Kwasi: Beki kinara  wa utupiaji Ligi Kuu 

04Dec 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Kwasi: Beki kinara  wa utupiaji Ligi Kuu 

WENGI wanadhani kuwa alibahatisha alipomfunga Aishi Manula bao safi la mkwaju wa faulo lililoipa timu ya Lipuli sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba Jumapili ya Novemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Beki wa Lipuli, Asante Kwasi (kushoto), akimdhibiti straika wa Simba, John Bocco, asilete madhara kwenye lango lake kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopigwa hivi karibuni kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Saam na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Hiyo ni kwa sababu mashabiki wengi nchini huwa wanazifuatilia zaidi mechi zinazozihusu Simba na Yanga zaidi.

Mchezaji wa timu nyingine atakayewika kwenye mechi kati ya timu hizo mbili, basi kila shabiki atamjua siku hiyo.

Asante Kwasi, beki wa Lipuli, haikuwa mara yake ya kwanza kufunga mabao ya aina hiyo.  Kwenye orodha ya wafungaji bora anaonekana ana mabao matano, akiwa sambamba na Ibrahim Ajibu wa Yanga na Shiza Kichuya wa Simba.

Hata hivyo, kiuhalisia ni kwamba beki huyo raia wa Ghana amefunga mabao manne, huku moja linalohesabika kuwa la tano kwake, akiwa amejifunga.

Beki huyo wa kati mwenye matumizi mazuri ya nguvu na akili, alisajiliwa msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Mbao FC ya Mwanza.

Baadhi walianza kumjua tangu msimu uliopita akiwa na Mbao FC, hasa alipokuwa kikwazo timu hiyo ilipocheza na timu za Simba na Yanga.

Ndiye beki pekee kwenye Ligi Kuu mwenye mabao mengi zaidi, akiwashinda hata baadhi ya mastraika wa timu mbalimbali nchini.

"Juhudi binafsi na kujituma zimenipa nafasi ya kufunga mabao niliyonayo hadi sasa na kuwazidi washambuliaji wengi wa Ligi Kuu hapa nchini," anasema Kwasi na kuongeza.

"Ingawa kazi ya kufunga ni ya washambuliaji, lakini na mimi kama beki nina wajibu wa kwenda mbele kusaidia na kutumia nafasi zinazopatikana," alisema beki huyo.

Anasema matarajio yake ni kuendelea kujituma zaidi ili kufunga mabao mengi zaidi.

"Nataka kufunga mabao mengi zaidi msimu huu, najua ligi ni ngumu msimu huu kwa sababu kila timu imejipanga kupata ushindi na timu itakayozubaa inapoteza mchezo," anasema.

Kwasi alianza kufunga mabao Septemba 30 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara wakati timu yake ikicheza dhidi ya Ndanda.

Kwenye mechi hiyo ambayo wenyeji walishinda mabao 2-1, Kwasi akifunga bao la kufutia machozi la Lipuli kwa mkwaju wa faulo, lakini akijifunga bao moja na Ndanda ikaondoka uwanjani na ushindi.

Novemba 5, alifunga bao kwa mkwaju wa penalti, Lipuli ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa, kabla ya kufunga bao lake la nne msimu huu Oktoba 29 kwa mkwaju wa penalti akiibeba timu yake ya Lipuli kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu yake ya zamani, Mbao FC.

Kwenye mechi dhidi ya Simba alifunga bao kwa mkwaju wa faulo na kuwa la tano kwake msimu huu kiasi cha kuifanya timu hiyo ya Msimbazi kummezea mate na kuingia katika mchakato wa kumsajili kwenye kipindi hiki cha dirisha dogo.

 

Habari Kubwa