Kwanini wanandoa waachane uzeeni?

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kwanini wanandoa waachane uzeeni?

MPENZI msomaji, naamini kwa kudra ya Mwenyezi Mungu umeingia salama mwaka mpya 2019. Sote tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kibali na upendo wake mkuu aliotuonyesha kwa kutuvusha salama.

WANANDOA WALIODUMU KWENYE MAPENZI KWA KIPINDI KIREFU

Mwisho wa mwaka, mara nyingi huwa na pilikapilika nyingi na hasa sherehe mbalimbali zikiwamo harusi, wengine wakibariki ndoa, vipaimara vya watoto, sherehe siku za kuzaliwa na kadhalika. Matukio yote hayo ni ya furaha na nderemo za hapa na pale.

Hata hivyo, wakati hayo yakijiri, wengine humaliza mwaka vibaya yakiwemo matukio ya ajali mbalimbali, kufiwa na wapendwa na zaidi sana wengine wanaachana kwa talaka au kinyemela, huku wengine wakiwa na makusudio ya kuachana uzeeni. Ili mradi tu matukio ya kuhuzunisha.

Leo msomaji wangu nataka tujadili kipengele hicho cha mwisho kwa wale walioachana au wako katika makusudio ya kuachana uzeeni.

Kabla sijaendelea, hebu nikupe kwa mhutasari nini maana ya ndoa. Ndoa ni muunganiko wa mwanaume na mwanamke kuishi pamoja kama mume na mke muda wote wa maisha yao.

Ndoa ni muungano kati ya mwanaume na mwanamke unaokubalika kitamaduni na kidini ambao unatarajiwa kudumu, kuwapa haki sawa za kijinsia na kutosheleza majukumu mengine ya kijamii.

Ili muungano huu uwe kamili ni sharti;- Wanaooana wawe wamekubaliwa napasipo kulazimishwa na mtu. Na kwa mtazamo mwingine, ndoa ni ya mwanaume na mwanamke, ndoa ni agano la kudumu la maisha na ndoa ni tendo la heshima mbele za Mungu.

Pia ni agano kati ya mume na mke au ni mkataba wa kiungu kati ya mume na mke waliokubaliana kuishi pamoja. Ndoa ni jambo la kiroho. Ndiyo maana maandiko yanasema;-

Marko 10:6-9  “Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa siyo wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, wanadamu asikitenganishe”.

Kwa mantiki hiyo, mke na mume wanapooana, wanakuwa mwili mmoja. Lakini siyo mwili mmoja wa damu na nyama, bali ni mwili mmoja katika roho. Kuwa mwili mmoja maana yake ni kwamba ni kuwa na nafasi moja, wazo moja na ni kuwa na mawasiliano ya karibu kwenye ulimwengu wa roho (mtandao katika ulimwengu wa roho) kati yako na mumeo.

Haiwezekani mwanaume apate tatizo na mwanamke asifahamu kama wanayo mawasiliano ya karibu kati yao. Kumbuka mwanamke ni mlinzi wa mwanaume. Yeremia 31:22…”Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanaume”.

Mpenzi msomaji, andiko hilo la Mungu limezungumzia habari ya ulinzi, kwamba mwanamke atamlinda mwanaume. Hii ikimaanisha kwamba mwanamke anapompiga kisogo mwanaume, tayari anakuwa hana ulinzi, lazima ataishi kwa hofu, maisha yatayumba na hatakuwa mtu wa furaha hata kama atajitutumua vipi.

Hii imedhihirika wazi pale wanandoa wanapotengana au kuachana kwa sababu mbalimbali. Kumbuka hata kwenye tafsiri ya ndoa hapo juu nimesema ndoa ni pale mke na mume wanapooana na kuwa mwili mmoja. Kwa mantiki hiyo, mmoja anapochepuka, tayari ndoa imepata dosari.

Mwaka ulioisha, imeshuhudiwa mitikisiko mingi ya ndoa. Mifano ilidhihirika pale wanandoa wanapokutana katika matukio ya ama kuozesha vijana wao au kuoza binti zao.

Kwa maneno mengine vijana wanapofunga ndoa, ndipo wazazi wao hujikuta wakilazimika kuwa pamoja katika matukio hayo lakini baada ya hapo kila mmoja hutawanyika kivyake kwani tayari walishaachana au wako katika hatua za kupeana talaka uzeeni.

Ukiuliza sababu za kuachana uzeeni unaweza kuvunja mbavu kwa kicheko, hazina mashiko! Hizi sababu nitazielezea kwa kina katika sehemu ya pili ya makala haya wiki ijayo. Nikiuliza, Je, nani vinara, wanawake au wanaume na kwanini?

Wanandoa uzeeni ndio wakati wanapaswa kuambatana kwa upendo na furaha na kumshukuru Mungu kwa umri waliofikia. Aidha, wanapaswa kuweka mkwazo kando na kumuomba Mungu awape uzee mwema. Hiyo ndiyo neema na hekima.

Na kwa hakika, ndoa zinazodumu hadi uzeeni ni baraka kwani pamoja na kupitia changamoto mbalimbali zimeweza kuvuka salama hadi katika hatua zilipofikia.

Je, unalo suala la kifamilia/ndoa/mahusiano linalokutatiza? Wasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]

 

Habari Kubwa