Kwanini amri za viongozi wa kitaifa hazitekelezwi Zanzibar?

14Feb 2016
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kwanini amri za viongozi wa kitaifa hazitekelezwi Zanzibar?

Pamoja na viongozi wa kitaifa kubanwa kiitifaki na kuwanyima fursa na wasaa wa kuchaganyika na watu wa kawaida, lakini wamekuwa wakifahamu na kupata mambo mengi kuliko wananchi kutokana na kusaidiwa na vyombo vya kimamlaka na kiutawala.

RAIS WA ZANZIBAR DK. ALI MOHAMED SHEIN AKISALIMIANA NA KATIBU MKUU WA CUF, MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD

Kutokana na uongozi kuwa ni dhamana ya kuongoza wananchi, ndiyo maana kila penye tatizo la kitaifa mtu wa kwanza kuangaliwa au kuwajibika huwa ni kiongozi wa kitaifa kabla ya wasaidizi wake.

Hata hivyo, kuna matatizo yameanza kujitokeza kwa muda mrefu ya kutoheshimika maagizo na amri zinazotolewa na viongozi wa kitaifa kwa manufaa ya wananchi na maendeleo yake.

Inapotokea amri au maagizo ya viongozi kupuuzwa na kutotekelezwa huwa ni udhaifu na dosari mbaya katika kuthamini dhana ya utawala bora na kupwaya kwa nidhamu, utii na uzingatiaji miiko ya uongozi na utendaji.

Matatizo hayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya watendaji wa serikali na kusababisha wananchi kuishutumu serikali na mambo kubaki palepale, licha ya viongozi kutafuta njia ya utatuzi kwa kutoa maagizo na maamuzi.

Septemba 2012, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa amari ya kuondosha michago katika upatikanaji wa huduma za uzazi kwenye hospitali na vituo vya afya vya serikali kutokana na wananchi wengi kushindwa kuzimudu kabla ya kujifungua.

Michango hiyo ya gharama za tiba na vifaa ilionekana kama mateso mara mbili kwa kinamama wanaojifungua kwa upasuaji, kutokana na gharama kubwa ya upatikanaja wa vifaa tiba.

Uamuzi huo ulipokelewa kwa furaha kubwa na wananchi huku wakiamini Rais wao amesikia kilio cha wanyoge baada ya kutoa amri wapatiwe bure huduma hizo.

Hata hivyo, utekelezaji wa agizo hilo umekuwa ukifanywa kwa kuchechemea na kusababisha malalamiko ya wananchi kubaki vile vile, hali inayotafsirika na wananchi wengi kwamba Rais wao amekosa kuheshimiwa.

Kwa madhumuni ya kuondoa kero kwa wananchi, Januari 12, 2013 Rais Dk. Shein alitangaza rasmi kuondoa michango katika sekta ya elimu kwa wanafunzi wa ngazi ya maadalizi, msingi na gharama za mitihani kwa wanafunzi wa sekondari.

Lengo kubwa la kuondosha michango hiyo ni kuendeleza misingi na malengo ya Mapinduzi ya kutoa elimu bure kwa wananchi wa Zanzibar, ili kunufaisha wananchi wengi wakiwemo wanyoge.

Hata hivyo, wanafunzi wakiwemo kutoka familia za wanyoge, wamendelea kutozwa michango. Baadhi wameshindwa kumudu na kuwapa wakati mgumu wanafunzi na wazazi.

Aidha, mwezi uliopita Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar alipiga marufuku walimu kudai michango baada ya tatizo hilo kuendelea kujitokeza na kuwaumiza wazazi wasiokuwa na uwezo.

Pamoja na Wizara yenye dhamana kujitetea kuwa wakati mwengine wanashindwa kutekeleza maagizo au maamuzi ya viongozi wa kitaifa kutokana na mahitaji kuwa makubwa kuliko bajeti, wakati umefika amri wa maagizo ya viongozi kutekelezwa kwa wakati ili kutowafedhehesha mbele ya jamii.

Katika matumizi ya fedha za umma, kuna huduma ambazo zinahitaji kupewa vipaumbelele kutokana na umuhimu wake kwa wananchi kama upatikanaji wa matibabu, elimu na huduma za maji safi.

Ni kweli kuwa mwalimu makini hawezi kuacha watoto wasisome kwa sababu ati ya ukosefu wa chaki wakati kuna wazazi wana uwezo wa kuchagia na watoto wa wanyoge wakanufaika; ndiyo maana michango imekuwa ikiendelea kukithiri licha ya kutolewa amri ya kufutwa.

Ni kweli, pia, daktari makini hawezi kuacha kumfanyia upasuaji mama mjamzito kwa sababu eti ya ukosefu wa vifaa tiba wakati mhusika ana uwezo wa kununua ili kuokoa maisha yake na kiumbe kilichomo tumboni, na ndiyo sababu michango inaendelea.

Lakini wakati umefika watendaji wakuu kutekeleza kwa vitendo maagizo ya viongozi wa serikali wa kitaifa kwa madhumuni ya kuondoa kero na hasara wanazopata wananchi, hasa wanyonge wakati viongozi hao tayari wameonyesha nia ya kuwatatulia wananchi matatizo yanayowakabili ili kuweka sawa hali ya upepo Zanzibar.

Habari Kubwa