Kutojua kuswaki kikamilifu kunavyotishia kuangamiza wengi

22Oct 2017
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Kutojua kuswaki kikamilifu kunavyotishia kuangamiza wengi

UNA matatizo ya kuumwa meno ambayo pia hutoboka? Wataalamu wanakushauri usikimbilie kutaka kuziba angalia jinsi unavyoyasafisha kinywa chako, kama hujui muulize mtaalamu wa kinywa na meno namna ya kuswaki.

Hii ni kwa sababu magonjwa mengi ya meno yanatokana na usafishaji duni wa kinywa, lakini pia tiba ya meno kwa kuziba na ‘gundi au sementi’ zenye zebaki ni hatari kwa mgonjwa tena ni kitisho kwa watoto ambao hawajazaliwa, wachanga pamoja na wadogo.

Maradhi ya meno yanayowasumbua watu wengi ni matokeo ya elimu duni kuhusu namna ya kutunza kinywa ikiwamo kusafisha au kupiga mswaki na ulaji vyakula vyenye sukari nyingi .

Yote haya yamefanya kuwe na ongezeko la matatizo ya kinywa na wagonjwa wa meno, anasema Mtaalamu wa Kinywa na Meno, Dk. Emilton Ndanshau.

Anaeleza kuwa magonjwa hayo hutegemea na hatua ya ugonjwa wa jino, baadhi hufika hospitalini likiwa limeoza, limetoboka na hata kuvunjika na kwamba zama hizi rika zote zinaathiriwa na tatizo hili.

Aidha, pamoja na ongezeko hilo idadi ya wanaokwenda hospitalini kupewa tiba ni ndogo na hata wanaofika wamechelewa na kusababisha meno kung’olewa.

Baadhi ya tiba ambazo hutolewa hospitalini ni pamoja na kuyaziba badala ya kuyang’oa na kwamba dawa zinazotumiwa ni ‘composite resin, glass ionomer na dental amalgam’

Kati ya dawa hizo ambazo hutumika mara kwa mara zina madini ya zebaki au mercury, ambayo wataalam wa tiba wanaeleza kuwa yana madhara hasa kwenye ubongo, mfumo wa fahamu na wa uzazi ikiwamo kuharibu mimba.

KUZUIA ZEBAKI AFRIKA

Oktoba 13 kila mwaka ni siku Afrika ya kuhimiza tiba ya meno bila dawa zenye zebaki.

Asasi za kiraia zaidi ya 40 nchini huungana na mataifa mengine ya Afrika kuhimiza tiba ya meno isiyo na dawa ya zebaki ili kulinda afya za wajawazito pamoja na watoto na kwamba kuendelea kwa matumizi hayo kunaathiri ubongo wa mtoto tangu akiwa tumboni na kumpunguzia uwezo wa kufikiri.

Ofisa Progarmu Mwandamizi wa Shirika la Maendeleo na Mazingira na kudhibiti Kemikali (Agenda), Dorah Swai, akizungumza kwenye kongamano jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, anasema siku hiyo inalenga kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya zebaki.

Anasema matumizi mbadala ya kutibu jino kwa dawa isiyo na zebaki yatasaidia kuondoa madhara ya dawa hiyo inayosababisha mwili kutetemeka, kiharusi, uoni hafifu, watoto kuzaliwa na ulemavu, kuharibu mbegu za uzazi, maumivu ya kichwa pamoja na uchovu.

“Kinamama walio katika umri wa kuzaa ni kundi lililo hatarini zaidi pamoja na watoto wadogo ambao wengi wao huathrika tangu wakiwa tumboni, iwapo mama ameathiriwa na zebaki mwilini,” anasema Swai.

“Agosti mwaka huu mkataba wa wa usitishwaji matumizi ya zebaki kimataifa umeridhiwa na nchi 50 na kupitishwa na mkutano wa kidiplomasia wa kimataifa jijini Minamata nchini Japan.”

ELIMU DUNI UTUNZAJI MENO

Pamoja na kuwa tatizo la meno husumbua wengi kama yalivyo magonjwa mengine, wataalam wanaeleza kuwa elimu duni kuhusu utunzaji kinywa na meno ni tatizo Tanzania.

Dk. Ndanshau Anasema elimu kuhusu utunzaji wa kinywa na namna ya kusafisha meno kwa mswaki na njia nyingine za asili kama vile vijiti kwa baadhi ya jamii, hazifanyiki kwa usahihi.

