Kumkosa Nyerere kunavyopishana na uchumi

18Oct 2019
Profesa Godius Kahyarara
Dar es Salaam
Nipashe
Kumkosa Nyerere kunavyopishana na uchumi
  • Hakuuvaa Ukomunisti, wala Ujamaa Mapinduzi
  • Shida haikuwa Ujamaa, bali mitikisiko kiuchumi

MTU anapotafsiri mfumo wa uchumi wa Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, ni kwamba uliangukia ujamaa wa kidemokrasia, uhuru wa kiuchumi, kujitegemea, usawa haki na fursa ya kumiliki na kunufaika na uchumi wa kitaifa.

Profesa Godius Kahyarara.

Kiongozi  huyo alichukia mfumo wa kinyonyaji uchumi duniani na umuhimu wa nchi kusimamia uchumi, kujitosheleza kwa kujenga viwanda na kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje.

Mwalimu Nyerere, alikataa masharti ya vyombo vya fedha vya kimataifa; Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, yaliyokuwa kinyume na sera na mwelekeo wa Tanzania wakati ule.

Madhara ya masharti hayo, yalionekana katika kulazimisha mashirika hayo kubadili mtazamo na kuanzisha Mikakati ya Kuondoa Umasikini na Nafuu ya Madeni, mambo ambayo Mwalimu Nyerere aliyatabiri mwaka 1979.

Wakosoaji wa Sera za uchumi za Mwalimu Nyerere, baadhi yao waenda mbali na majibu mepesi kuwa Mwalimu Nyerere, hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya uchumi.

Lakini kiuhalisia, kiongozi huyo wa nchi, msomi wa kiwango cha juu, akiwa na shahada ya uzamili aliyosomea fani za Uchumi, Siasa, Anthropolojia ya Jami, Sheria ya Katiba na Faslsafa ya Kiimani.

Ni katika zama watu hizo wachache walipata fursa ya kusoma mchanganyiko huo wa kitaaluma. Kimsingi, anthropolojia, inatafsirika kuwa “elimu ya binadamu inayohusiana na habari za asili na maendeleo yake ya awali.”

Hivyo, Rais Nyerere, alikuwa na uwezo mkubwa kimataifa katika kufuatilia na kushiriki mijadala na mipango ya uchumi kimataifa na ule wa nchini.

ALIKOSIMAMA KIUCHUMI

Mwalimu Nyerere aliamini katika ujamaa wa kidemokrasia, ambao ni tofauti sana na ukomunisti, uliojikita katika falsafa za Kina Karl Marx na Fredick Engels chini ya muunganiko wa nchi za kisoshalist kama za Urusi, China au Cuba, zilizojikita katika mapinduzi ya wanyonge walionyonywa na mabepari na kutawala dola.

Ujamaa aliousimamia Mwalimu Nyerere, chimbuko lake ni Ulaya Magharibi na unajulikana kama Ujamaa wa Kidemokrasia (Fabian system) na ulianzia Uingereza na nchi za Ulaya.

Tofauti na mifumo hiyo mingine ya kijamaa, huo una sura ya hiari na umekuwapo kwa muda mrefu na bado unaishi.

Vyama kama vya Democrat nchini Marekani au Labuor ya Uingereza na nchi za Singapore, Emirates, Scandinavian, India na barani Asia, nyingi sera zake zinaangukia chungu kimoja na siasa za Mwalimu Nyerere.

Mtandao wake umejikita zaidi kwa wanyonge, wenye asili tofauti na Marekani hasa  weusi na jamii ya kiasia na msingi mkuu wa chama, ni usawa wa kijamii na kiuchumi, ukihimiza serikali kusimamia sera za kiuchumi kusaidia vyama vya wafanyakazi kumlinda mlaji na yale ambayo Mwalimu Nyerere aliyasimamia.

Kadhalika, chama cha Labor cha Uingereza, hata baadhi ya wasomi, wamekuwa wakihoji kwanini CCM haijabadili sera zake? Hapo inazaa swali jingine, kwanini Mwalimu Nyerere aliamini katika mfumo huo wa ujamaa wa kidemokrasia katika kujenga uchumi?

Ilikosimamia imani ni kwamba, kutokana na muundo wa maisha ya Waafrika, ikiwamo Tanzania, maisha ya jamii kushirikiana, kusikilizana na kujadiliana, mfumo sahihi wa maendeleo yao ungekuwa huo wa ujamaa wa kidemokrasia.

