Kuna haja ya kutafuta kiini cha mauaji haya

27Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kuna haja ya kutafuta kiini cha mauaji haya

UNAPOSHIKA magazeti, kusoma mitandaoni au kusikiliza vyombo vya habari kinachojiri ni habari za matukio ya mauaji ya watu wakiwamo wake kuuliwa na waume au watoto kuuawa na walezi akiwamo baba wa kufikia.

KUKITHIRI KWA MAUAJI

Mume kuua mkewe au  mke kumuua mumewe na mama au baba kuua mtoto  sababu  ni wivu wa kimapenzi, chuki,  kuiba fedha ambayo ni kiasi kidogo , sababu nyingine ni  kuchelewa kupika au kuunguza mboga, ndiyo yanayojiri kwenye vyombo vya habari.

 

Matukio hayo yanazidi kuongezeka siku hadi siku kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari . Jambo ambalo limenifanya niwaze kwa sauti kupitia ukurasa huu ni hofu kuwa huenda wanaotenda matukio hayo wanakuwa pengine na tatizo kiakili.

 

Matukio ya wivu wa kimapenzi yamekuwepo enzi na enzi kutokana na ukweli kuwa mapenzi yanagusa hisia na mtu anapoingiliwa kwenye mahusiano au ndoa yake huweza kufanya jambo ambalo baadaye hulijutia.

 

Lakini haya ya watoto kuuwa na wazazi au walezi na wengine chanzo kikiwa ni wivu wa mapenzi nayo yanasikitisha kwamba mtoto anaingiaje kwenye mgogoro wa wazazi naye kuwa mhanga wa mgogoro kiasi cha kuchinjwa kwa madai kuwa mama alizaa na mtu mwingine na baba kubambikiwa.

 

Matukio mengine ni mama kumchinja mtoto wake kwa kuwa ametumia chenji au ameiba fedha, najiuliza kwa kumuua mtoto huyo ndiyo fedha itarudi? Ndiyo utakuwa umetatua tatizo au umesababisha shida kubwa zaidi  ya kutupwa  gerezani kwa maisha  yote.

 

Kwa baba anayeua mtoto naye atajikuta katika mateso hayo  kwa kuwa kwa mujibu wa sheria kuua ni jinai tena ni shitaka lisilo na dhamana, maana yake kwa kipindi chote cha kusubiri kesi kusikilizwa hadi hukumu utakuwa mahabusu.

 

Mara zote kesi za mauaji huchukua muda mrefu kusikilizwa na kutoa hukumu ikihusisha vikao vya  Mahakama Kuu vinavyofanywa mara moja kwa mwaka.

 

Lakini kama jamii yatupasa tujiulize ni kwanini matukio haya yanaongezeka ? Kuna nini kiasi cha kushindwa kudhibiti wingi wa hasira?

 

Kwamba unakuwa na hasira hadi unashika kisu, panga, shoka au kitu chochote unampiga nacho mtoto au  mwenza au unamkatakata hadi anakufa kwasababu umehisi ana mahusiano mengine au mtoto ameiba?

 

Ni sawa na matukio ya ulawiti wa watoto wa kiume nayo yanaongezeka kila uchao, jambo linalonifanya nijiulize kwa kufanya hivi anafaidika nini?  Kwamba hakuna wanawake anaoweza kuwa na mahusiano nao hadi amharibu mtoto wa mwenzako?

 

Kuendelea kuwapo kwa matukio haya yanayotendwa kwa watoto wadogo ambao hawawezi kujitetea ni jambo lenye kuumiza sana kwa kuwa wapo waliodanganywa kwa kupewa zawadi ndogo ndogo na wengine kufanyiwa ukatili wa ngono kwa vitisho vya kuuawa.

 

Kama wanajamii wanapaswa kuanza kuchukua hatua madhubuti dhidi ya matukio haya ambayo mengi yana athari za kisaikolojia kwa watu wote, unapomuua mtoto lazima wazazi wataumia na watabaki hawana maelewano maisha yote.

 

Unapoua mke au mume utaanzisha  uhasama baina ya ndugu wa pande zote na hakuna uwezakano wa jamii hizo kuishi kwa kuelewana na wakati huo kuna watoto wenye damu za pande zote.

 

Inapotokea mzazi mmoja ameondoka kwa kuhukumiwa kifungo gerezani watoto watabaki na mzazi mmoja, lakini wataishi na sonona  maishani na kuathirika katika ukuaji wao.

 

Kwa mke au mpenzi aliyeuawa na mzazi mwenzie maana yake ni kuingia kwenye mgogoro na watoto wake ambao tayari yamelazimishwa kubaki yatima kwamba mzazi mmoja yupo gerezani na mwingine amefariki na sasa hawana mtu wa kuwahudumia.

 

Haya yanatengeneza watoto wa mazingira magumu ambao hawana wa kuwalea kwa kuwa uzoefu unaonyesha wengi waliolelewa kwa ndugu wamepitia mateso kiasi cha kukimbilia mitaani.

 

Ni vyema kila mmoja akajiuliza faida za matukio haya na wataalamu wanasema haifai kufanya maamuzi wakati una furaha au hasira sana, kwa kuwa hautakuwa na muda wa kujiuliza maswali mengi katika kufanikisha jambo . Utalifanya kwa hasira au kwa furaha  hivyo kusababisha matatizo makubwa zaidi.

 

Jamii isiishie kusikitikia matukio hayo bali ianze kuchukua hatua madhubuti ikiwamo vikao vya mitaa na vijiji kuzungumza ubaya wa kutenda hivyo na kujipanga kuhakikisha kunakuwa na mikakati ya maadili na kuandaa jamii au kizazi cha kesho.

 

Tutafakari!

 

Habari Kubwa