Kwa ilani hizi Tanzania isiyo na magonjwa inawezekana

16Sep 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Kwa ilani hizi Tanzania isiyo na magonjwa inawezekana
  • *Zahanati moja kwa watu 1,000…ACT.
  • *Kutibu wagonjwa KITEHEMA …SAU

WAKATI huu wa kuelekea uchaguzi mkuu mambo yanayowabana Watanzania ni pamoja na changamoto za huduma za afya, upatikanaji elimu bora na maji safi na salama. Masuala hayo yanaelezwaje ndani ya ilani za vyama?

Tiba mtandao ni miongoni mwa mikakati inayotajwa na wanasiasa kwenye kuimarisha afya. PICHA:MTANDAO.

Wagombea wanapoendelea kunadi sera na mikakati na mipango yao majukwaani, Nipashe inaangaza ahadi zilizomo kwenye ilani za vyama zenye kuboresha afya kwenye vyama vya Sauti ya Umma (SAU), CUF, ACT Wazalendo, CCM na CHADEMA.

Kwa kuwa ahadi ndani ya ilani hizo ni nyingi lakini uboreshaji wa afya ni suala la kipaumbele na kila chama kinatambua hilo.

MKAKATI WA SAU

SAU, katika ilani yake, inaitaja afya kama msingi wa kila kitu na kwamba bila afya bora mtu hakuna uzalishaji na kuchangia uchumi wa taifa.

Chama kinakiri sehemu za kupata matibabu ni chache hivyo kusababisha wananchi kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma za afya, tena hawana uhakika wa matibabu kwa vile hawana pesa.

“Upatikanaji dawa hauridhishi , kuna upungufu mkubwa wa waataalam hasa vijijini, hivyo mkakati ni kujenga zahanati kila kijiji.”

Aidha, kinakusudia kujenga kituo cha afya kila kata kitakachohudumia mama na mtoto, kujenga hospitali kila wilaya na sita za rufani kwa kila kanda zenye kutiba saratani.

SAU itatumia tiba mtandao (telemedicine) inayofanyika kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutibu na kutoa matibabu bure kwa kila mtu.

CUF IMEJIPANGAJE?

Yapo mengi ambayo ilani ya CUF inataja kuhusu afya, ukurasa wa 136 inaainisha changamoto za huduma hiyo na kueleza kuwa hospitali nyingi za serikali zina uhaba mkubwa wa wagonjwa kwa sababu hawawezi kumudu gharama za matibabu.

Ilani inasema, kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo la afya, serikali ya umoja wa kitaifa chini ya CUF itatenga asilimia 15 ya bajeti ya serikali kuboresha huduma za afya.

Miongoni mwa yatakayofanyika ni kutoa, huduma za msingi za afya bure na zitakuwa ni haki ya kila Mtanzania.Mkazo utakuwa kukinga pamoja maradhi na chanjo.

Aidha, virutubisho vitaongezwa katika vyakula hasa unga wa mahindi, wa ngano na kutoa elimu ya afya kwa kina.

“Tiba ya saratani, kisukari, figo na shinikizo la damu na baadhi ya maradhi ya kuambukiza kama vile malaria, kifua kikuu,Ukimwi na minyoo, itapatikana bure.”

Kadhalika ili kufidia pengo vyanzo vingine vitachangia huduma za afya japo serikali itatenga asilimia 15 ya bajeti.

Serikali itaboresha utaratibu wa bima ya afya, waajiri watatakiwa kuwakatia bima wafanyakazi na kuwawezesha wanachama wa mpango huo kupata huduma popote nchini.

CCM NAO VIPI?

Kuanzia ukurasa wa 124 wa ilani yake, CCM inaelezea mengi ambayo serikali imefanya miaka mitano iliyopita na kutaja mkakati mingine ya miaka mitano.

Chama kinaahidi kuweka kipaumbele sekta ya afya kwani inagusa maisha ya Watanzania na ustawi wa taifa na kwamba serikali itaendelea kutoa bure huduma za afya ya mama na mtoto, kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Jingine ni kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na pia CCM itaweka mazingira kwa sekta binafsi kujenga viwanda ili kuzalisha dawa, vitendanishi na vifaa tiba kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini ili kupunguza mzigo kwa serikali wa kuagiza bidhaa hizo nje.

Kufikia 2025 serikali itaongeza vituo vya kutolea huduma za afya kwa asilimia 20 ya vituo 8,446 vilivyopo sasa.

Kadhalika itaimarisha mifuko ya bima za afya NHIF na CHF ili kuwezesha kila mtu kuwa na bima hiyo.

CHADEMA WANA LIPI?

Ukarasa 42 wa ilani una taarifa za afya zinazosema kwa kushirikiana na sekta binafsi itawapa wananchi wote huduma bora ya afya, itajenga, kuendeleza na kutumia miundombinu ya afya kiubia baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Itaongeza udahili wa wanafunzi wa mafunzo ya watendaji wa afya ili kukidhi mahitaji ya jamii kwa mfumo wa ubia sekta binafsi na ya umma (PPP) lakini mbia mkuu ni serikali.

Inaahidi kutoa motisha kwa watendaji wa sekta ya afya kwa nafasi zao, kukuza matumizi ya teknolojia kwenye afya.

Ilani hiyo inasema, serikali ya Chadema itaimarisha Baraza la Taifa la Utafiti wa Kitabibu kwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya utafiti wa kitabibu na kuutoa kwa wakati.

Ilani inaahidi kusajili taasisi za ndani za utafiti wa kitabibu, tiba asili na tiba mbadala ili kuboresha sekta ya afya nchini.

Aidha, itahimiza sekta binafsi kuwekeza katika kuanzisha huduma ya usafiri kwa wagonjwa katika hospitali za umma, kuanzisha mchakato wa kujitathimini kwa wahudumu wa afya kwa ajili ya maisha yao viwango vya maslahi na ubora kwa ajili ya utoaji huduma.

ACT-WAZALENDO

Masuala ya afya yanatajwa kuanzia ukurasa wa 22 sehemu ya 3.2.1, chama kikiahidi kusimamia ujenzi wa zahanati mijini na vijijini kufikia lengo la kuwa na zahanati moja kwa watu 1,000.

Itajenga na kuboresha hospitali za mikoa ili ziwe za kisasa, zenye kukidhi viwango vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwekeza na kuboresha uchunguzi wa maradhi.

Itafanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya afya kwa kuwa na hospitali kubwa tatu za kanda zenye hadhi, uwezo na viwango vya kimataifa zikijengwa Mara, Ruvuma na Singida.

Sehemu ya 3.2.2. ya ilani inasema, itawezesha wafanyakazi wa afya hasa kwenye ngazi ya zahanati kutoa elimu ya afya kwa umma wakishirikiana na viongozi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji, ili kuzuia maradhi.

Habari Kubwa