Kumesheheni raha kitalii, yanayostaajabisha duniani

21Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kumesheheni raha kitalii, yanayostaajabisha duniani
  • Ghorofa refu ulimwenguni
  • Maajabu; binadamu, miujiza
  • Ikulu ruksa; ona bahari bandia
  • Hakuna trafiki, wala foleni njiani

DUBAI ni sehemu ambayo nafsi za dunia nzima zinakutanishwa. Sababu hiyo ikitokana na namna nchi hiyo ilivyosheheni mkusanyiko wa watu wa mataifa mbalimbali idadi kubwa ikiwa ni wafanyabiashara.

Watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani, wakiwa kwenye jangwa mashuhuri kwa utalii, Dubai. picha: mpiga picha wetu

Ni nchi ndogo iliyoko katikati mwa Mashariki ya Kati, yenye idadi ya watu wasiozidi milioni 3.5, iliyosheheni vivutio kemkemu vya utalii, yenye ustaarabu wa hali ya juu kutokana uhalifu kwao ni ‘bidhaa adimu.’

Safari yangu ilianza saa 10: 30 kuelekea Dubai International Airport ambako ni umbali wa maili 2,750 kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Ni mwendo wa saa tano kuwasili Dubai, kwa ndege hiyo kubwa yenye uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 450. Saa nne usiku tayari ilishafika.

MSHANGAO UNAANZA

Moja ya vilivyonishangaza ni uwanja ni mkubwa sana na idadi ya wageni wanaowasili uwanjani nayo kubwa sana. Uwanja umejaa ndege nyingi zinazoruka na kutua kwa wakati mmoja na inawachukua abiria wastani wa dakika 10 kutoka kwenye ndege hadi eneo la kutoka uwanjani.

Hapo nyenzo inayowasaidia ni kuwepo magari maalum ya kusafirisha abiria kutoka kwenye ndege, kuwapeleka sehemu ya kutokea.

Kivutio kingine, uwanjani ni licha ya kupambwa na ndege za mashirika mengine makubwa kama Fly Dubai, ndege kubwa za Shirika la Ndege la Emirates, ambalo ndilo nilisafiri nalo na linakadiriwa kuiwa ndege kufika 275, ndio kivutio kikuu; zimo ndege aina ya Boeing 165 na Airbus 110.

NILIPOINGIA JIJINI

Lingine la kuvutia Dubai, ni namna jiji lilivyopambwa kwa barabara za juu karibu kila eneo, kiasi kwamba siyo rahisi kukuta foleni hata dakika moja katika maeneo yote yake.

Barabara zimejengwa kwa ustadi mkubwa, makutano yote yamejengwa katika barabara za juu, zinayawezesha magari sita ya upande mmoja kwenda na mengine sita yanayorudi kupita kwa kasi, hata kumaliza foleni na kuifanya Dubai kuwa ya kipekee.

Ni eneo linalotengeneza mvuto kwa kutazama namna magari ya kila upande yanavyopishana kwa kasi, bila ya kusababisha msongamano.

Miundombinu yake na hasa barabara na daraja, Dubai imejitahidi kuweka barabara za juu kila sehemu waliyoona inaweza kuzaa msongamano, kiasi kwamba unaweza kutoka uwanja wa ndege hadi hotelini kwako bila kusimama hata sekunde.

Jambo lingine la kushangaza Dubai, ni kwamba huwezi kuona gari kuukuu, mengi ni mapya na ya kifahari na nilipotaka kufahamu sababu, mwenyeji wangu aliniambia uchumi umestawi na serikali haiwatozi kodi kubwa wananchi wanapoyaagiza.

“Hapa huwezi kuona gari kuukuu na hutaliona mpaka unaondoka, kwa sababu gari likikaa mwaka au miaka miwili mtu anaweza kuagiza lingine kwa sababu ya unafuu wa kodi,” anasema.

HAKUNA TRAFIKI

Kivutio kingine cha kufurahisha, ni kwamba si rahisi kukuta askari wa usalama barabarani anayeongoza magari au askari wa kawaida akiranda mtaani, ilivyo kawaida kwenye miji mingine mikubwa duniani.

Mwongoza watalii niliyeambatana naye, aliniambia kuwa zimewekwa kamera kila umbali wa kilomita moja barabarani, hivyo madereva wanajiongoza kwa kuwa adhabu ya kuzidisha mwendo ni kubwa.

