yana maajabu kiafya na pia matumizi ya mafuta hayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.

Matumizi ya mafuta ya ufuta yamekuwa yakiongezeka kwa kasi na Kwamba umaarufu wake unaongezeka kwa kuwa wengi wanaamini ni dawa kutokana na unafuu utokanao na maradhi mbalimbali, kwamba kuna ukweli uliothibitika kuwa, mafuta ya ufuta yanasaidia matatizo ya ngozi, meno,  mifupa pamoja na kuwa na manufaa mengine mengi.

Aidha, wanataja vilivyomo katika mafuta ya ufuta kuwa ni madini ya manganese, shaba, calshamu, chuma,    Zinc, thiamine, vitamin B6 , phosphorus, magnesium na protin.

 

Habari Kubwa