Kupiga chabo ni maradhi ya akili?

23Sep 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Kupiga chabo ni maradhi ya akili?

MACHO hayana pazia, yanatazama kila pahala ilimradi mboni imeelekeza huko, tena yanaona mengi yakiwamo mazuri na mabaya, ya hatari na yenye kuokoa.

Wanawake wenye maumbile kama haya wanapovaa na kuonyesha maumbo yao, wanaweza kuwa chanzo cha watu kupenda kuwapiga  chabo.  PICHA: MTANDAO.

Huona yanayopendeza hata yanayochukiza. Huona yanayofurahisha na kuhuzunisha.

 

Macho hupeleka taarifa kwenye ubongo kwa yale inayoyatazama, ubongo hutafasiri, huvuta hisia za uzuri na uchungu.

 Tena macho hayana mipaka, kitakachoyazuia kuangalia hiki na kuacha kile hata kope zikipepesa pembeni ni kwa sekunde kadhaa, kisha hurudi kwenye hali yake ya kawaida ili kufaidi kilichokatiza mbele yake.

Macho hutazama pale mwanamume au mwanamke anaposhindwa kujisitiri na kukaa vibaya tena maungo yanayohitaji stara ya kufichwa yanapoonekana hapo hukazana kutazama kweli kweli. Pia mwanadada anapovaa nguo za kuonyesha maungo, akikatisha mbele ya watu wengine lazima shingo na jicho vielekee huko huko.

CHABO

Ni hayo macho hupiga chabo na kuwachungulia waliokuwa kwenye hali inayohitaji faragha kubwa. Hapa ndipo nilipotaka kupazungumzia, msamiati huu hutumika katika maeneo tofauti kumaanisha kuibia au kutazama kitu bila ridhaa ya wahusika au watenda jambo lenyewe.

Kwa mfano utakuta mwanafunzi darasani anapiga chabo ili kuibia majibu ya maswali au mtihani unaomshinda.

Lakini chabo ninayotaka kuijadili hapa ni mtu kuwachungulia watu wengine wakati wa kujamiiana, au wakivua nguo ama wakiwa watupu bila nguo.

Kwenye hili mpaka leo jamii ina mkanganyiko wa kujiuliza kuwa hii ni tabia au ni maradhi yanayomkabili mhusika. Kama ni ugonjwa chanzo ni nini, na unatibikaje? Iwapo ni tabia asili yake ni nini, je, tabia hiyo inaweza kubadilika na mtu akawa na mwenendo mwema?

Ukikaa vijiweni kwenye vijana wengi utasikia viroja ukikuta wanajadili au wanavyowajadili wapiga chabo huku wengine wakijinasibu kwa majigambo juu ya ubingwa wao katika chabo.

CHABO HULEMAZA

Kuna moja ya simulizi ambayo niliwahi kuisoma kuwa yupo  jamaa mmoja ambaye  mazoea ya kupiga chabo yalimfanya akawa anampiga chabo mkewe wa ndoa. Nukuu ya simulizi yake ni hii “nimekuwa mtu wa kupiga chabo sana kabla sijaoa lakini kwa sasa nimeoa nina mke na mtoto ila kale ka katabia bado kapo. Inafikia hatua namvizia mke wangu akiwa anaoga au amekaa ‘kihasara’ nampiga chabo bila kujua napata raha na moyo kusuuzika”.

Kisa kingine ambacho kilishawahi kutokea Novemba, 2017 na kuripotiwa na kituo cha East Afrika Radio ambapo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, alimsimamisha kazi Mwenyekiti wa Kijiji cha Sayu, Mataifa Balekele (54), kwa kulalamikiwa na wananchi kuwa ana tabia ya kuwachungulia kwenye madirisha wakiwa wamelala usiku. Na huko ni kupiga chabo.

Lakini ukirudi kwenye maisha ya uswahilini kuna watu wanajulikana kwamba mabingwa wa chabo na ukichunguza madirisha ya nyumba za maeneo hayo mengi utayakuta yana matundu, usidhani ni uchakavu, hasha ni kwa ajili ya chabo.

