Kwanini India inachukulia ngono kwa ahadi ya kuoa ni ubakaji?

14May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kwanini India inachukulia ngono kwa ahadi ya kuoa ni ubakaji?

IWAPO mwanamume atashindwa kutimiza ahadi ya kumuoa mwanamke, ngono baina ya wapenzi wawili walioelewana inaweza kuchukuliwa kama ubakaji?

Mahakama ya ngazi ya juu zaidi nchini India, imetoa jibu la swali hilo na kusema kuwa ni “ndio.”

Katika uamuzi muhimu, Mahakama imepitisha uamuzi wa Mahakama ya Awali na kumtia hatiani daktari mmoja kwa kosa la ubakaji katika Jimbo la Kati la India la Chhattisgarh.

Hiyo ni kwasababu alikuwa na makubaliano ya uhusiano wa kingono na mwanamke baada ya kumuahidi kuwa atamuoa, lakini hakutimiza baadaye ahadi hiyo na kumuoa mtu mwingine.

Majaji L Nageswara Rao na MR Shah walisema mwanamke alimruhusu daktari kufanya naye ngono kwasababu aliamini kwamba alikuwa na lengo la kumuoa kwa hiyo haiwezi kuchukuliwa kuwa alimruhusu kufanya tendo la ngono kwa hiari.

Bado India ni taifa lenye itikadi za kihafidhina linapokuja katika suala la ngono na mambo yanayohusu jinsia kwa ujumla.

Mabikra huzawadiwa na mwanamke anayejulikana kuwa aliwahi kufanya tendo la ngono nje ya ndoa, huwa inakuwa vigumu kwake kuolewa.

Majaji walisema kwamba mshtakiwa alikuwa na “lengo la wazi” la kutomuoa, na kuongeza kuwa “tendo la ngono linalofanyika bila dhana halisi, haliwezi kuchukuliwa kama hiari.”

Hata hivyo, Mahakama ilipunguza kifungo cha miaka 10 alichokuwa amefungwa na Mahakama ya Mwanzo na kumpa adhabu ya kifungo cha miaka 7 jela.

Majaji wamesema kwamba “ni lazima akabiliwe na athari za uhalifu alioutekeleza.”

Hii si kesi ya kwanza kwa mujibu wa data za serikali za mwaka 2016.

Polisi walirekodi kesi 10,068 za aina hiyo za ubakaji “zinazofahamika kama za waathiriwa wa ahadi ya kuolewa.” Mwaka 2015, idadi ya kesi hizo zilikuwa ni 7,655.

Majaji wa Mahakama ya Juu zaidi ilishauri Mahakama za Mwanzo “kuchunguza kwa makini ikiwa kweli mwanamume aliahidi kumuoa muathiriwa au kulikuwa na njama nyingine tangu mwanzo na kwamba alifanya tendo la ngono kwa lengo tu la kuridhisha nafsi yake.”

Hii ina maana kuwa kama mwanamume atathibitisha kuwa kweli alitaka kumuoa mwanamke lakini akabadili nia hiyo baadaye, bado haitakuwa ubakaji.

Haichukuliwi kama ubakaji ikiwa itabainika kuwa alikuwa na njama mbaya tangu mwanzoni mwa mahusiano yao.

Lakini kama kweli tendo hilo lilifanyika kwa “lengo fulani” si rahisi kuthibitisha, na uamuzi huachiwa majaji na pia kuna hofu kuwa sheria hiyo inaweza kutumiwa isivyotarajiwa.

Na ukweli ni kwamba, kutokana na idadi kubwa ya kesi hizo, Jaji Pratibha wa Mahakama ya Juu ya Delhi, alisema mwaka 2017 kuwa wanawake hutumia sheria za ubakaji wakati wanapokuwa na mahusiano mabaya ya ndoa.

“Mahakama hii imeshuhudia mara kadhaa idadi ya kesi ambapo watu wote wawili, kwa utashi wao na kwa kupenda kwao, huanza uhusiano wa kimwili…sasa wakati uhusiano unapovunjika kwa sababu fulani, mwanamke anatumia sheria kama silaha ya kumuadhibu mwenzi wake,” anasema Jaji na kuongeza:

“Huwa wanatumia kitendo walichokubaliana kama matukio ya ubakaji labda kutokana na hasira na kuchanganyikiwa, na hivyo kupotosha lengo halisi la sheria zenyewe.”

Jaji anasema hii inahitaji kuwapo na mipaka ya wazi kati ya ubakaji na ngono ya makubaliano, hususan wakati ambapo malalamiko ni kwamba mwanamke aliahidiwa kuwa ataolewa.

Wahindi wengi wanaamini kwamba sheria za ubakaji, hazipaswi kutumika kudhibiti mahusiano ya kujamiiana, hususan katika matukio ambapo wanawake wana wakala na wanaingia katika mahusiano kwa utashi wao.

Wengi katika Mahakama pia wanaonekana kuwa na maoni sawa na haya na kwa kiasi fulani inaelezea ni kwanini idadi ya watu wanaopatikana na hatia kwa kosa hili huwa ndogo na katika kesi nyingi mshtakiwa huondolewa mashtaka.

Mengi kati ya malalamiko ya ubakaji wa kutelekezwa na wapenzi wanaowaahidi kuwaoa hutoka katika familia maskini katika maeneo ya vijijini

Mnamo mwaka 2016, Mahakama Kuu ya Bombay ilisema kuwa mwanamke msomi mtu mzima ambaye alikuwa na mahusiano ya ngono ya kukubaliana, baadaye hawezi kudai amebakwa uhusiano unapokuwa mbaya.

Wakili wa ngazi ya juu na mwanaharakati mwenye makao yake Mumbai, Flavia Agnes, hata hivyo anadai kuwa kile tunachopaswa kukikumbuka ni kwamba mengi kati ya malalamiko haya hutoka katika familia maskini na wanawake kutoka jamii zenye matatizo katika maeneo ya vijijini.

Anasema wanawake hao mara nyingi hulaghaiwa kuingia katika mahusiano ya ngono na wanaume wanaowapa ahadi za uongo za kuwaoa na baadaye kuwatelekeza mara wapatapo ujauzito.

Aliongeza kuwa chini ya mfumo wa sasa wa sheria, sheria ya ubakaji huenda ndio inayoweza kuwasaidia kudai uharibifu au hata kupewa haki yao.

Ndio maana anapendekeza kuwa kipengele cha kutengana chini ya sheria ya ubakaji cha kukabiliana na kesi hizi kitumike badala ya adhabu kali za jela ambapo mwanamume anayepatikana na hatia ya kumlaghai mwanamke anaweza kulipa faini, na kuwajibishwa kwa malezi ya mtoto atakayezaliwa. BBC

Habari Kubwa