Kung’ara kwa walima tangawizi kitaifa Same na magonjwa kuwavuta shati

13May 2022
Ashton Balaigwa
SAME
Nipashe
Kung’ara kwa walima tangawizi kitaifa Same na magonjwa kuwavuta shati

TANGAWIZI ni zao la viungo nchini linalostawi milimani na baadhi ukanda wa tambarare, maeneo ya kitropiki kutoka usawa wa bahari, mwinuko wa mita 1500 au zaidi na inahitaji mvua kiasi cha milimita 1200 hadi 1800 na joto sentigredi 20 hadi 25, lenye udongo tifutifu, rutuba na isiotuamisha maji.

Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka TARI Makao Makuu, Dk Joel Meliyo (wa pili kutoka kushoto),akitoa elimu kwa wakulima kuhusu magonjwa yanayoshambulia tangawizi katika kata ya Miamba wilaya Same mkoani Kilimanjaro. PICHA: ASHTON BALAIGWA.

Hapo kunapatikana mikoa ya Kilimanjaro wilayani Same, Mbeya, Ruvuma, Morogoro, Kigoma ,Pwani, Kagera, pia visiwani Zanzibar.

Tangawizi ni kiungo kinachoongeza ladha na harufu katika vinywaji kama juisi, pia vyakula nyama, mikate, biskuti na keki. Pia, ni muhimu katika utengenezaji dawa kama za mafua,kikohozi na pumu,

Umaarufu wake umeongezeka  karibuni kutokana na mlipuko wa ugonjwa Covid 19, tangawizi imetumika katika dawa mbalimbali kutibu au kinga dhidi ya maradhi hayo.

MAMBO YA SAME

Wilaya ya Same ina historia ya kuongoza kilimo cha tangawizi, kuanzia kata ya Miamba tangu mwanzoni mwa miaka 1990 na baadae kuenea katika kata nyingine tisa, ambako kilimo hicho kimeshamiri.

Mwenyekiti wa Ushirika wa Wakulima wa Tangawizi, Mbaraka Ally,anasema kuongezeka uzalishaji unaofikia zaidi ya tani 25,000 kila msimu, umeshinikiza kuanzishwa kiwanda cha kusindika tangawizi kikubwa zaidi Ukanda wa Afrika Mashariki.

Ghafla kuanzia mwaka 2018, uzalishaji tangawizi ulianza kukumbwa na changamoto ya mlipuko wa magonjwa kama kuoza matunguu na madoa kwenye majani yanayobadilika rangi kuwa njano.

Hapo ikachangia uzalishaji kushuka kwa kasi kutoka wastani tani 25 hadi 30 kwa ekari, kuteremka kuwa tani 10 hadi 15.

Hilo likamuibua aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo (sasa Waziri) Hussein Bashe, mnamo Julai 18 hadi 9 mwaka jana, akafanya ziara wilayani Same alikopokea malalamiko ya wakulima katika kata ya Miamba, kuhusu kuwapo magonjwa yanayoozesha tangawizi.

Pia walimueleza Waziri Bashe  namna kipato chai kinashuka, wakiomba serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuingilia kati.

ALICHOKIFANYA BASHE

Baada ya kusikiliza kero hizo,Waziri Bashe aliagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI) kupeleka wataalamu wa magonjwa ya mimea kutafiti kinachoathiri tangawizi na kuwapa majibu wakulima, watatue tatizo hilo.

Aidha, akiagiza TARI kuanzisha Kitalu cha kuzalisha mbegu za tangawizi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Same, huku uongozi wa wilaya  ukipewa maelekezo kutenga eneo la kuikabidhi TARI, ambako kungetumika kuzalisha mbegu kwenye kata ya Miamba.

UTEKELEZAJI ULIVYO

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geoffrey Mkamilo,anasema wakapokea na kutekeleza agizo la Waziri Bashe haraka, kwa kupeleka timu ya watafiti kutoka kituo cha Tengeru, Arusha na walianza kazi  kwenye mashamba ya wakulima, walikochukua sampuli za udongo na majani ya zao hilo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha TARI -Tengeru,Mpoki Shimwela, anafafanua malengo mahususi yalikuwa kutambua aina ya magonjwa kwa kutembelea maeneo yaliyoathirika, pia kutoa ushauri wa namna bora ya kudhibiti magonjwa.

