Kutoka SUK hadi siasa za chuki, uhasama

25May 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Kutoka SUK hadi siasa za chuki, uhasama

WAHENGA hawakukosea waliosema kuwa umoja ni nguvu utengano ni dhaifu, wakimaanisha kuwa bila ya umoja miongoni mwa wanajamii huenda kukatokea athari mbalimbali ikiwamo za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Baadhi ya wananchi wa Zanzibari wakiwa katika foleni kwa ajili ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana. PICHA: MAKTABA

Umoja unaohitajika kwa Wazanzibar sasa umeondoka kutokana na mihemko ya kisiasa, hali iliyosababisha ubaguzi miongoni mwao.

Ubaguzi huo umezidi kushika kasi baada ya tume ya uchaguzi Zanzibar kufuta uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana na kufanya uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu ambao chama kikuu cha upinzani Chama Cha Wananchi (CUF), hakikuunga mkono uamuzi huo wa tume na kususia uchaguzi huo.

Wanaharakati mbalimbali walitegemea kuwa siasa za chuki na uhasama zimeondoka Zanzibar kutokana na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini hali ni tofauti na mategemeo ya wanaharakati.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na ule wa wa marudio uliofanyika Machi 20, kumekuwapo na hali ya ubaguzi katika visiwa vya Unguja na Pemba na kufikia wananchi wa visiwa hivyo kubaguana mfano kunyimana huduma muhimu za kijamii.

Hivi karibuni kumeripotiwa kesi nyingi za ubaguzi hasa kisiwani Pemba jambo ambalo limezusha mjadala mkubwa kwa wakazi wa Zanzibar.

Kutokana na CUF kususia uchaguzi wa marudio kwa madai kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, ulikuwa huru na haki, Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad aliwataka wafuasi wake pamoja na wananchi wa Zanzibar kutotoa ushirikiano wowote kwa serikali iliyopo madarakani kwa madai kuwa serikali hiyo sio halali.

Maalim Seif aliwasisitiza wafuasi na wananchi hao kuwadharau viongozi wa Serikali waliyopo madarakani kutokana na kubaka demokrasia ya Zanzibar.

Tangu kiongozi huyo wa kisiasa ambaye anaushawishi mkubwa Zanzibar hasa kwa wafuasi wa CUF kutoa agizo hilo, tayari wafuasi wa CUF wameanza kutekeleza agizo hilo kwa vitendo kuigomea Serikali.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Uvuvi na Mifugo, Hamad Rashid Mohammed, alikwenda katika diko la wavuvi mtoni kukutana na wavuvi na kujadili changamoto zinazowakabili, lakini kwa kuwa wavuvi wengi katika eneo hilo ni wafuasi wa CUF waligoma kuonana na waziri huyo.

Wavuvi hao zaidi ya 80 walikataa kukaa pamoja na waziri huyo ili kujadili changamoto mbalimbali za uvuvi na jinsi ya kuzitafutia ufumbuzi.

Wakizungumza na Mwandishi wa makala hii, wavuvi hao walisema wamegoma kuzungumza na waziri huyo, kutokana na walichokidai aliwasaliti Wazanzibar kwa kushiriki uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu na kubaka demokrasia ya Zanzibar.

“Hatujataka kukutana naye hatuna habari naye kwa sababu hatufai alitusaliti na kutugeuka kaifilisi Katiba inayopendekezwa na uchaguzi wa Zanzibar na viongozi wote wa serikali hatutokua na masharikiano nao na sisi tumeamua kumfanyia dharau,” alisema Haji Salum Bakari mvuvi wa eneo hilo.

Katibu wa jumuiya ya wavuvi wa Kojani, Omar Muhammed Ali, alisema Hamad Rashid, alimwita na kumwomba wafanyekazi kwa pamoja na awakusanyie wavuvi ili kuzungumza nao changamoto zinazowakabili na ndipo alipoamua kuwakusanya wavuvi hao kwa sababu aliona ni jambo zuri.

“Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu niliona ni bora tushirikiane kwa pamoja ili wavuvi tuweze kueleza changamoto zinazotukabili maana tunakabiliwa na changamoto nyingi,” anasema Omar.

