Kwa nini CCM inataka Cuf iendelee kusema Zanzibar?

02Mar 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Kwa nini CCM inataka Cuf iendelee kusema Zanzibar?

HALI ya kisiasa Zanzibar imeendelea kuwa ya utata na sasa Chama cha Wananchi (Cuf) ambacho ni chama kikuu cha upinzani kimeanza kupaza sauti kuhusu maumivu kinayoyapata.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui.

Chama hicho sasa kinasema kimechoshwa na maumivu kinayoyapata yanayotokana na vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui, anataja baadhi ya vitendo hivyo kuwa ni pamoja na kuvunjwa ofisi zao na kuchukuliwa bendera.

Anataja moja ya ofisi iliyovunjwa kuwa ni ile iliyopo eneo la Dunga na kwamba hatua hiyo haina faida katika siasa za visiwa hivyo.

Anasema msimamo wa chama hicho kukataa kushiriki katika uchaguzi wa marudio kama ilivyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), siyo kosa.

Mwanasiasa huyo anasema hilo ni jambo la hiari na mtu ama chama kisipolifanya haliwezi kuwa kosa kisheria na hicho kisiwe kigezo cha chama au mwananchi yeyote kuhujumiwa ama kushambuliwa.

Anasema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kisiwe na wasiwasi kuhusu suala la uchaguzi kwa kuwa baada ya wao Cuf kukataa marudio ya uchaguzi hakuna chama kingine chenye uwezo wa kushinda Zanzibar zaidi ya CCM.

Chama hicho kinawakataza wafuasi wake kutokaribia katika vituo vya kupigia kura wakati wa uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Machi 20, na kuwasisitiza kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi na maendeleo.

“Niwaambie CCM msiwe na wasiwasi mtashinda tu katika uchaguzi wenu wa Machi 20, kwani vyama mnavyoshindana navyo havina uwezo wa kushinda wala kupata asilimia moja ya kura na wala msijipe hofu sisi hatushiriki uchaguzi huo kwani tayari uchaguzi umeshafanyika tokea octoba 25 mwaka jana ambao ulikua huru na haki,”anasema.

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Hamad Masoud Hamad, anasema itikadi za vyama itarigharimu eneo la visiwa vya Zanzibar.

Anasema yapo mambo mengi yameandaliwa katika uchaguzi wa marudio ikiwemo kuwadhalilisha na kuwapiga wafuasi wa CUF hasusani kisiwani Pemba.

Mwenyekiti wa wilaya ya kati wa Cuf, Khamis Kombo anasema wamechoka kuvumilia vitendo wanavyofanyiwa wafuasi wao kwa kuwa havikubaliki kisheria.

Anasema hujuma zote zinazofanywa visiwani humo dhidi ya Cuf, wanaoumia ni wananchi wa kawaida lakini siyo viongozi wa chama hicho ngazi ya juu.

Anaongeza kuwa kibaya zaidi kwa sasa Cuf imeshindwa hata kutoa taarifa polisi kuhusu matukio hayo kwa kuwa hakuna mtu anayewasikiliza.

“Tukio hili la kuvamiwa na kuvunjwa ofisi zetu tumeripoti polisi lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na jeshi la polisi,”anasema .

Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi anasema matukio mengi yanayotokea katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika maskani na mabaraza ya Cuf huwa yanakosa ushahidi.

Anasema wahalifu wanatumia mwanya wa kisiasa kwa kufanya vitendo vya hujuma ili kuonekana kuwa chama kimoja ndicho kilichofanya uhalifu dhidi ya chama kingine.

Msangi anasema polisi wanaendelea kudhibiti uhalifu hasa katika kipindi hiki ambacho Wazanzibari wanasubiri uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Uchaguzi katika visiwa hivyo unarudiwa baada ya ule uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana kufutwa na ZEC.
ZEC ilifuta uchahguzi huo kwa madi kwamba ulikuwa umetawealiwa na kasoro nyingi zikiwamo za kuwapo majina ya wapigakura kuliko wale waliojiandikisha kwenye daftari .

Hatua hiyo ya kufuta uchaguzi imeendelea kupingwa na wadau mbalimbali hapa nchini, lakini ZEC imekataa kusikiliza maoni hayo na sasa imeandaa uchaguzi wa marudio.

Habari Kubwa