Anasema, licha ya kutoonekana askari katika mji huo kiwango cha uhalifu kiko chini sana na iwapo mtu atafanya uhalifu askari huwasili haraka kwenye eneo la tukio kufanya kazi yao kudhibiti chochote cha kiusalama.

“Ukizidisha mwendo uliowekwa adhabu ni Dola za Marekani 150 (Sh. 330,000) sasa watu wanajisimamia wenyewe hakuna anayependa kutoa kiasi hicho cha pesa hapa sheria inafanyakazi sawasawa watu wanaogopa kufanya makosa,” anasema.

Katika raha hiyo ya siku saba za utalii Dubai, sikumwona askari awe wa usalama barabarani au wa kawaida, mwanajeshi, hata mgambo. Ustaarabu umetamalaki.

Nilipomdadisi mwenyeji wangu kulikoni hali hiyo hakuna askari, aliniambia wapo, lakini wanafanya kazi zaidi za kuendeshea ofisini, kwani barabarani kila mtu anajisimamia na maeneo yote ya mji yana kamera, hivyo si rahisi kufanyika uhalifu.

Ingawa siku zote hizo nilikuwa nazungushwa kila kona ya nchi, bado nilikuwa makini kutaka kujiridhisha kama kweli hakuna askari barabarani na sikufanikiwa mpaka nilipopanda ndege, kurejea jijini Dar es Salaam.

ILIVYO DUBAI

Dubai sehemu ya muunganiko wa mataifa saba yanayounda United Arab Emirates (UAE), ambazo ni Dubai, Abudhabi, Shalja, Agman, UmAlqudium, Fujiarah na Ras Al Khaima, ambayo yanazungumza Kiarabu.

Mji mkuu wa mataifa haya ni Abudhabi, ambao unaelezwa kuwa na akiba kubwa ya mafuta ndani ya UAE. Ni mwendo wa nusu saa kutoka Dubai kuufikia mji huo.

Kuna cha mshangao ulioko, ni namna ruksa iliyoko kwa kiongozi wa taifa, Sheikh Mohamed Bin Rashid, alivyotoa uhuru kwa watalii na raia wa kawaida kufika kwenye makazi yake maarufu kama ‘Zabir Palace’ kwa ajili ya kupiga picha na hata kupiga soga.

Mamia ya watalii wamekuwa wakifika kwenye makazi hayo kupiga picha, bila ya kuvuka kizuizi kinachoelekea kwenye geti kubwa yaliko makazi rasmi kupiga soga na picha kadri wanavyotaka, pasipo kubughudhiwa na mtu.

Mwongoza watalii Mohamed, anayeniambia amefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 20, anasema kilichosababisha Sheikh Mohamed kutoa uhuru wa kwenda kwenye makazi yake, ni baada ya kusikia maombi mengi ya wanaotaka kumjua, hasa alivyoleta mageuzi makubwa nchini humo kwa muda mfupi.

“Sheikh Mohamed ni mtu wa watu, ni mtu anayefanya mambo makubwa kwa nchi yake, lakini yuko kawaida sana, aliposikia watu wengi wakiwamo watalii wakitaka kujua yalipo makazi yake, alisema ‘waacheni watu waje’ ndipo ukaanza utaratibu huo,” anaeleza Mohamed.

HAKUNA UCHAGUZI

Licha ya kuwapo maenedeleo makubwa, nchi hiyo haina mfumo wa kuwa na uchaguzi na mmoja wa wenyeji wa Nipashe, katika ziara yake huko, anasema wananchi wameridhika na kutohusishwa na hatua hiyo ya demokrasia, badala yake wamejikita kwenye uzalishaji mali, biashara na uchumi kwa ujumla.

“Kila taifa ndani ya UAE lina kiongozi wake na kiongozi wa jumla wa UAE kwa sasa ni Sheikh Khalifa. Iwapo litatokea lolote wakataka kupata kiongozi mwingine, wanakaa hawa masheikh wa mataifa yaliyounda UAE wanachagua kiongozi wao wenyewe,” anasema.