Msimamo ulikuwa ni kupigania uhuru wa kiuchumi, unaoshirikisha wananchi kupanga na kumiliki uchumi wa nchi yao, umma kumiliki rasilimali za taifa na kwa maendeleo ya kitaifa.

Mtazamo wa Mwalimu, alisimamia dhana Afrika kuwa na nguvu ya pamoja, ili ijitawale kiuchumi, iheshimike na kuwa na sauti katika mfumo wa uchumi wa dunia, kwa kuondoa unyonyaji hasa katika uuzaji bidhaa nchi za viwanda  na kupangaji bei.

Jingine, kiongozi huyo wa nchi alisimamia biashara baina ya nchi za Afrika kupitia OAU, kundi la mataifa 77 masikini na kushiriki katika mikataba kama ya Lome

Iko wazi aliwaongoza Watanzania kuanzisha ujenzi wa uchumi wa kijamaa wa kidemokrasia. Msingi mkuu ulikuwa ni uchumi uliojikita katika usawa na kuheshimiana; kuwapa haki raia nchini kumiliki uchumi ; kutoa haki ya kupata hifadhi ya maisha na mali  liyo nayo kwa mujibu wa sheria,

Mengine ni kuhakikisha haki ya malipo halali ya kazi; umiliki rasilimali za nchi kama dhamana kwa vizazi vijavyo na wajibu wa serikali kuhakikisha inasimamia ukuaji wa uchumi.

Njia kuu za uchumi ikiwamo viwanda, benki, mashamba makubwa, nyumba za kupangisha, migodi na rasilimali nyingine zilitaifishwa na kuhamishiwa milki ya umma.

HATUA YA MAFANIKIO

Katika kutekeleza mipago na mtazamo wa uchumi chini ya Mwalimu Nyerere, mafanikio makubwa ya viwanda yalipatikana, hasa kufikia katikati ya miaka ya 1970, nchi ikijitosheleza kwa bidhaa za viwandani.

Hapo zinaorodheshwa vifaa vya ujenzi, redio, umeme, nguo, vyakula, vinywaji, dawa na pembejeo. Mchango wa sekta ya viwanda kwa Pato la Taifa liliongezeka kwa asilimia 400.

Mchango wa sekta ya viwanda ajira ni kwa asilimia mia 500 na uwekezaji hiyo ilipaa sana, huku mauzo ya nje yaliongezeka kwa zaidi, kutoka asilimia 9.9 ya mwaka 1966 hadi asilimia 22.3 katika miaka ya 1980.

Pia, Tanzania ilifanikiwa kupunguza utegemezi wa bidhaa zilizoagizwa kutoka nje hasa vifaa vya shule, nguo, vyakula, vyombo vya nyumbani, mbolea na maeneo mengine.

Maendeleo katika sekta ya kilimo Mwalimu Nyerere, alihimiza kilimo katika ngazi ya vijiji na mashamba makubwa kupitia sera na maelekezo kama vile Siasa ni Kilimo; Kilimo cha Kufa na Kupona; Kilimo ni Uti wa Mgongo.

Tanzania iliendelea kuwa mzalishaji mkubwa duniani wa mazao kama mkonge, korosho, chai, pareto, tumbaku, kahawa na karafuu na nchi iliwekeza zaidi katika utafiti na vituo vya utafiti wa mbegu bora kama vile: Ukiriguru- Mwanza; Uyole, Mbeya; Ilonga- Kilosa; Maruku Bukoba’ na Naliendele iliyoko Masasi.

Hiyo iliendana na Kuimarishwa kwa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, ambacho awali kilikuwa Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ni mafanikio yaliyokuwa wazi nchi kuwa na akiba zaidi ya fedha za kigeni kuliko matumizi yake  ambayo kitalamu inatamkwa ‘Positive Trade Balance’ na ndio jambo lililopandisha thamani ya fedha za Kitanzania. Inakumbukwa wakati huo, kila Dola moja  ya Kitanzania, ilikuwa na thamani ya shilingi tano.

Ndio zama wastani wa miongo minne sasa inatimu mabasi ya daladala yalizaliwa, kwa maana ya kutoza nauli kwa bei ya shilingi tano.

