Kuondoa matumizi ya fedha za kigeni katika biashara: faida au harasa

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kuondoa matumizi ya fedha za kigeni katika biashara: faida au harasa

MABADILIKO yananukia katika mazingira ya biashara nchini, na katika kuthamanisha au kukisia thamani ya shilingi ya Tanzania, kutokana na kuzuia matumizi ya fedha za kigeni katika biashara za kawaida.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (Kushoto) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu (katikati) wakiwa katika moja ya mikutano ya kifedha nchini. PICHA: MTANDAO

Inaelekea fedha hizo zitatumika katika kubadilisha fedha ili kusafiri, au kwa malipo ya watu binafsi katika biashara ambako serikali haihusiki, lakini iwe ni makubaliano ambayo siyo sharti la kupata huduma eneo lolote, kwani kinacholengwa hasa ni hicho.

Ni kama vile kuna hasara pale nchi inapotumia fedha za nchi nyingine badala ya fedha zake yenyewe, hisia ambayo inazuia mjadala pale matumizi hayo yakisaidia utamanishi wa biashara.

Katika miaka iliyopita wakati biashara ya nyumba na viwanja maeneo ya ufukweni ikiwa imeshika kasi na watu wakiwa na fedha za kutumia, kimsingi bei zilikuwa zinatajwa kwa fedha za Marekani.

Ilirahisisha tarakimu kwa kulitaja kwa fedha zinazopunguza 'sifuri' tatu mwishoni katika matamshi, na wakati huo huo kulenga soko la wateja tarajiwa ambao wanatumia fedha za kigeni katika mahitaji yao ya kila siku.

Ni kama kutoa ishara kwao kuwa eneo hilo lina mazingira ya ugeni au mtu anakutana na wageni kwa urahisi, ajisikie vizuri zaidi kwani mchanganyiko huo unarahisisha mawasiliano ya kijamii, lugha inayotumika, au huduma.

Mahali ambapo labda kulikuwa na mshangao kiasi fulani ni pale ilipoelezwa kuwa hata Benki Kuu (BoT) imeagizwa kutotumia sarafu za kigeni katika kuuza amana za serikali, yaani kununua fedha kutoka mabenki kwa ajili ya shughuli za kila siku za serikali.

Zipo nchi kadhaa kama Afrika Kusini na hata Kenya ambao fedha yao ya ndani inaonekana katika masoko ya nchi za jirani kutokana na wingi wa biashara kati yao, na kwa sehemu isiyo haba Benki Kuu inachukua mikopo kwa fedha za nchi.

Katika mijadala inayoendelea hivi sasa, mkasa unanyemelea mabenki yenye fedha nyingi amana za serikali kwa fedha ya 'rand,' siyo kwa fedha za kigeni.

Serikali inaponunua bidhaa au huduma kwa fedha za ndani thamani yake inabaki hiyo hiyo ya kitarakimu (nominal, yaani kwa jina lake la awali, kama ni Sh.milioni 20 basi ni hiyo), na siyo inavyobadilishwa katika soko la fedha.

Inapoingia deni kwa fedha za kigeni ni suala lingine, kwani wakati wa kulipa itabidi ilipe kwa fedha za kigeni ambazo thamani yake kwa fedha za nchi ni tofauti na ilivyokuwa awali.

Ni hali ambayo ina maana kuwa anayetoa mkopo analindwa kutokana na mabadiliko ya thamani ya fedha katika soko, na anayepata mkopo (yaani serikali) ndiye anayebeba pengo hili, hivyo anatumia fedha nyingi zaidi kulipa deni.

Msingi wa fedha za serikali ni kodi, na sehemu kiasi tu ndiyo inayotokana na misaada kutoka nje, au mikopo.

Kuna mikopo na`misaada ya moja kwa moja kutoka nje ambayo lazima itakuwa katika kielelezo cha fedha za nje, na mahitaji ya mikopo ya ndani ambayo sasa itaendeshwa kwa fedha za nchi, kwa mujibu wa tangazo hilo.

Ndiyo hapa kuna suala la athari za tangazo hilo kwa biashara ya fedha na upatikanaji wa mikopo ya kuendesha shughuli za serikali endapo kila kitu kitafanywa kwa fedha za ndani, halafu pia kuna suala la thamani ya shilingi katika mazingira hayo, linaloendana na upatikanaji wa mikopo, mazingira yake kiutawala.

