Kutoka kuuza lita moja ya asali hadi kusafirisha tani kadhaa nje

27Aug 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Kutoka kuuza lita moja ya asali hadi kusafirisha tani kadhaa nje

HATA mbuyu ulianza kama mchicha, ndivyo imeweza kuwa kwa Esther Lema, ambaye anafanya biashara ya kuuza asali maeneo mbalimbali nje na ndani ya nchi, huku akimiliki mizinga 600 ya nyuki mkoani Tabora.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Esther mwenye miaka 33, anasema, alianza biashara hiyo kwa mtaji wa Shilingi 40,000, kwa kununua lita tano za asali na kutembeza mitaani na sasa amefikisha mtaji wa Shilingi 6,000,000.

Lakini leo anazungumzia biashara kubwa ya asili inayovuka mipaka kutoka Tanzania hadi Somalia na ndoto yake ni kulitawala soko la Afrika Mashariki kuanzia Dar hadi Nairobi na pia Congo.

Katika mazungumzo yake na gazeti hilo, anasema alianza biashara hiyo mwaka 2019 baada ya kuacha kazi ya kushona nguo aliyoifanya kwa miaka sita jijini Dar es Salaam na kuongeza: "Niliamua kubadili kazi baada ya kuona ushonaji unachelewesha kufikia malengo ya kuinua kipato changu, ndipo nikajaribu biashara ya kuuza asali nikianzia na dumu la lita tano," anasema Esther.

Anafafanua kuwa alinunua dumu la asali la lita tano kwa Sh. 40,000 na kuigawa katika chupa za lita moja, ambapo kila lita aliuza kwa Shilingi 12,000, na kwamba aliuza kwa siku moja na kuimaliza.

"Nilinunua nyingine ya lita tano nayo ikaisha, ikabidi ninunue dumu la lita 20 ambalo nilikaa nalo kwa muda wa siku mbili nalo likaisha, nikaongeza jingine nikaendelea kufanya hivyo kwa miezi nane," anasema.

Esther anasema, baada ya kuona biashara ya asali inazidi 'kuchanganya', akapata wazo la kwenda mwenyewe Tabora kuifuata huko na kuachana na mtindo wa kuagiza watu wamletee na kuongeza:

"Niliamua kusafiri kwa treni hadi Malongwe mkoani Tabora ambako asali inapatikana kwa wingi, nilikuwa sipajui, sina ndugu, lakini nikaamua kwenda, ili nitimize lengo la kufanya biashara."

Anasema, akiwa ndani ya treni, alikutana na mzee mmoja na kumweleza kile kinachompeleka huko na kumwelekeza sehemu ambayo asali inapatikana kwa wingi, ambapo walishuka naye.

Licha ya kuhofia usalama wangu, kwani tulishuka saa tisa za usiku kwenda nyumbani kwa mzee huyo huko Malongwe, kumbe ni mtu mwema tu, tulifika nikanunua asali madumu mawili ya lita 20 kutoka kwa watoto wake," anasema.

Akiwa na mtaji wa Shilingi 200,000, alidhani dumu la lita 20 ni Sh. 100,000, lakini anabahatika kulinunua kwa watoto hao kwa Sh. 70,000 kila moja na hivyo kubakiwa na Sh. 60,000, na kurudi Dar es Salaam kuendelea kuuza na kusafiri hadi Malongwe kununua nyingine kila ilipokwisha, lakini baadaye mmoja wa watoto wa mzee huyo alimshauri amiliki pori na kuweka mizinga yake.

AMENUNUA PORI

Anasema, alinunua pori lenye zaidi ya eka 10 kwa Sh. 500,000 na kuanza na mizinga 100, na kwamba kadri mambo yalivyochanganya, aliongeza mingine na sasa ana jumla ya mizinga 610.

"Baada ya kuwa na mizinga yangu, niliachana na mtindo wa kununua asali kwa wauzaji wengine, badala yake ninarina yangu mwenyewe na kwenda kuuza maeneo mbalimbali nchini," anasema.

Anasema, katika mizinga hiyo, anaweza kuvuna mapipa matano hadi sita ya asali, na kwamba uvunaji hufanyika mara mbili kwa mwaka Februari na Juni na anatumia wafanyakazi wake watano aliowaajiri kwa kazi hiyo.

"Biashara ya asali imebadili maisha yangu, kutoka mtaji wa Sh.40,000 hadi kufikia Sh. milioni sita, pia nimefanikiwa kujenga nyumba Mbezi Makabe na ninasomesha watoto wangu wawili kwenye shule za kulipia,"anasema.

MALENGO YAKE

Esther anataja baadhi ya malengo yake kuwa ni kuongeza mizinga hadi kufikia 2,000, kuwa na duka la kuuza asili Afrika Mashariki na kuwa msambazaji bidhaa hiyo kwa wateja wengi eneo hilo.

"Ninatarajia kupanua soko zaidi kwani nimekuwa nikiuza asali Dar es Salaam Arusha na Nairobi Kenya na sasa nimepata wateja kutoka Somalia, hivyo sina budi kupanua zaidi biashara yangu na kuvuka mipaka ya Afrika Mashariki," anasema.

Aidha anasema, anajipanga kuhamasisha mabinti wengine kufanya biashara ya asali kwa kuwa inalipa na kwamba kuna kipindi inaadimika ambapo dumu la lita 20 linanunuliwa kwa Sh. 160,000 hadi 170,000.

"Msimu unapokuwa mzuri, dumu la lita 20 za asali huuzwa kati ya Sh. 80,000 hadi 100,000, ikiadimika ndipo bei inapanda hadi kufikia 170,000, hivyo mtu akiwa na mizinga kidogo, inaweza kubadili maisha yake kwa kuiuza kwa faida kubwa hasa wakati inapoadimika," anasema.