Kwanini wanaodhuru raia hawakamatwi Zanzibar

07Feb 2016
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
Kwanini wanaodhuru raia hawakamatwi Zanzibar

HIFADHI ya maisha ni haki ya msingi kwa kila binadamu, ndiyo maana imepewa uzito mkubwa katika katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Kifungu cha 13(1) na (3) cha katiba ya Zanzibar kimesema ‘Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtesa.
Bahati mbaya matukio ya watu kuvamiwa na kupigwa wakiwa katika matembezi au nyumbani yamekuwa yakiongezeaka na kutia hofu wananchi bila ya wahusika kuchukuliwa hatua, licha ya uhalifu huo kufanyika hadharani mchana.
Pamoja na Kifungu cha 12(1) cha Katiba ya Zanzibar kueleza watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulidwa na kupata haki sawa mbele ya sheria, vitendo vya kudhuru raia vinafanyika Zanzibar.
Tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka jana, mikasa ya watu kupigwa bila ya kuwa na sababu na mali zao kuharibiwa yamekuwa matukio ya kawaida visiwani hapa.
Lakini vitendo hivyo vinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria, na kuvuruga msingi wa amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake.
Bado haifahamiki kama matukio hayo ni ajenda ya kisiasa au watu wameamua kufanya uhalifu wa kupiga wengine bila ya kuiba mali wakiwemo wanafunzi.
Alhamisi iliyopita katika mji mdogo wa Jang'ombe Taifa mkoa wa Mjini Magharibi, wananchi walivamiwa saa mbili usiku na kupigwa na watu waliokuwa na silaha za kienyeji, ikiwemo mikanda ya jeshi, bakora na vitu vyenye ncha kali.
Wazee, wanafunzi na kina mama wajawazito walikuwa ndiyo waathirika wakubwa baada ya kushindwa kutimua mbio.
Watu hao waliokuwa wameficha nyuso zao kwa kutumia vitambaa, walipiga watu mitaani pamoja na kila waliyemkuta amepumzika katika baraza yake nje ya nyumba, kama ulivyo utamaduni wa Zanzibar.
Mbali na uharibifu wa mali walizovunja katika maduka ya chips na kusababisha hasara kubwa kwa wahusika walioamua kufunga maduka kutokana na hali ya wasiwasi, pia watu wazima walilalamika kusikia maumivu mwilini baada ya kuchapwa mikanda mgogoni na kwenye makalio.
Mkasa huu umesababisha hali ya wasiwasi na kusababisha baadhi ya familia kupunguza nyendo za matembezi ya usiku, na kulazimika kujifungia mapema nyumbani wakihofia kupigwa.
Pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadama Khamis kueleza jeshi lake limeanza kuwasaka watu waliohusika na shambulio, hilo bado vyombo vya dola vinahitaji kuongeza nguvu na utaalamu katika kuwatafuta wahalifu wa makosa makubwa visiwani Zanzibar.
Tabia ya watu kuendelea kuhujumiwa bila wahusika wa uhalifu kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria na kufunguliwa mashitaka, hakuleti taswira nzuri katika kupambana na uhalifu mkubwa na wenye hatari kwa amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake.
Shambulio la Jang'ombe Taifa limetanguliwa na tukio la kuvamiwa kituo cha Radio cha Hits FM na kuchomwa mato sutudio yake.
Kabla ya matukio hayo mawili, viongozi wawili wa dini waliwahi kumwagiwa tindikali na mmoja kuuwawa kwa kupigwa risasi hakiwa katika kazi ya utumishi wa kiroho. Hakuna watu waliokamatwa na kufikishwa mahakamani mpaka sasa.
Pamoja na matukio hayo kuleta athari kubwa ya kimwili na kiafya, watu waliofanya vitendo hivyo wamekwama kwa muda mrefu kupatikana licha ya vyombo vya dola kuwa kazini.
Kwa kuwa serikali ina wajimbu wa kulinda usalama wa raia na mali zao, inapaswa kuongeza nguvu na utaalamu katika kukabiliana na uhalifu huo ili kuondoa tatizo la raia kuhujumiwa ndani ya nchi yao.
Kutokana na mazingira ya kijografia ya Zanzibar na idadi ndogo ya watu, haiwezekani watu waendelee kufanya uhujuma dhidi ya raia bila ya kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Bahati nzuri Zanzibar imebahatika kuwa vikosi vitano vya ulinzi, mbali na vile vya muungano wakiwemo Polisi, Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) hivyo haiwezekani uhalifu dhidi ya raia ukafanyika na wahusika wasipatikane.

Habari Kubwa