Tatizo muhimu ni kuwa pale mikopo inapotokana na fedha za ndani thamani yake inaporomoka pale thamani ya shilingi inapobadilika katika soko, na inavyoelekea hivi sasa mlinganisho wa kila siku wa shilingi na fedha za nje utapungua, kwani soko litakuwa limepungua.

Kwa mfano wakati wa Bajeti ya Serikali pale inapotakiwa mikopo ya ndani, haitokani na mabenki ya ndani ambayo kimsingi yanatumia shilingi, kwa kuwa hawana amana za kuweza kuikopesha serikali fedha za uhakika na wao kuendelea na biashara bila matatizo.

Ni mabenki ya nje yenye amana za ziada, kwa mfano wakala wa M-Pesa anavyotafuta 'float,' ndivyo nao wanavyouliza makwao.

Kimsingi fedha hizo siyo za Tanzania na haziko katika shilingi yetu, ila zina thamani kiasi fulani kwa fedha zetu wakati mkopo unapotolewa, na sasa kama unapotolewa kwa fedha zetu ina maana kuwa wanatoa mkopo kama benki ya ndani yenye amana kubwa, si kama benki ya nje.

Ina maana benki ya nje kwanza inunue fedha za ndani Benki Kuu halafu iikopeshe serikali kwa fedha za ndani, jambo ambalo linaleta ukakasi kibiashara.

Ina maana kuwa mabenki ya ndani kwa viwango tofauti yatakuwa yanatoa amana zao za uendeshaji wa kawaida kutoa mikopo kwa serikali, kama ambavyo zinakopesha wafanyabiashara, au serikali, amana chache.

Moja ya athari za hatua hiyo ni kupunguza utoaji nje fedha zinazotokana na faida ya mauzo ya amana za serikali hasa kwa mabenki ya nje yenye amana za fedha za kigeni au kuweza kuita viwango tofauti vya fedha hizo kulingana na makubaliano ya malipo (utoaji wa mkopo) kwa wakati uliopo.

Hatua hiyo itapanua wigo wa kushiriki kwa mabenki tofauti katika soko la fedha kununua amana za serikali (hati za kuikopesha kwa riba maalum) na hivyo kugawana faida zake kwa upana zaidi kati ya mabenki.

Lakini matokeo yake ni kuwa benki zitalenga zaidi kuikopesha serikali kuliko ilivyo sasa, kwani wale wa fedha za kigeni ni kama wanaondolewa.

Hatua hiyo vile vile inaweza kuathiri uwezo wa Wizara ya Fedha na wizara zinazoendesha mashirika ya umma yenye mahitaji ya mikopo, kwa mfano TANESCO ambako mwaka 2006 Waziri wa Fedha Zakhia Meghji aliinua mkopo wa pamoja (consortium) kati ya mabenki kadhaa, lakini zaidi ilikuwa nibenki ya Stanbic, mkopeshaji mkuu wa serikali, kiasi cha shilingi bilioni 350.

Ni wazi kuwa mikopo kama hiyo (ya kibajeti) itaendelea kutolewa kwa fedha za kigeni, ila mikopo midogo midogo ya uendeshaji (kujazia mahitaji ya) shughuli za kila siku ni budi sasa iwe kwa fedha za ndani. Serikali itapunguza mzigo wa kulipa fedha za kigeni, ila mikopo itapungua.

Umuhimu wa hatua hiyo kiuchumi unarudisha suala hilo katika kile alichosema Mwalimu zama zile, kuwa "kupanga ni kuchagua," hivyo serikali inaelekea zaidi kupunguza deni la serikali na jinsi linavyokua kila mwaka, kwani sehemu yake kubwa ikiwa katika fedha za kigeni linakua kwa haraka zaidi.

Hivyo madeni ya kawaida yatakuwa kwa fedha za ndani, na hivyo yatakatwa makali yake kutokana na kubadili fedha hizo kwa nyingi zaidi za kigeni, au kwa mapato bandarini ambako serikali inapata fedha nyingi za kigeni.

Ina maana vile vile kuwa biashara itabidi zijiendeshe zaidi kwa fedha inazokusanya na kulipwa, siyo zitegemee mikopo zaidi.