BAHARI BANDIA

Maajabu mengine ya Dubai, ni namna walivyotengeneza bahari bandia katikati ya mji, kwa kuchimba kiasi cha kilomita nne na kuunganishwa eneo na maji ya bahari, kisha kukatengenezwa eneo maarufu kwa watalii kwa jina la Marine Parks.

Hapo pana la kushangaza na inamchukua mtu muda kuamini ‘bahari bandia’ katikati ya jiji kutokana na ukubwa na mwonekano. Hapo pamesheheni watalii wanaoshangaa.

Mtalii mmoja kutoka Serbia, Abela Sakitasna tuliyekuwa naye kwenye boti tukitalii kwenye bahari hiyo bandia, alinieleza kwamba hata yeye hakuamini kirahisi alipoambiwa kuwa hiyo ni kazi ya binadamu na kwamba si eneo la asili.

“Mandhari ya kuvutia sana nimependa sana huu ubunifu mkubwa, kuleta bahari katikati ya mji ni wazo la ajabu kabisa huwezi kuamini hata kidogo,” alieleza mtalii huyo,

Vivutio vya utalii Dubai na watalii wanaofurika hasa msimu wa baridi kutoka mataifa mbalimbali duniani ni wengi sana.

Mbali na eneo hilo, mji huo una fukwe za nyingi, bustani za kushangaza, majengo marefu zaidi duniani na mchanganyiko wa watu wa jamii zote duniani.

Kuna kivutio cha kipekee, hapo ni bustani ya maajabu maarufu kama Miracle Garden, kama inavyojieleza kwa jina lake. Ni bustani ya maajabu kutokana na ustadi na ubunifu mkubwa uliotumiwa na wataalamu kuitengeneza.

Ni kivutio kikubwa cha watalii hasa msimu wa baridi kwenda kushuhudia usanifu wa kipekee na kustaajabisha, uliofanywa na wajenzi mahiri duniani.

Mmoja wa watalii kutoka nchini Lithuania, Jane Brendes, aliniambia kuwa maishani mwake hajawahi kuona bustani inayostaajabisha kama hiyo, iliyosheheni kila aina ya maua yenye mambo tofauti na ya kuvutia.

“Hii ni ajabu kweli. Huu ni ujuzi uliofanywa na watu wanaoipenda kazi yao, kuchanganya maua mazuri kwa kiwango hiki na kuwa na maumbo ya kushangaza. Ni jambo lenye kuleta mvuto nilikuwa nasikia ‘Miracle Garden’ nashukuru nimeona mwenyewe,” anasimulia mtalii huyo.

Eneo lingine lenye mvuto wa ajabu ni jangwa lililoko umbali wa kilomita 40 kutoka jijini, ambako watalii hutembelea huko msimu wa utalii kuona wanyama mbalimbali kama ngamia, kwenye eneo maarufu kama ‘Dubai Sunset Desert Safari.’

Hapo pamekuwa mvuto wa kipekee, hasa namna magari yanavyosafiri ndani ya jangwa, kutokana na kuwa na miinuko mikubwa na miteremko mikali, kiasi kwamba mtalii anaweza kudhani gari linaanguka.

Kutokana na hali hiyo, sasa yanapelekwa magari ya kisasa yanayosukuma magurudumu manne yaani ‘four wheel drive’ kwani wenyeji wanasema magari mengine hayawezi kufika maeneo husika yanayolengwa.

MAENEO YA AJABU

Maajabu mengine ya Dubai ni kitu kinachoitwa La Perle. Ni ukumbi wa maonyesho wenye maajabu ya kushangaza duniani, ukiwa na jumla ya viti 1,300 uliojengwa chini ya hoteli. Umetengenezwa kwa nakshi za ajabu, kiasi cha kushangaza wengi wanaofika kushuhudia maonyesho ya sanaa yanayofanywa kwenye ukumbi huu.

Hapo kuna bwawa la kuogelea lililoko kwenye ukumbi huo ni la maajabu, kwani wasanii wamekuwa wakizama na wasionekane walikotokea.

Katika onyesho la hivi karibuni, jumla ya watu zaidi ya 1,000 waliokuwa kwenye ukumbi huo, walishikwa na butwaa kuona mmoja wa vijana waliokuja kama watazamaji, kutoswa kwenye bwawa hilo na kutoonekana tena.