Anasema upigaji wa mswaki na namna ya kutoa vyakula ambavyo vimesalia kwenye meno baada ya kula, ni tatizo.

“Ukishakula wengi wetu tunapenda kutumia vijiti au ‘toothpick’ lakini tunatumia isivyo, kijiti ni kinene unatakiwa kukipasua view viwili na utapatikana wembamba ambao ukiingiza kijiti kitaweza kutokeza hadi mwisho, kikiwa kinene kitafanya uchafu ulio katikati ya jino usitoke,” anaeleza.

MENO KUPOTEZA UIMARA

Sababu za meno kuwa dhaifu ni ulaji vyakula vyenye sukari zaidi kama pipi, ice cream, keki na biskuti vinavyosababisha kubakiza uchafu katikati ya meno hivyo kuwa kisababishi cha meno kukosa uimara, kuoza na kutoboka.

Pia kutosafisha kinywa ipasavyo na aina ya miswaki au vifaa vinavyotumiwa kusafisha meno.

Anasema elimu ikitolewa kuanzia shule za msingi, itawajengea uelewa zaidi watoto na kufahamu afya ya kinywa na kwamba watoto ndiyo waathiriwa wakubwa kwani hula kila mara bila mpangilio na kupendelea vyakula vilivyo na sukari zaidi.

Hata hivyo, hawafamu namna ya kuswaki na kupiga mswaki mara ngapi kwa siku.

Anasema kitaalamu mtu anatakiwa kuswaki mara mbili kwa siku, ili kujiwekea uhakika wa afya ya kinywa na kulinda meno.

MKATABA WA KIMATAIFA
Septemba 25 mwaka huu, mkutano wa kwanza wa Wanachama wa Mkataba wa Minamata wa Zebaki (First Conference of the Parties (COP 1) uliliridhiwa jijini Geneva nchini Uswisi, ukishirikisha mataifa zaidi ya 130.

Lengo la mkutano ni kujadili changamoto za kiulimwengu za uchafuzi wa mazingira na afya ya binadamu unaotokana na zebaki.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) Ibrahim Thiaw, anasema uzinduzi wa COP 1, ni nafasi ya kufanya kazi kuelekea kwenye umakini wa ubebaji, uhifadhi na utupaji wa taka na bidhaa, usitishaji na matumizi yote ya zebaki.

Aidha, anataja haja ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa na ulinzi wa kisheria wanaouhitaji na kuwaelewesha madhara ya kuingiliwa na taka za zebaki kwa jamii yenye uwezekano wa kuathirika zaidi, wanawake na watoto.

Thiaw anasema Shirika la Afya Duniani (WHO) limeainisha kuwa zebaki ni kati ya kemikali 10 au kundi la kemikali zenye athari kubwa kwa biandamu.

“Tafiti zinaonyesha kuwa watoto katika nchi za Brazili, Canada, China, Columbia na Greenland wanaathirika kwa kula samaki wenye zebaki. Inaathiri maisha ya kila siku ya watoto hao na familia zao, kwa miaka ijayo zebaki itakuwa na athari za muda mrefu kijamii na kiuchumi kwa nchi zao, hii ndiyo sababu ya kuwapo Mkataba wa Minamata.”

“Ni mkataba wa kwanza wa kimataifa uhaohusu mazingira na afya kwa kipindi cha muongo mmoja ni kwa sababu ni moja ya eneo muhimu la kufikia Agenda ya Maendeleo Endelevu ifikapo 2030,” anasisitiza.

ATHARI

Zebaki inaathiri mfumo wa fahamu na ina uwezo wa kufanya hivyo popote. Madini haya huingia kwenye mazingira kutokana na shughuli za binadamu kama kilimo, ufugaji au tiba na inaingia katika mfumo wa vyakula (food chain), ikiliwa inajikusanya mwilini na inaweza kuharibu ubongo, moyo, figo, mapafu na mfumo wa kinga kwa watu wa rika zote.

Zebaki ni mbaya zaidi kwa mimba na watoto wadogo ambao mfumo wao wa fahamu unakua na kwamba unapotokea uharibifu kwenye ubongo hautibiki. Hakuna kiwango salama cha madini ya zebaki kwa binadamu na madhara yanaweza kutokana na kiwango kidogo cha zebaki.

Habari Kubwa