Kupeana nafasi wangapi watarudi kwa mwaka au watasomea wapi?

02Jun 2020
Michael Eneza
Dar es Salaam
Nipashe
Kupeana nafasi wangapi watarudi kwa mwaka au watasomea wapi?

WAKATI wanafunzi wanarudi vyuoni na kidato cha sita, suala linaibuka kuhusu mbinu za kuhakikisha kuwa wanaendelea na masomo, huku tahadhari zikichukuliwa kuhusu kusambazwa virusi vya corona.

Wanafunzi wa vyuo vikuu kote nchini, wameanza masomo jana baada ya serikali kufunga taasisi hizo mwezi Machi kuepusha kuenea virusi vya corona. PICHA MTANDAO.

Kwa kukisia kwa karibu, matazamio ya wakuu wa idara tofauti serikalini na uongozi wenyewe ni kuwa hatari ya corona iendelee kupungua kwa kasi hii ya sasa, na shughuli zirudi kama kawaida.

Ikiwa hivyo, Tanzania na labda nchi kadhaa nyingine za Afrika, au labda kwa wingi wao, zitakuwa visiwa ambako janga la corona limepita pembeni, wakati dunia ikihangaika na maelfu ya vifo.

Hata hivyo matazamio hayo hayawezi kuwa msingi wa kusimamia sekta za uchumi kwa jumla na elimu kwa upande mwingine, ambayo ni sekta ya huduma za jamii kama ilivyo tiba.

Kukaa katika mfumo huo wa matazamio ni kuweka elimu rehani, ambako watu 10 wakipata corona katika kipindi kifupi, hatua za kwanza za kufunga mashule zinaanza upya, jambo ambalo halitawezekana.Unatakiwa mfumo wa kusimamia elimu kwa watoto na vijana wadogo, bila kuhatarisha afya zao na za familia pia.

Licha ya kuwa serikali ilitangaza kurudi shuleni kwa vijana wa kidato cha sita kwani wanaojiandaa kwa mitihani ya kitaifa, wakati inaangalia hali inavyokwenda kuhusu maambukizo ya corona kabla ya kufikia uamuzi kuhusu shule za msingi na sekondari, kuna kigezo kingine.

KUHITAJI NAFASI

Kurudi shuleni na vyuoni pia kumeambatana na hitaji la kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapeana nafasi wawapo darasani au katika mabweni.

Ndiyo maana inavyoelekea kuna ulazima wa mazingira ya uendeshaji wa sekta tofauti kijamii ubadilike, uendane na mahitaji ya janga la corona, ambako hadi sasa tunaweza kusema tumepona, ukilinganisha na kinachotokea maeneo mengi duniani, hata kwa majirani zetu.

Ina maana kuwa licha ya kwamba sisi ni kisiwa cha kuibana corona kwa kiasi fulani, bado kuna tahadhari ya muda mrefu tunayotakiwa kuitilia maanani, ili tusije kujifunza kwa njia ngumu zaidi, endapo kutojali kutatoa mwanya kwa maambukizo kupanuka kwa kasi. Na bado katika mazingira hayo elimu ya chini iendelee.

Dhana ya kupeana nafasi ndiyo itakayobadili kimsingi jinsi elimu inavyosimamiwa, kwani hitaji la kwanza la kila mtoto kupata elimu limefikiwa kwa kiwango fulani, ila katika mazingira ya watoto kutumia nafasi ndogo ya darasa ukilinganisha na miongozo iliyofuatwa kwa miaka mingi hapo awali.

Tatizo lilikuwa ukifuata miongozo ya idadi ya wanafunzi na waalimu kwa darasa moja, ukubwa wake na vifaa, utaishia kuwa na shule chache zenye ubora, na watoto wengi kubaki nyumbani bila elimu, wakitegemea makuzi kwa utamaduni wa makabila yao. Serikali ikakataa hilo.

Janga la corona linaingia na ‘rungu’ la kupasua utulivu huo kwa kuhitajika kuwapa watoto na vijana wadogo wa sekondari elimu katika mazingira ambako hawajazani. Haitakuwa vyema kutumia shule zilizopo ‘kwa nafasi’ halafu wengine wabaki nyumbani, ila kubadili mfumo wa matumizi ya raslimali ili elimu iwe na kipaumbele cha pekee, ikiwa ni pamoja na kutumia maeneo ya wazi yaliyojengwa, ambayo yamepigwa na corona hayawezi kutumika kiuchumi kwa ufanisi.

Ni njia pia ya kuelekeza uwezo wa kitaaluma wa vijana waliomaliza shule za sekondari na vyuo kuwapa kazi ya kusomesha mitaani kwa ujira wa kujikimu, tofauti na mshahara wa kawaida ila una uhakika, tofauti na kubangaiza kutafuta kazi.

Ili serikali iweze kupata fedha za kukodisha kwa bei poa (kwani ni majengo au sehemu za wazi ambazo hazitumiki kwa sasa) itabidi iangalie upya mifumo ya ajira na mishahara au marupurupu serikalini, na pia idadi ya waajiriwa katika sekta tofauti, ili kuokoa fedha.

Ina maana kuwa uwezo wa waliojiriwa serikalini kupanga maslahi wanayotaka (hali ambayo ilipungua sana baada ya kuingia awamu ya tano) utapungua zaidi, kwani elimu ndiyo urithi ambao wazazi wanawapa watoto wa wakati huo. Vijana wanakuwa wasindikizaji huku wakijiandaa kuchangia jukumu hilo, kwani sasa haliachiwi familia.

Suala la kupanga upya umuhimu wa elimu katika mfumo mzima wa jamii na raslimali siyo la nafasi peke yake ila linaonekana hata katika kufungua shule zenye kidato cha sita, kuacha vyuo na vyuo vikuu.

Baada ya shule kadhaa kutoa matangazo kuwa wanafunzi waje na vifaa au bidhaa zinazoweza kutumika endapo kuna tatizo la maambukizo ya corona, kama malimau, tangawizi na vinginevyo, wizara ilikataa jambo hilo kabisa.

Ilisema ni kazi ya shule kuhakikisha hilo, ambayo ni sawa na kusema ni Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ndiyo ihakikishe vifaa vya afya na visaidizi muhimu endapo tatizo linazuka. Wizara hiyo haitakuwa imejipanga kwa suala hilo na hapo kuna mkanganyiko.

Yako matazamio maeneo mengi duniani kuwa inaweza kupatikana chanjo ya corona hadi kufikia mwaka huu na kufanyiwa majaribio kwa makundi ya watu kuona kama inaweza kuzuia Covid-19.

Ila wanataaluma wanatofautiana kuhusu uwezekano huo kwani yako magonjwa yanayofanana na Covid-19 (homa kali ya mapafu) bado hayana chanjo.

Ni maradhi ambayo yapo kuanzia 2012 (SARS) na 2014 (MERS) ilioripotiwa Mashariki ya Kati, ila ni yote ni shida ya kupumua kama ilivyo homa ya ‘serious acute respiratory syndrome.’ SARS pia ilianza wakati virusi vya wanyama pori wanaoliwa China vilipoingia kwa binadamu, hali ambayo pia ni chanzo cha ugonjwa wa ebola uliojikita zaidi Congo, ambao pia wanadaiwa kula sokwe.

Habari Kubwa