Kusamehe wanaokukwaza ni tiba ya roho inayokuletea furaha

13Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kusamehe wanaokukwaza ni tiba ya roho inayokuletea furaha

BADO tumo ndani ya Januari, mtiti wa ada kwa watoto wanaorudi shule ni gumzo kwa wazazi na walezi huku suala hili likisambaa mno kwenye mitandao ya kijamii likiambatana na nukuu zilizotungwa na watu mbalimbali zenye utani, dhihaka na kuamsha ari ya kuwajibika kwa wazazi.

Kutokusameheana kunaweza kuwa chanzo cha kuvunja uhusiano wa kidugu, kikazi na wa ndoa. Lakini pia kunasababisha maradhi. Samehe usimbebe mtu kwenye fikra na moyoni kwako kwani unayeumia ni wewe. PICHA: MTANDAO.

Utani huu binafsi naufurahia kwa sababu nautazama kama njia nzuri ambayo jamii imeona kuitumia ili kukumbushana kwenye kuwajibika katika masuala ya familia na malezi. Kwa wale waliofanikiwa kuwapeleka watoto wao shule wameshinda kwenye mitandao ya kijamii wakitu-postia picha zenye kufurahia mtoto kurudi shule.

Ndugu zangu mwaka bado mbichi sana ndiyo kwanza leo ni siku ya 13 au wiki mbili tangu uanze baadhi yetu wapo kwenye kujizatiti kuweka mipango ya mwaka mzima na namna ya kuitimiza huku wengine wana maruweruwe ya kutokujua wanatoka vipi na wanakwendaje.

Kwa wale ambao bado wapo kwenye maruweruwe wamekumbushwa na mwandishi wa makala wa siku nyingi Maggid Mjengwa kwenye ukurasa wake wa facebook ameweka makala fupi yenye kichwa cha habari kisemacho “Mwaka mpya ni kama noti ya elfu kumi ya bongo, ukiichenji tu, inapukutika”.

Akiweka msisitizo mkubwa kwenye makala hiyo Mjengwa anasema;” Kesho ni siku ya 10 ya mwaka mpya. Na mwaka ulivyo ni kama noti ya 10,000 ya Bongo. ukiichenji tu, utashangaa inavyopukutika.Ukae sasa ukijua, kuwa kesho ndio Januari 10.

Hivyo, mwaka mpya wa 2019, kama noti tumeshauchenji. Subiri sasa uone siku, wiki na miezi inavyopukitika. Fumba na kufumbua utasikia tumeshaingia Aprili, Pasaka na kisha, kinaitishwa mapema, kikao cha Bunge cha Bajeti ya Serikali…. Ukitoka hapo utafikiri mwaka unateremsha milima ya Kitonga”.

Msingi unawekwa kwenye kujipanga na kuweka maazimio na malengo kwa wakati na muda,usije ukaishia kupanga tu huku siku,wiki,miezi ikiwa inakwenda kwa kasi kuliko ya kutimiza malengo yako. Nikusisitize muda haukusubiri, unateremka kwa kasi kubwa, usipokimbizana nao utakuacha ukishangaa mwaka umeishaje.

Wiki iliyopita kwenye safu hii niliandika kuhusu tatizo la kuahirisha ahirisha maazimio yako kunavyosababisha ushindwe kutimiza yale maazimio, mipango na malengo uliyoyakusudia, huku nikiwa nimepanga mwezi huu wote niwe nawakumbusha masuala mbalimbali yanayokwamisha wengi kutimiza yale waliyoyakusudia.

Licha ya kwamba katika kutimiza malengo kuna vikwazo vingi kuna vinavyoweza kuepukika na vingine visivyowezekana hilo halisababishi kumfanya mtu kutopanga kufanya chochote bora upange ushindwe kuliko kutokupanga.

Wakati nikiwa nasoma machapisho mbalimbali katika kufanya utafiti ili nipate jambo la kuandika wiki hii niliamua kushirikisha wadau wangu kama wana wazo lolote la karibu, kwenye kujadiliana mmojawapo akaniambia,”Dokta andika kuhusu msamaha, watu wanashindwa kusamehe ndiyo maana wanakwama kwenye vitu vingi”.

Wala sikujiuliza mara mbili, nilimkubalia hapo hapo huku nami nikilitazama kwa ukubwa zaidi kwa kujiuliza maswali kadhaa haraka haraka, Je kusamehe kuna mchango wowote katika kutimiza malengo na maazimio yako?

Kuna athari zozote zitakazojitokeza endapo unapovuka mwaka mwingine huku ukiwa na vinyongo vya mwaka uliopita? Je kutokusamehe ni maradhi au tabia ya mtu mmoja mmoja?.

Maswali hayo matatu nitayatumia kujengea msingi wa makala hii na nitajadili kwa kina kusamehe na mafaniko ya mtu.Wengi wetu tushawahi kusikia mara nyingi tu kuhusu kusamehe na kusahau.Kusamehe ni kuamua kutomchukulia mtu hatua na kuondoa kinyongo moyoni mwako kutokana na jambo baya ulilofanyiwa na mtu huyo.