Anaeleza kuwa aliwapa taarifa baadhi ya manahodha wa vyombo vikubwa na vidogo vya uvuvi kuhusu ujio wa waziri huyo na walilikubali, lakini anashangaa wavuvi wote waligeuka na kukataa kataka kuzungumza na waziri wa uvuvi kwa madai ya kuwa hawamtambui.

Anasema inawezekana baadhi ya watu wamejitokeza na kuwajaza chochoko wavuvi hao ya kukataa kuzungumza na waziri huyo, bila ya kutoa taarifa.

“Nimwombe waziri achukulie hizo ni changamoto asivunjike moyo na niwaombe wavuvi hizi ni kazi za kawaida ni vyema kushirikiana ili kufikia malengo katika sekta ya uvuvi,” anasema.

Waziri Hamad Rashid alilazimika kuondoka bila ya kuzungumza chochote na wavuvi hao baada ya kugoma.
Hata hivyo, alisema wakati wa siasa za chuki na uhasama umepitwa na wakati na sasa kazi iliyobaki ni kushirikiana kwa pamoja katika kuliletea taifa maendeleo.

Alirusha kijembe kwa CUF akieleza kuwa kama ni kweli wavuvi hao wanatekeleza agizo la Katibu Mkuu wa CUF kuigomea Serikali iliyopo madarakani alihoji kwa nini asianze yeye ambaye ndio kiongozi mkuu katika chama hicho kugomea mali za serikali iliyopo madarakani ambayo anadai haitambui.

“Mimi naona baadhi ya wananchi wanafuata mkumbo na kama wanadai mimi ni msaliti niwaambie tu mimi sio msaliti na nilitaka kuonana nao, kujadili jinsi gani ya kutatua changamoto zinazowakabili ili kupata maendeleo, lakini kama maendeleo hawayataki Serikali haitosita kutoa maendeleo hayo bila ya ubaguzi,”alisema Hamad.

alihoji, wavuvi au wafuasi wa CUF watashindana na Serikali hadi lini wakati wenyewe walisusia uchaguzi mkuu wa marudio kwani kila chama kilikua na haki ya kushiriki uchaguzi huo na lengo la kuanzishwa kwa chama cha siasa ni kushika dola.

Wakati hayo na mengine mengi yakiwa yanaendelea visiwani hapa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kuwasimamisha kazi mara moja watumishi wa umma wanaoonekana kuchukua mawazo ya baadhi ya viongozi wa kisiasa wakati wakitekeleza majukumu yao.

alisema haiwezekani kwa mtumishi wa umma akaachwa aendelee kufanya anavyotaka hasa katika kuwatumikia wananchi kwa njia za unyanyasaji au ubaguzi, huku akiendelea kula mshahara wa Serikali.

Balozi Seif alisema taratibu za kuwafukuza watumishi waliosimamishwa na watakaosimamishwa kazi kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za utumishi Serikalini zitafuata hapo baadaye kwa wale watakaoshindwa kubadilika kutokana na vitendo vyao vilivyo nje ya maadili yao ya kazi.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haiwezi kuvumilia maovu ya watu na hata mtu mmoja atakayoyafanya dhidi ya Serikali na wananchi akiyatolea mfano matendo ya kutengwa kwa baadhi ya wananchi katika kupatiwa huduma muhimu za kijamii kama usafiri wa baharini, barabarani na zile za kibiashara kwa kuuza au kununua bidhaa.

Hata hivyo, alisema kwamba Serikali inaelewa kwamba hali ya Pemba bado si nzuri, hivyo kupitia vyombo vya dola italazimika kuimarisha zaidi ulinzi ili kuwapa fursa pana wananchi na uwezo wa kuishi kwa amani, utulivu na upendo miongoni mwao.

Balozi Seif alisema cheche za shari na uvunjifu wa amani zinazofanywa kisiwani Pemba zina dhamira ya wazi ya kutaka jamii ya Kimataifa iione Zanzibar iko katika vurugu kubwa zilizosababishwa na matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, uliofutwa kutokana na sababu mbalimbali.

Habari Kubwa