Kwanini wengi wanatafsiri Januari mwezi mgumu zaidi

23Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kwanini wengi wanatafsiri Januari mwezi mgumu zaidi

NI mwezi Januari mlango wa mwaka mpya. Ni kipindi chenye ushuhuda wa wazazi wengi wenye watoto wanaumiza vichwa. Huo ni mwezi unagongana na mengi kama vile kulipa kodi ya nyumba, karo za shule kwa watoto.

Kariakoo, jijini Dar es Salaam, eneo lenye pilika nyingi za wazazi na watu wengine wakinunua mahitaji ya kifamilia na binafsi, hususan kati ya mwezi Desemba na Januari, hata ikawaacha baadhi katika hali ngumu kukabili mahitaji makuu ya mwezi huu. PICHA: MTANDAO

Hapo ndipo wazazi nao wameubatiza majina ya kila aina, ikiwamo ‘mwezi mrefu usioisha’ na ‘mwezi mmoja ndani ya miezi mitatu’ na mengine mengi.

Kupitia swali hilo gumu, ndipo gazeti la Nipashe liliamua kutafuta majibu kutoka kwa wanajamii undani wa Januari kuwa ‘pasua kichwa’ na gumzo kwao, kuliko miezi mingine.

Yanayomkabili mzazi yanajumuisha baadhi ya malipo kama karo za shule ambazo hata hivyo hazilipwi mara moja, kununua vifaa vya shule kama daftari, sare za shule na kwa wanaoenda bweni bajeti inatanuka.

Pia magumu mengine ya Januari ni hali ya hewa, jua kali ikiambatana na joto, bidhaa kupanda bei pamoja na ukosefu wa pesa.

WADAU

Mama Evance, mkazi wa Mbezi Makabe, Dar es Salaam mwenye mtoto wa darasa la sita mjini humo ana ufafanuzi:

“Unajua mwezi Januari wengi wanauona ni mgumu, kwa kuwa asilimia kubwa ya wazazi wanatumia pesa vibaya mwezi Desemba kutokana na sikukuu hizi mbili Krismasi na Mwaka Mpya.’

“Wanasahau kwamba kuna jukumu kubwa la kulipa karo za watoto kwa mwezi Januari, matokeo yake inapofika wanajikuta wanahaha kutafuta pesa kwa ajili ya karo na kujikuta wanachukia mwezi Januari.”

“Kwa kuwa huwa naweka mipango mapema naona mwezi Januari ni mwezi wa kawaida kama miezi mingine,” anaongeza.
Mzazi wa mtoto anayesoma katika shule ya sekondari binafsi iliyoko wilaya jirani ya Bagamoyo, Mama Junior, anayeishi Mbweni, Dar es Salaam, katika mada hiyo naye ana hoja anayounganisha na maswali:

“Unajua mimi naweza kusema kuwa wazazi wengi wa kitanzania wanaishi bila mipango, maana suala la elimu na kodi za nyumba sio suala la kushtukiza kama msiba au ugonjwa, ni suala linalojulikana tangu unapoleta mtoto duniani.

“Kwanini usiwekeze pesa kidogo kidogo kwa ajili ya elimu ya wanao? Lakini cha ajabu wengi wanawekeza katika mambo yasiyo na maana, matokeo yake inapofika Januari watu ‘vijasho’ vinawatoka, lakini unajiuliza hivi hawa watu hawakujua kwamba mwezi Januari ni majukumu muhimu?”

Mwingine anasema asilimia kubwa ya Watanzania hawana nidhamu na utamaduni wa kutunza pesa, kwa kuzielekeza katika yasiyo ya lazima katika maisha yao.

“Anaweza kuwa na pesa aliyotunza kwa sababu ya karo au kodi ya nyumba, lakini anaposikia kuna sherehe mahali fulani au kuna nguo nzuri kaipenda anaitumia bila kufikiria kwamba hakuna sehemu yoyote atakakopata ili kurudishia ile pesa.

“Kwa kifupi maisha ya watu wengi ni ya kubahatisha na wanaishi bila nidhamu hata kidogo. Hakuna mzazi asiyejua kama anasomesha na kujua kiasi cha ada ya mwanawe au wanawe kwa mwaka,” anasema.