Anasema, walijikita katika aina ya vimelea vinavyosababisha magonjwa hayo, namna ya kuyadhibiti na kupunguza kusambaa ugonjwa wa kuoza na kukauka majani katika maeneo mengine kunakolimwa tangawizi.

MATOKEO YA UTAFITI.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wakulima na Mkuu wa Wilaya ya Same, Edward Mpogolo, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka TARI Makao Makuu,Dk. Joel Meliyo, anasema wamebaini kuwepo magonjwa yanayosababishwa na bakteria, pia fangasi, tatizo kuu ni kuwepo mbegu zisizo za uhakika zinazowezesha kubeba magonjwa, pia kupungua rutuba udongo.

Anafafanua, kubainika kilimo duni cha tangawizi na kutokuwapo chanzo salama cha uzalishaji au uhakika wa mbegu, wakulima wengi wakiandaa mbegu kienyeji.

Dk. Mileryo anasema wakulima wanatumia mbolea ya samadi zenye walakini wanazonunua kutoka  kwa wafugaji, kunakonyeshewa mvua, pia kukaa juani muda mrefu, kunapoteza virutubisho.

Anataja wamebaini magonjwa na dalili za upungufu mkubwa wa virutubisho, akivitaja kwa majina ya kitaalamu ‘Potassium’ na ‘Naitrojeni’ katika maeneo mengi ya uzalishaji.

Bosi huyo wa utafiti wa TARI, anasema wamebaini dalili za madoa katika majani zikiashiria kuwepo magonjwa yanayosababishwa na viini vya ugonjwa uitwao ‘Phyllosticta Zingiber’akifafanua dalili zake za madoa.

Dk. Meliyo anasema, kutokana na utafiti huo, wamewashauri wakulima wengi kusafisha mashamba, kuepuka umwagiliaji kwa njia ya anayoiita ‘sprinkier’ inayoeneza magonjwa na kufanya kilimo cha mzunguko kwa maeneo yaliyoathirika, wakipanda mazao mengine yasiyokuwa katika kundi moja na mimea iliyoathirika.

Ushauri mwingine anautaja, wakulima watumie mbolea za viwandani na samadi, wakifuata kiwango kinachoshauriwa kila mwaka cha ‘Naitrojeni’ na ‘Pottasium’ kwa kuwa tangawizi asili yake ni zao la mizizi, lipandwe kwa mstari kuwezesha kufanyika palizi na kunyanyua udongo.

AHADI YA TARI

Mratibu wa Taifa wa Usambazaji wa Teknolojia za Utafiti za Kilimo kutoka TARI Makao Makuu, Mshaghuley Ishika, anasema baada ya kubaini magumu ya wakulima, wanakusudia kuweka kambi katika vijiji hivyo kunakolimwa tangawizi wawaelimishe.

Ishika anadokeza wanayokusudia kuelimisha, ni namna ya kujua mbinu bora za ulimaji tangawizi, kuwasaidia, kujua matumizi bora ya mbolea na viuatilifu, muda sahihi wa kuvuna, kutengeneza mbolea ya mboji, badala ya samadi iliyo duni.

WAKULIMA WALIVYOPOKEA

Mkulima wa tangawizi kutoka kijiji cha Goha, William Kilango, anakiri wanafanya kilimo hicho bila ya kufuata kanuni bora, hata kusababisha kuangukia magumu ya magonjwa yanayoathiri zao hilo.

Hapo anaiomba TARI kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya Same, ipige kambi katika vijiji vyao wakiwaelimisha kilimo bora, ili iwafikie kwenye tija itakayoinua kipato chao.

Mkulima Kunt Mjema kutoka kata ya Miamba, ombi lake serikalini, waharakishiwe wataalamu kwa kuwa wameshaanza kutayarisha mashamba yao ya tangawizi.

Mkuu wa Wilaya ya Same Edward Mpogolo, anaipongeza TARI kuitikia haraka agizo la Waziri wa Kilimo, hata kufanikisha utafiti unaoondoa changamoto za walima tangawizi, akitaja inachangia asilimia 60 ya mapato ya wilaya.

Habari Kubwa