Kwa sheria hizi mlungula unapitaje uchaguzi mkuu? (2)

16Sep 2020
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Kwa sheria hizi mlungula unapitaje uchaguzi mkuu? (2)

UCHAGUZI ni mchakato unaosimamiwa na sheria ili kudhibiti udanganyifu na mbinu mbalimbali za kuwavuta wapigakura iwe kuwaahidi ajira, nyadhifa na hata misaada ya pesa.

Kila kinachopokelewa wakati wa uchaguzi ili kujenga mazingira ya kupata kura au kupata upendeleo wa aina yoyote huchukuliwa kuwa ni rushwa. Ndiyo maana kuna sheria zinazokataza kutoa hongo, lakini kwenye uchaguzi hali ni shwari? Wagombea hawawalipii nauli wapigakura?

Vipi taarifa kuwa mgombea fulani anawaandalia wapigakura au wajumbe chakula na vinywaji? Sheria zinasemaje? Makala hii iliyoanza tangu wiki iliyopita inaangaza sheria, uwapo wa rushwa na pengine hatua za kuchukua kuidhibiti.

Kaulimbiu ya Tanzania tangu uhuru mwaka 1961 ni kupata maendeleo na ili kuendelea unahitajika watu ambao ni nguvukazi, ardhi, siasa safi na uongozi bora.Ndiyo maana uchaguzi unafanyika ili kuwapata viongozi bora. Hivyo kwa mujibu wa sheria ni lazima uongozi huo asitokane na rushwa.

Sheria zinalenga kuwezesha uchaguzi uwe huru, wa haki, wa wazi na unaoaminika.

Baadhi ya sheria hizo ni ile ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010 inayokataza kutoa au kusaidia kuwezesha kupata ajira au wadhifa sehemu za kazi kwa lengo la kufanikisha kupigiwa kura.

Inakataza pia kutoa zawadi, mkopo, msaada, ahadi au kitu chochote au kuingia makubaliano na kufanikisha uteuzi kutokana na zawadi, mkopo, msaada, ahadi au makubaliano yaliyoingiwa baina ya mgombea na wapigakura.

Aidha, Sheria ya Gharama za Uchaguzi namba 6 ya Mwaka 2010 inawakataza wagombea kulipa au kuagiza kulipwa fedha ili zitumiwe kwa ajili ya hongo katika kura za maoni au uchaguzi wowote.

Halikadhalika, inaweka jinai kupokea au kukubali fedha, zawadi, mkopo, msaada, ahadi, wadhifa au kitu chochote chenye thamani ili raia apige kura.

Sheria hiyo pia inakataza kutoa au kupokea shukrani baada ya uchaguzi, lakini haishii hapo inazungumzia malipo haramu.

Kifungu cha 22 (a) na (b) kinasisitiza kuwa ni kosa kwa yeyote kwa njia ya rushwa kutoa, kuandaa, kulipa kwa ujumla au sehemu, gharama ya kutoa au kuandaa chakula, kinywaji, burudani au mahitaji ya au kwa ajili ya mtu yeyote kwa madhumuni kumshawishi raia kupiga kura au kuzuia kupiga kura katika mchakato wa uchaguzi.

KUKATAZA KUTOA USAFIRI

Sheria hiyo inakataza kusafirisha wapigakura, yote yakianishwa kifungu cha 23 (1) (a), (3) na 23 (4): Inakatazwa mgombea au wakala na chama cha siasa kuwasafirisha wapigakura kwenda au kutoka kituoni kwa kukodi gari, chombo cha majini, mnyama au usafiri wa aina yoyote ile kwa kuwatolea nauli.

MAKATAZO MENGINE

Kununua au kuuza kadi ya mpigakura ili kumzuia kupiga kura. Aidha, inakataza kutoa rushwa kwa mgombea ili kumshawishi ajitoe kwenye kugombea.

Sheria pia zinakataza mgombea kuomba au kupokea rushwa ili ajitoe kwenye mchakato. Pia kutoa rushwa ili kuteuliwa kugombea, kuomba au kupokea rushwa ili kumteua mgombea.

Kushawishi au kupokea rushwa ili kumpigia kura mgombea fulani au kuacha kupiga kura, yote yanakatazwa na sheria hiyo.