Mwalimu Msesa kutoka Shule ya Msingi Miembe Saba, Kibaha mkoani Pwani, anachangia: “Kwanza mwezi Desemba, hasa walio kwenye sekta ya kuajiriwa wanalipwa mshahara mapema sana.

“Hivyo, pesa nyingi hutumia kwenye sikukuu na mwezi Januari ni mwezi wa kulipa karo za watoto asilimia 90, wanabana pesa kuelekeza kwenye elimu, hivyo biashara nyingi sana haziendi na kusababisha kukosa mzunguko wa pesa kwenye mfumo.

Anasema ni hali ya kawaida, watu wakilalamika sana mwezi Januari kwa kuwa na uhaba wa pesa na huwa ngumu hata kuendesha sherehe kwa kutegemea michango ya watu.

“Kwa kuwa asilimia 70 ya watu wanakuwa na uhaba wa pesa mwezi huu kwa kiwango kikubwa sana, ukitofautisha na miezi mingine ndani ya mwaka husika,” anasema Mwalimu Msesa.

MITANDAONI

Hata kwenye mijadala ndani ya mitandao ya kijamii, mfano ‘twitter’ na ‘WhatsApp’ wazazi wengi wanajadili namna shule nyingi nchini zinagoma kupokea mtoto shuleni, pasipo kutanguliza ada kwa kiasi fulani cha makubaliano.

Ni sura ya mijadala inayoangukia pia kuthamini mahitaji ya shule kama vifaa vya kujifunzia na kodi za  nyumba. Baadhi ya mijadala inapendekeza, ni vyema  wazazi wanaosomesha watoto kuweka akiba katika taasisi fedha kama benki, kwani shule nyingi zina utaratibu wa kulipa karo kwa njia ya benki.

Pia katika  kuepusha changamoto za kukosa karo na vifaa muhimu vya wanafunzi, kuna wazazi wanaowashauri wenzao kuweka mipango endelevu ya kuweka akiba kwa ajili ya karo na kodi za pango.

Wanasema ni mbadala chanya kuwaepusha wazazi  na adha ya kukosa mahitaji kama kodi za nyumba na ada za watoto shuleni, kwani matarajio ya wamiliki wa shule na nyumba kupokea kodi na ada kwa muda mwafaka.

Ni mjadala pia unaoangukia tabia binafsi, wazazi kukumbushwa kukabiliana na majibu hasi kuhusu malipo ya madeni dhidi yao.  

SAFARI IJAYO

Ukiwa ni mwanzoni wa mwaka mpya 2021, jamii inatakiwa kujitathmini na kuzingatia kuishi kwa malengo, ili kuondokana na dhana potofu ya kuhisi kwamba, Januari ni mwezi mgumu na unaochelewa kuisha.

Ni kanuni inayoelezwa pale inapopangwa mambo kwa uangalifu, iko bayana utafanana na miezi mingine kwa sababu ‘makandokando’ yake yanakuwa yamekabiliwa.

Pia mwaka 2020 unakumbukwa, janga la maradhi ya corona liliyumbisha wengi kwa mengi. Kiuchumi, akiba binafsi ziliyumba kwa kiasi kikubwa cha fedha walitumia kujikimu na familia zao.

Hapo ina maana gani? Hata wamiliki wengi wa shule wategemee wazazi wengi hawako sawa kiuchumi na si ajabu kasi ya malipo kusuasua.

Wapo waliopoteza kazi za vipato vyao, kutokana na janga hilo na wafanyabiashara wengi waliotegemea mali kutoka nje ya nchi, hawakuzipata. Yote yanaifanya Januari 2021 mwezi mgumu zaidi, kuliko nyinginezo.

Lakini, kwa sababu ni lazima maisha yaendelee, watu nao wanapaswa kujifunza nidhamu kubwa ya kutunza pesa. Ni wakati wa kubadilika.

Hivyo, mwaka 2020 umeacha darasa na nidhamu kubwa kwa wazazi na watu wengi waliozoea kuchukulia mambo yataenda kirahisi kila wakati na kama walivyopanga.

Kuna chumba cha kujifunza kwamba kuna dharura yoyote inaweza kutokea kama janga la corona lilivyopiga hodi mwaka jana.

Habari Kubwa