Kuzoea kwetu yanayokosewa kunayahalalisha

14Feb 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Kuzoea kwetu yanayokosewa kunayahalalisha

JAMII ikipuuza kukomesha mambo mabaya, inayazoea, inayahalalisha na kuyafanya sehemu ya maisha yake. Yakishazoeleka hivyo, akijitokeza mwana jamii akataka kuyabadili, huyu ndiye huonekana kukosea!

WAZIRI WA FEDHA DK MPANGO

Haishangazi leo serikali kulaumiwa kuzuia vikao mahotelini kuokoa fedha yake wakati kumbe mahoteli yalikuwa yakifaidika kwa vikao hivyo!

kuyazoea, kuyahalalisha na kuyafanya yawe utaratibu rasmi na matokeo yake kuyafanya yawe utamaduni wetu au utaratibu wetu wa maisha. Nchi imejaa rushwa, wizi wa fedha ya umma na matumizi mabaya ya fedha.

Tumelazimishwa kuyazoea mpaka yamekuwa kama mambo yenye kumjengea mtu sifa nzuri kwamba ana akili sana, anajua kutumia ofisi au nafasi na anajua kupanga mipango huku mwadilifu anazungumziwa kinyume cha sifa hizo!

Tumejilazimisha mpaka imetuingia akilini kwamba upinzani wa kisiasa ni uadui na wapinzani, maadui wakubwa, wa chama kinachoongoza nchi ni watu wa daraja la chini, wa kutwezwa na kudhalilishwa na vyombo vya dola, hasa polisi.

Wapinzani wanawachukulia watu wa chama tawala kuwa maadui wao wakubwa, wezi na wahujumu wa nchi hata kama hayo ni matatizo ya mtu mmoja mmoja wa itikadi yoyote.

Tunalaani mno ubaguzi wa dini, kabila na kanda lakini tunauzoea, tunaukubali na kuujenga ubaguzi wa kiitikadi! Watu gani sijui sisi! Kuna idadi kubwa ya watu hawafanyi kazi kabisa.

Kazi yao ni kuwepo ofisi za Uhamiaji, za Mamlaka ya Mapato, Mahakama, baadhi ya vituo vya polisi na kwenye stendi kuu za mabasi kutafuta watu wa kuwasaidia hili na lile kwa malipo.

Tumeacha watu hawa wazoeleke na kuifanya kama moja ya ajira wakati rasilimali watu hiyo kubwa iliyotapakaa nchi nzima ingetumika kuzalisha mazao shambani ingeongeza vya kutosha pato la serikali lakini sivyo, tumewazoea na kuwarasmisha.

Inakera mno unapofika kituo cha basi kusafiri unapozungukwa, kama mtuhumiwa aliyekamatwa, na watu wanaokutajia sehemu mbalimbali kukuuliza kama unaenda huko wakati mwenyewe unajua unaenda wapi na kwa usafiri upi.

Eti wale wanaofika nawe kwenye basi uliloliendea mwenyewe wanalipwa kwa kutofanya chochote! Hawa wapiga debe wa daladala Dar es Salaam wanafanya kazi gani huku watu wakijua waendako na wanagombania mabasi?

Tumeizoe na tumeikubali hali hiyo kuifanya iwe kama ajira rasmi. Kwa ufupi, kuyazoea na kuyakubali makosa ya kiwango chochote, kunajenga utamaduni wa kuyazoea.

Watu walipoanza kujenga mabondeni, wangekatazwa kwa robo ya nguvu iliyotumika kuwabomolea nyumba, mabondeni kusingekuwa na nyumba. Walizoeleka, wakakubalika na kufikia kuwa kama wamehalalishwa.

Wakapatiwa maji, umeme na mitaa yao ikatambulika mpaka kuwa na viongozi wao wa serikali za mitaa! Njia ya kuondoa hali hii. Kwanza, ni kufuta kwa hatua na kwa umakini yaliyozoeleka ambayo hayako sawa.

Pili kila mwenye mamlaka kwenye eneo lake azuie lolote lisilo sawa linaloanza kujengwa ili lisikue na kuzoeleka. Liwe la lugha mbovu au lolote la kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni linalokosewa kama hili dogo la vijana kuvaa suruali chini ya makalio.

Habari Kubwa