Pia, ndio wakati ambao Paundi za Uingereza zilikuwa na thamani ya Sh. 20. Hata waliodai kama vile Benki ya Dunia na IMF, kwamba shilingi ilipandishwa zaidi thamani kuliko uhalisia. Dai la thamani ya shilingi ya Tanzania ilizidishwa kwa wastani wa asilimia 57.

MATATIZO UCHUMI

Kuanzia katikati ya miaka ya 1970 mpaka mwanzoni mwa 1980, kulikuwapo matatizo ya kiuchumi kitaifa, baadhi ya walioko nje ya nchi kunyooshea mkono sera ambazo hazikuwa sahihi.

Hata hivyo, taarifa zilizopo zinasisitiza kuwa matatizo haya hayakutokana na sera za uchumi za serikali ya Mwalimu Nyerere, bali yalitokea wakati akiwa Rais wa nchi. Ni matatizo yanayoorodheshwa katika maeneo kadhaa;

Mosi, kuna suala la kupanda bei ya mafuta kwa asilimia 400 na hatimaye serikali ilijikuta ikitumia asilimia 60 ya fedha za kigeni kuagiza mafuta peke yake.

Pili, ni kuvunjika iliyokuwa  Jumuiya ya Afrika (EAC) mwaka 1977, kuliilazimisha Tanzania kuwekeza katika mashirika ya Reli(TRC), Ndege (ATC), Posta na Mawasiliano (TPTC) na Bandari (TPH), ili kuzinusuru huduma hizo.

Tatu, ilikuwa suala la kutokea ukame uliaothiri sehemu kubwa ya nchi, huku soko la mazao la mkonge duniani lilianguka. Awali zao hilo lilikuwa na soko kubwa kuingiza zaidi fedha za kigeni, kufungua biashara na ajira mjini na shambani.

Jambo la nne linatajwa kuwa, mwaka 1978, Tanzania ililazimika kuingia katika vita na Uganda.

Inaelezwa, katika kupambana na matatizo haya makuu manne, ndipo Rais Nyerere alianzisha mchakato wa kuwa na mfumo wa kuzalisha umeme, mradi wa Stiglers Gauge.

Katika hilo, mtikisiko wa bei ya mafuta uliifanya nchi kutumia zaidi ya asilimia 90 ya umeme unaowashwa kwa kutumia mafuta na serikali ikitumia asilimia 60 ya akiba yake fedha za kigeni, kuagiza mafuta.

Ukame huo ulilazimisha uagizaji chakula kutoka nje ya nchi na ni matatizo hayo yanayoweza kudondosha uchumi wowote uwe wa kijamaa kibepari au kikabaila. Ni mitikisiko wa kiuchumi, ambao kitaalamu hakukuwa na  uhusiano wowote na sera zilizobuniwa na kusimamiwa.

NINI CHA KUJIFUNZA?

Umuhimu wa kujitegemea ili kuwa na uhuru kiuchumi

Viwanda ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo na hatimaye nchi kwa ujumla

Mkakati wa kuchataka angalau asilimia 85 ya pamba kujitosheleza wenyewe

Ni vyema serikali ikaendelea kusimamia uchumi ikiwamo viwango vya riba, kulinda thamani ya shilingi na usimamizi wa uzalishaji kuanzia ugani, pembejeo, bei na upatikanaji wa masoko.

Nchi masikini iendelee kuwa na sauti ya pamoja katika kupigania usawa katika uchumi wa dunia.

Afrika ina fursa ya kukuza biashara miongoni mwao na kubadilishana uzoefu wa kiuchumi.

Mashirika ya umma yakisimamiwa vizuri, yana faida zaidi kwani serikali inapata kodi pamoja na gawio tofauti, biashara binafsi ambazo zinatoa kodi peke yake.

Sera ya ujamaa na kujitegemea bado haijapitwa na wakati na ni tofauti za kimtazamo kwani ujamaa wa kidemokrasia una fursa ya kuamua aina ya mfumo wa uchumi na si kweli mfumo wa kiuchumi ndio inaamua mfumo wa itikadi.

Inaelezwa, bado fedha nyingi zinatengwa kwa ajili ya sekta kuu kama afya na elimu na kuna bodi ya mikopo, bodi ya nafaka, bima ya afya, hifadhi ya jamii, huduma za ugani kwa wakulima, vyote vinategemea ruzuku kubwa ya serikali.

Kitaaluma, mwandishi wa makala hii bingwa wa uchumi.

Habari Kubwa