Kuupuuza UVIKO-19 sasa kwaiibua CHAKUA

26Aug 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Kuupuuza UVIKO-19 sasa kwaiibua CHAKUA
  • *Wajitosa ndani ya vyombo vya usafiri, stendi

VITA dhidi ya UVIKO-19 imepata nguvu mpya baada ya Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA) kusambaza maofisa wake kuhamasisha abiria ndani ya mabasi kuchukua tahadhari.

Katibu wa CHAKUA kanda ya kaskazini, Godwin Mpinga, akitoa elimu ya kujikinga na UVIKO-19 kwa abiria ndani ya basi, jijini Arusha. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Hatua hiyo inafuatia hali ya kusuasua kujihadhari na ugonjwa huo inayoonekana kwenye maeneo na mikoa mingi nchini.

Wahamasishaji hao, wapo mikoa yote ya Bara wakiendelea kutoa elimu ndani ya daladala, mabasi makubwa na kwenye vituo vya mabasi hasa vikubwa.

Msemaji wa CHAKUA, Solomon Nkiggi, anasema, wanahimiza abiria na wananchi maeneo hayo kuvaa barakoa, kunawa mara kwa mara, kutumia vitakasa mikono, lakini pia kuepuka kula ovyo bila kunawa na kuzingatia maelekezo ya mwongozo wa afya kujikinga na corona.

"CHAKUA tuna nafasi ya kuhakikisha abiria wanakuwa salama wanapoanza safari hadi wanapofika mwisho, hivyo tunashiriki kikamilifu kutoa elimu ya kujikinga na corona," anasema Nkiggi.

Kwa mujibu wa Nkiggi, wanachukua hatua hiyo, baada ya kubaini kuwa tangu mwongozo utolewe, abiria wengi na hata makondakta na madereva hawajabadilika, hali inayoweza kuchangia kuenea kwa ugonjwa huo.

"Maelekezo ya serikali yanaagiza wasafiri kuwekewa miundombinu ya kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kabla ya kuingia kwenye vyombo vya usafiri, lakini kuna sehemu mambo hayo hayatekelezwi," anasema.

Msemaji huyo anaongeza kuwa, wamiliki wa vyombo vya usafiri wanaelekezwa kuweka vitakasa mikono katika vyombo hivyo, kwa usalama wa afya za abiria.

Aidha, CHAKUA mbali na kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo, anasema, chama hicho kinahimiza viongozi wake na wanachama kupata chanjo ya corona kwa ajili ya usalama wa afya zao na wa abiria pia.

OMBI KWA WIZARA

Katibu wa CHAKUA kanda ya kaskazini, Godwin Mpinga, anaiomba Wizara ya Afya, halmashauri na wadau wengine, kusambaza vifaa vya kunawia mikono kwenye vituo vya mabasi vinavyozingatia mahitaji ya wenye ulemavu.

Anasema, katika kanda hiyo, serikali imeweka huduma hizo katika stendi kuu za mabasi, ili kukinga wananchi dhidi ya corona, lakini inahitajika zaidi kuwakumbuka wenye uhitaji maalumu.

"Kwenye stendi kuu ya mabasi Arusha kuna matangi madogo ya maji na sabuni, lakini wakati maji yanaisha hayawekwi mengine kwa wakati. Lakini pia hakuna vifaa ambavyo ni rafiki kwa walemavu," anaongeza.

Anasema, kuna haja ya kuweka miundombinu ambayo ni rafiki kwa kundi hilo ambalo mara nyingi halifikiwi na huduma hizo kutokana na kukosekana miundombinu rafiki.

"Kwa mfano tangi la maji na sabuni vimewekwa juu kwenye ngazi maalum ambako mlemavu hawezi kufikia. Tunashauri miundombinu hiyo iwe rafiki kwa kundi hilo ili kila mmoja ahudumiwe," anasema.

KUSIMAMIA MWONGOZO

Julai mwaka huu, Wizara ya Afya, ilieleza kuwa wagonjwa wa UVIKO -19 walifikia 682 na kutoa mwongozo mpya wa kudhibiti ugonjwa huo.

Takwimu hizo zilitolewa na Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, zilifuatiwa na maelekezo ya Katibu Mkuu, Profesa Abel Makubi, akatoa mwongozo mpya unaoelekeza namna ya kujikinga na maradhi hayo.

Mwongozo huo unaainisha kuepuka misongamano katika shughuli za kijamii, ndani ya vyombo vya usafiri, kwenye vituo vya mabasi ya mijini na mikoani.

Aidha, ndani ya daladala abiria wakae kulingana na idadi ya viti ‘level seat’, lakini bajaj na bodaboda madereva na wateja wao wavae barakoa na kuepuka msongamano wa abiria, kwa kuwa ugonjwa huo unaweza kusambazwa kupitia vyombo vya usafiri.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa mwongozo huo, bado hakujawa na mabadiliko kwenye baadhi ya vyombo hivyo na Dar es Salaam hali ni mbaya zaidi, kwa vile maagizo hayo yanapuuzwa kila mahali isipokuwa hospitalini, ndani ya mwendokasi na ofisi zinazosimamia na kutekeleza mwongozo huo.

KUDHARAU UGONJWA

Mkazi wa jijini Dar es Salaam anayejitambulisha kwa jina la Shaban Bata, anasema, licha ya maelekezo ya serikali ya kujikinga na ugonjwa huo ndani ya vyombo vya usafiri, baadhi ya abiria, makondakta na madereva ni wabishi.

"Tunaelekezwa kwamba, kila abiria anayeingia kwenye chombo cha usafiri wa umma lazima avae barakoa, wengine hawafanyi hivyo, wanadai kwamba hakuna ugonjwa, corona ni ugonjwa wa wazee , matajiri au kama umeandikiwa kufa utakufa tu…" anasema Bata.

Anasema, daladala zinatakiwa kupakiza abiria 'level seat' na kuvaa barakoa, na kwamba hilo nalo halizingatiwi, badala yake abiria wenyewe, makondakta na madereva hawachukui tahadhari na msongamano uko pale pale.

"Binafsi nimefuatilia sana mwongozo huo, unaelekeza pia bodaboda wasibebe mishikaki na kuvaa barakoa lakini hilo nalo halifanyiki…," anasema.

Anaongeza kuwa, stendi kunatakiwa kuwe na ujumbe wa kuelimisha wasafiri mara kwa mara kupitia vipaza sauti na wanapokuwa safarini, madereva na wahudumu wa vyombo vya usafiri wahakikishe ujumbe wa kuelimisha unatolewa katika chombo mara kwa mara, yote hayajaonekana.

"Ukienda kwenye vituo vya daladala utakutana na msongamano nje na ndani ya mabasi hayo na muziki unaosikika ni bongofleva na singeli bila ujumbe wa kuhamasisha kuchukua hadhari.