Umati waliokuwa kwenye ukumbini wakiwa wanasubiri kuona nini kitatokea, walishangaa baada ya dakika 20 kijana huyo kutokea kwenye paa la ukumbi huo, hali iliyozidisha mvuto kwenye onyesho hilo, hivyo kusababisha shangwe.

Maporomoko ya maji kwenye ukumbi huo, ni maajabu ya kusisimua, kwani kuna wakati hutokea maporomoko ya maji kutoka kwenye kona mbalimbali za jingo, hilo kiasi cha kusababisha maji kujaa kuanzia kwenye bwawa la kuogelea lililojengwa kwenye eneo hilo, kisha yanatoweka katika mazingira ya kutatanisha na ajabu.

Mtalii kutoka Hispania, Berbas Bornos, aliyehudhuria onyesho hilo, aliniambia kuwa wahandisi waliojenga ukumbi huo wamekwenda mbele zaidi kwa namna ulivyonakshiwa kwa teknolojia na ubunifu wa ajabu.

“Nimeshuhudia mambo mengi ya ajabu, lakini ukumbi huu ni aina yake na kwangu mimi yanayofanyika hapa ni maajabu, kweli ni maajabu na katika akili ya kawaida inashangaza sana,” anasema.

Dubai Parks and Resorts ni eneo lingine la burudani la maajabu ya kuvutia maelfu ya watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani, yaliyomo ndani ya eneo hilo maarufu lililoko kilomita 25 kutoka katikati ya jiji.

Ndani ya eneo hilo kuna majengo yaliyosheheni maajabu mbalimbali likiwamo lile maarufu kama Dream works. Kwa uhakika hili ni eneo lililojaa maajabu mbalimbali kiasi kwamba mtalii hujiona kama yuko sayari nyingine.

Ndani ya jengo la ‘Dream Works’ kama linavyojitambulisha kweli kazi za ajabu zimefanyika kwa ustadi mkubwa, maajabu ambayo mtu hawezi kuamini kwamba binadamu anaunda vitu vya kustaajabisha kwa kiwango hicho.

Watalii wanaoingia ndani ya jengo hilo, hutembezwa chini ya ardhi kulikowekwa sanamu mbalimbali wanayozungumza na kufanya shughuli, mithili ya binadamu na wakati mwingine inatisha kuangalia, kwani maeneo mengi ni giza.

Mfano chini ya ardhi kwenye eneo hilo mtalii anayezungushwa kwa magari maalum yanavyosukumwa na umeme, anakutana na bendi za muziki za sanamu ambazo mtu anaweza kudhani watu halisi, kumbe sanaa.

Kwingine kunakoifanya Dubai kuwa na majabu ya kitaliii kutoka kinakoitwa Global Village, eneo lenye ukubwa wa wilaya nzima.

Hapo ndani yake kuna maduka ya kila taifa duniani yanayouza bidhaa zinazotengenezwa na mataifa hayo.

Ni eneo linalopata watalii wengi zaidi, kutokana na mvuto wake hasa bidhaa zinazopatikana kwa wingi na kama panavyojitambulisha kwa jina la ‘Global Village’ kweli ni kijiji cha dunia kutokana na maelfu kwa wafanyabiashara wa mataifa mbalimbali walivyokusanyika kuweka maduka yao katika msimu wa baridi unaoanzia Novemba hadi Aprili ya kila mwaka.

JENGO REFU

Kwa watalii wengi wanaotembelea Dubai hawawezi kuondoka bila kufika jengo refu kuliko yote duniani maarufu kama ‘Burji Khalifa’ lenye ghorofa zipatazo 160 ndani kumesheheni mambo mengi ya kuvutia.

Ni eneo ambalo muda mwingi lina msongamano wa watu wanaofurika kutaka kupata fursa ya kufika kileleni mwake.

Pia kuna eneo lingine jirani la Dubai Shopping Malls ambalo lina ghorofa tatu na maduka yanayoelezwa kufikia 1,250 yaliyosheheni bidhaa mbalimbali kila mahali duniani.

Kwa watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani, ni eneo ambalo wanakutana na msongamano wa ama wakiingia na kutoka, kwani ni eneo mtu anaweza kupata kila anachokitaka. Ama kweli Dubai, kuna maajabu ya utalii duniani.

Habari Kubwa