MAKOSA YA RUSHWA

Makosa ya rushwa katika uchaguzi yanatajwa na sheria hiyo kuwa ni kutoa mlungula kwa mpigakura ili kumshawishi kumpigia kura mgombea fulani au kuacha kupiga.

Kutoa takrima, hongo ili kupindisha sheria, kanuni na taratibu za uandikishaji wapigakura, uendeshaji wa kampeni, upigaji wa kura au utangazaji wa matokeo ya uchaguzi.

Makosa mengine ni kuomba au kupokea hongo ili kupindisha au kufumbia macho sheria, kanuni na taratibu za uandikishaji wapiga kura, uendeshaji wa kampeni, upigaji wa kura au utangazaji wa matokeo ya uchaguzi.

Kutoa hongo, kukirimu au kushawishi kunakohusisha wajumbe au maofisa wa usimamizi wa uchaguzi.

Ofisa Habari wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU), Kirumbi Matai, anasema taasisi hiyo ndiyo inayodhibiti, kuzuia na kupambana na rushwa kwa kuuelimisha umma athari ya rushwa kwenye uchaguzi na faida za kuwa na uchaguzi huru.

Aidha, anasema wananchi wanafahamishwa na kuelimishwa kuhusu kuthamani kura, nafasi na wajibu wa mwananchi kukataa na kukabili vitendo vya rushwa katika uchaguzi.

“Tunafanya utafiti wa mchakato wa uchaguzi kanuni na taratibu kubaini mianya ya rushwa na kupendekeza jinsi ya kuiziba.” Anasema Matai.

KWANINI KUNA RUSHWA?

Licha ya sheria, TAKUKURU na wadau wa uchaguzi kuwaelimisha wananchi kuhusu thamani ya kura kuwa ni mkataba wa kumuajiri mwanasiasa kwa miaka mitano, wananchi wanaendelea kuthamini ‘kitu kidogo’.

Kura inathaminishwa na bidhaa inalipwa kwa njia ya rushwa inayotolewa kwa mpigakura. Wengi wanapokea khanga, fulana, madera, chakula, fedha bila kujua kuwa thamani ya kura ni kubwa isiyoweza kupimika.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Sabatho Nyamsenda, anasema kuwapo kwa rushwa kwenye uchaguzi ni matokeo ya mfumo wa kiuchumi wa ubepari ‘neo liberalism,’ unaogeuza kila kitu kuwa bidhaa ikauzwa na kununuliwa sokoni na kwamba hata uchaguzi pia hugeuzwa kuwa gulio la kisiasa, ambapo mwanasiasa ndiye mteja na mpiga kura ndiye muuzaji na bidhaa inayouzwa ni kura.

“Kwa maana hiyo, kura hupoteza thamani (use value) na kubakia kuwa bidhaa yenye bei au exchange value, tatizo hili lipo katika hatua zote za uchaguzi, tangu kura za maoni ndani ya vyama vya siasa hadi katika uchaguzi mkuu wenyewe.”.

Kwa hiyo licha ya kuwapo sheria suala la “mkono mtupu haulambwi” au “penye udhia penyeza rupia.” Ni mambo yanayotawala fikra za wapigakura ambao wanaamini kuwa ni lazima kutoa kitu ili mtu apate kura yake.

UNAHITAJIKA UTAFITI

Pengine ni wakati wa wadau kufanya utafiti na kuona kitu gani kinachowafanya wapigakura na wengine wanaoshiriki uchaguzi kuona kuwa ni lazima wapate pesa au kitu kwanza ili wamchague mgombea? Kwanini wajione kuwa wanahitaji kulipwa?

Wawe wajumbe wa kupitisha majina ya wagombea, wahamasishaji wapigakura na makundi mbalimbali ya kijamii ni sababu zipi zinazowavuta watake kupewa pesa na vitu na wagombea wa uongozi?

Huenda marupurupu manono na malipo makubwa wanayopata wanasiasa yakawa sababu ya kuwafanya wapigakura kuona kuwa wagombea ni mabilionea wanaoweza kuwapa pesa na vitu kwa vile kuwa mwanasiasa ni sawa na kumiliki kisima cha mafuta au utajiri mkubwa.

Habari Kubwa