 Hali hiyo haiishii hapo, chunguza tena milango na madirisha ya nyumba za wageni za ‘uswazi’, gesti zilizo nyingi zina matundu ni ishara kwamba mwendo ni ule ule wa kupiga chabo.

MAKUNDI YA CHABO

Hawa wapiga chabo nawagawanya katika makundi makuu matatu. Kundi la kwanza wale wanaopenda kuona watu wengine wakiwa wanavua ama kubadili nguo, jingine raha yao ni kuwaona watu wengine wakijamiiana na kundi la mwisho wale wanaowachungulia watu wanaokaa vibaya.

Msomaji wangu hebu tutafakari kwa kina kuna raha gani pale unapotazama maungo ya mwili wa watu wengine ama kuwatazama wenzako wakifanya tendo la ndoa?

Kila aliyetafakari anaweza kuwa na jibu lake aidha lisilofanana na langu au msomaji mwingine. Wapiga chabo hufanya hivyo ili kupata mzuka wa kufanya tendo la ndoa na wapenzi wao ila wengine huhifadhi hizo kumbukumbu akilini na kuzitumia kwenye matumizi mengine ya kihisia.

Wanaohifadhi kumbukumbu ni wale wenye tabia za kujichua wenyewe, hivyo wakiwa wanafanya hivyo huvuta hisia za chabo zinazowasaidia kupata raha na kufikia mshindo kirahisi.

Unaweza kufikiri kuwa mpiga chabo baada ya kumchungulia mwanamke basi itakuwa njia ya kumsumbua na kuzungumza naye masuala ya uhusiano na mapenzi.

Hali hiyo huwa ni kinyume chake waathirika hawa walio wengi huwa hawawasumbui wale waliowaona kwa nia ya kuwataka kuwa nao kwenye uhusiano wa kimapenzi bali hufanya hivyo ili kupata hisia ambazo huwapa hisia za kufurahi zaidi kutoka kwenye tendo la ndoa.

Anapomchungulia mtu huona kama nyongeza kwake pale anapokwenda kujamiiana na mpenzi wake.

Kwa kawaida kati ya wanawake na wanaume, inaelezwa kuwa asilimia kubwa wanaume ndiyo wenye tabia ya kupiga chabo kuliko wanawake. Kisaikolojia chabo ni maradhi ya akili yanayompata mtu na kumfanya kupata hisia za kufurahia mapenzi kwa kuwatazama wengine wakiwa hawana nguo, au wakifanya tendo la ndoa.

 

NI UGONJWA WA AKILI

Kwa kitaalamu chabo ni matatizo ya akili na hujulikana kama“voyeurism”. Inasomwa ‘vouyarizimu’

Maradhi yapo kwenye kundi la magonjwa “paraphilia” ambapo ndani yake hujumuisha magonjwa yanayowahusisha wengine kupiga chabo, wapo wanaofanya mapenzi na wanyama kama mbuzi, ng’ombe na kondoo na kundi lingine ni la watu wazima  wanaofanya mapenzi na watoto wadogo.

Ufafanuzi wa aina ya magonjwa hayo unawasaidia kujibu maswali ya wale waliokuwa wanajiuliza kwamba kupiga chabo ni maradhi au tabia. Mpaka sasa hakuna sababu ya moja kwa moja inayooonyesha chanzo halisi kinachosababisha mpaka mtu anafikia hatua hii, lakini kuna mapito ambayo mtu akipitia anaweza kuangukia katika tabia hiyo ya kupiga chabo.

VICHOCHEO

Kwenye mtandao wa Psychology Today wametaja mambo yanayoweza  kusababisha jambo hilo ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, matumizi ya vileo kama vile pombe, bangi na mihadarati na hisia za kupata furaha zaidi. Mambo hayo yanaweza kuchangia mtu kuangukia kwenye tabia hizo.

Wataalamu wengine wa saikolojia wanasema kila mtu ni mpiga chabo pale anapopata fursa ya kufanya hivyo ila huogopa kujulikana ama kukamatwa hiyo huistahimili hali hiyo kwa kujificha asijulikane.

Jumapili Njema.

 

Habari Kubwa