Kusamehe kuna manufaa zaidi kwa yule aliyekosewa pale anapoombwa msamaha hupata faraja ya nafsi kwa kile kilichotokea. Ikumbukwe katika maisha mwanadamu ameumbwa akiwa na upungufu hakuna mkamilifu katika dunia hii, hivyo kukoseana ni jambo ambalo halipingiki pia ni vigumu mno kusema mwanadamu ataishi bila kumkosea mwingine.

Watu wengi hatulijui hili basi mtu akikosea basi unamjengea visasi na kujikuta tunapoteza muda mwingi katika kushughulika na visasi na kuacha kushughulika na mambo yanayoweza kutupatia mafanikio.

Pia kwanini unatumia kufikiri tu kuhusu mtu aliyekuumiza au kukukwaza? Na wangapi wanaweza kuhimili kuumizwa au kukwaza na wenzao na kuendelea shughuli zao pasipo kutetereka.Ingawa si rahisi kuhimili maumivu na si kila mtu anaweza hilo.

Kibaya zaidi unapoendelea kushikilia maumivu uliyoyapata huwa yanajikusanya nafsini mwako huku yakitengeneza sumu kali. Katika hali hiyo usipo msamehe mtu aliyekusababishia maumivu hayo utabaki kuumia tu na kushindwa kuendelea mbele na maisha yako.

Vilevile kuweka visasi muda mrefu hudumaza nafsi.Kudumaa kwa nafsi husababisha kutokuwa imara pale inapotakiwa kufanya maamuzi linapoibuka jambo lolote.

Nikufafanulie kidogo, mwanadamu akipata jambo lolote ambalo linahitaji maamuzi kitu cha kwanza huiuliza nafsi yake ili iweze kuamua jambo hilo. Sasa pale inapokutana na nafsi iliyoumizwa kwa kiasi kikubwa inasababisha kupunguza uwezo wa kufikiri vitu vipya, chuki, na visasi.

Hata hivyo, pamoja na kupunguza uwezo wa kufikiri kunakuzamisha katika dimbwi kubwa la mawazo, yanayokupeleka kujikita katika tabia zisizo za kimaadili kwa mfano ulevi, wizi na uhalifu. Kitendo cha kuangukia katika tabia zisizo kimaadili huwa hakitokei bahati mbaya.

Ni baada ya nafsi kushindwa maamuzi mazuri ya juu ya cha kufanya badala yake maamuzi mabaya hutawala wakati unafanya wewe mwenyewe hudhani kuwa unachokifanya ni mbadala wa kushindwa kwa jambo la msingi,kumbe wapi,nafsi ipo nyang’anyang’a.

Hivyo nafsi ikiwa imejaa visasi, maumivu, majeraha na uchungu huwa inashindwa kutoa maamuzi mazuri sababu huwa dhaifu,udhaifu huo wa nafsi huleta udhaifu kwenye kuamua mambo uliyopanga kufanya.

Kushindwa kusamehe ukiwa umekosea huwa ni maradhi ya nafsi ambapo mtu anayeshindwa kusamehe huwa hajijui kama ana hayo maradhi ambayo kwa kiasi kikubwa nafsi yake inakuwa imekongoloka haipo imara tena.

Tafiti ambazo zimewahi kufanywa na wanasaikolojia miaka ya nyuma, waligundua ya kwamba watu wengi hawana maendeleo yao binafsi kwa sababu hawatambui nguvu ya msamaha ilivyo na nguvu katika safari ya mafanikio.

Tafiti hizo hizo zinaendelea kusema watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu wamebeba mizigo mizito ndani nafsi zao.Sasa basi,unaposamehe hushusha mizigo hiyo chini na nafsi inaimarika huwa na nguvu zaidi kwenye maamuzi katika jambo lolote lililopo mbele yako.

Kwa mantiki hiyo kusamehe si tabia bali ni uimara wa nafsi katika kutafakari,kuamua, na kuona faida na hasara juu ya maumivu,uchungu na visasi alivyofanyiwa.

Na uimara na udhaifu wa nafsi huchangiwa vikwazo vya nje na ndani pia hutegemeana zaidi na historia ya mtu kwenye makuzi na malezi aliyopitia.

Kwenye ukuaji binadamu anapitia hatua mbalimbali kitabia na kiakili, kwenye tabia hutengenezwa kila haina ya tabia akiwa utotoni ukubwani tunayoyaona yanakuwa ni matokeo tu ya hujenzi wa tabia kutoka kwa wazazi na walezi waliomkuza.

Kwa kuwa mwaka ni mpya basi achilia, sahau , samehe yale yote ambayo ni machungu, makwazo, visasi na maumivu kwani havitokusaidia bali vitanyong’onyeza nafsi yako na kushindwa kuipa nafasi ya kukua na kuimarika ipasavyo.
Mwaka mpya na mambo mapya, jifunze kusamehe.

Habari Kubwa